TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA -- 35
Na Steve B.S.M
Mitchelle aliirejesha simu yake kwenye mkoba lakini bado hakujua afanye nini, alipatwa na butwaa lililomshika miguu akasimama hapo alipo kana kwamba sanamu, akiwaza na kuwazua, mambo kama mia moja katika kichwa chake yakienda na kurudi, yakijiuliza na kujipatia majibu yenyewe, kwa mara ya kwanza alijikuta katika hali ya kutoelewa chochote kinachoendelea, ubaya hakuwa na muda wa kujadili zaidi na nafsi yake, akakata shauri kurudi ndani, alipoingia tu mlangoni akakutana na wanaume wawili waliovalia nguo za wahudumu, mikononi wamebebelea bunduki, nyuso zao ngumu kama roho zao, wakamchukua na kuongozana naye mpaka ukumbini ambapo mnada ulikuwa unafanyikia, huko akakuta watu wote ukumbi mzima wamewekwa chini ya ulinzi mkali, wale waliokuwa wahudumu ndo' hao wamebebelea bunduki badala ya trey za vinywaji.
Mbele ya ukumbi alikuwapo bwana yule mnene, kipande cha mtu, mikono yake iko mifukoni, pembeni yake wamesimama wanaume wawili waliobebelea bunduki nzito, mwanaume huyo alikuwa anamtazama Mitchelle akiwa ameupinda mdomo wake mdogo, Mitchelle aliposogezwa karibu naye aligunia puani kwa kebehi alafu akasema, "Ndio wewe!" Kisha akacheka.
"Leo ni siku ya namna gani!" Akasema, "Leo ni siku ambayo nchi ya Taiwan haitakuja kusahau kamwe!"
Akamsogelea Mitchelle kwa mwendo wa taratibu, Mitchelle akamtazama kwa macho ya hasira alafu akamuuliza, " wako wapi watu wangu?"
Bwana huyu mnene akacheka, akacheka tena, akacheka mpaka kifua chake kikamuuma akipaliwa na mate, alipotulia akauliza huku akiwa na macho yanayolengwalengwa na machozi ya furaha, "watu wako? Watu gani?" Akaigiza kama mtu anayefikiri alafu akasema, "watu wako? Oh! Unamaanisha Dr. Lambert na Jennifer?" Akatabasamu, "hao ndo' watu wako?" Akauliza kwa kebehi, punde wakatokea Jennifer na Dr. Lambert wakitokea nyuma ya jukwaa, walikuwa wamevalia nadhifu, Jennifer alikuwa yu ndani ya suti ya kahawia wakati Lambert akiwa amevalia suti nyeusi isiyokuwa na tai, watu hao walisimama kando ya bwana huyu mnene wakamtazama Mitchelle kama mtu mgeni mbele ya macho yao.
"Jennifer!" Mitchelle aliita, na pasipo Jennifer kusema jambo Mitchelle akawa ametambua ya kwamba mwanamke huyo hakuwa upande wake, vilevile Dr. Lambert, lakini kwanini? Hakuwa anajua chochote, kila kitu kilikuwa 'surprise' hapa, Jennifer akampungia mkono akitabasamu akajikuta anapatwa na hasira za ajabu, hasira za usaliti, akataka kujifaragua lakini bwana Lambert akamsihi asifanye hivyo kwani atajiumiza mwenyewe, hapa Mitchelle akatabasamu alafu akasema,
"Dokta, umenisahau? Unadhani hawa wanaweza kunizuia mimi?"
"Najua hawawezi," Dokta akajibu na kuongezea, "ndo' maana mimi nipo hapa." Akatoa kifaa fulani mfukoni mwake na kusema, "huu ndo' mwisho wako, Mitchelle, ni muda wa kulipia dhambi zote ulizozifanya."
Dokta akaenda mbele kwa kumweleza ni namna gani alikuwa anapandikiza vitu vyake katika 'antidote' alokuwa anampatia, na kama haitoshi namna gani walivyokula njama pamoja na Jennifer kwenye kumpandikizia vitu vya ziada katika kahawa yake.
"Vitu vyote ulivyokuwa unatumia na kukusababishia uraibu vilikuwa ni zao la mikono yangu, hiyo ndo' ilikuwa kazi yangu, na kwasababu ulikuwa ni kiumbe kisichokuwa na madhaifu, ilikuwa ni jukumu langu kukutengenezea udhaifu tutakaoweza kuutumia kwenye kukupata na kukumudu."
Mitchelle alijaribu kufurukuta, Dr. Lambert akabonyeza kifaa chake, mara moja akajihisi shoti ya umeme mwili mzima! Kufumba na kufumba alijikuta chini akiwa hajiwezi, hana nguvu kabisa, anahema kama mbwa wa mashindano, hakuwahi kujihisi mdhaifu kiasi hiko maisha yake yote.
"Haikuwa kazi rahisi kufanya hili," Dokta akasema akimkaribia, "na nilijua kwa mwenendo wa kukupatia dawa ingalichukua muda mrefu sana kukamilisha mpango wangu, hapo ndo' kukajenga hitaji la kahawa tamu, kahawa ambayo najua bila shaka umeinywa hata asubuhi ya leo, kwa pamoja vimeleta mafanikio haya."
Dokta alitazama kifaa alichokishikilia mkononi mwake alafu akasema, "huwezi kuishi bila antidote, mwili wako umeshakuwa 'addicted', hautavuka juma moja, vilevile hautaweza kuishi siku zaidi ya tatu bila ya kupata kahawa yako tamu, utapoteza nguvu na kutokomea, mbaya ni kwamba vitu hivi vipo kwenye mikono ya adui yako, sasa yapasa kuwa mtiifu."
Dokta alimkabidhi bwana yule mnene kifaa hicho alafu akamwambia kwa sauti ya chini kuwa kifaa hicho hufanya kazi ndani ya mita kadhaa karibu na mlengwa wao, hivyo muda wote kiwapo karibu kwaajili ya kuongeza ufanisi wake, baada ya maelezo hayo yeye pamoja na Jennifer wakaondoka zao wakimwacha Mitchelle akiwa chini hajiwezi, pamoja naye wapo wanaume lukuki walioshikilia bunduki nzito nzito, kidogo tu bwana yule mnene akabofya kifaa alichopewa na dokta, Mitchelle akatetemeka mpaka kupoteza fahamu zake!
Alipotelea kwenye kiza kinene kisicho na ukomo.
***
Taipei, Taiwan, majira ya saa nne asubuhi ...
Bwana mmoja aliingia ndani ya sebule nzuri, alikuwa amevalia suti nyeusi, nywele zake maridadi amezilazia nyuma, mwendo wake wa ukakamavu, akatazama na kumwona Dr. Lambert pamoja na Jennifer, watu hao walikuwa wamekaa kwa utulivu katika makochi makubwa malaini, mbele zao kuna vistuli vidogo vya kioo, vistuli hivyo vilikuwa vimebebelea glasi zenye vinywaji.
Bwana huyo aliyeingia akasema, "yupo tayari." Basi Dr. Lambert na Jennifer wakasimama na kuongozana na bwana huyo kidogo wakaingia ndani ya ofisi walimokutana na bwana mmoja aliyeketi akiwapa mgongo, pembezoni ya bwana huyo alikuwapo mwanaume yule mnene, mtu wa miraba, amesimama kama sanamu akitazama kwa macho yaliyofungwa na ndita kana kwamba ametoka kugombana na mtu.
Bwana yule alowaleta wakina Jennifer ofisini hapa akanena kwa lugha yake anayoijua kisha akaondoka zake kutoa faragha, bosi mkubwa alokuwa amekaa kitini akajigeuza na kukutana uso kwa uso na wageni wake, mara moja Dr. Lambert akatabasamu, sijui nini kilimfurahisha.
Bosi huyo alikuwa mwingi wa mashavu na uso mweupe pe usokuwa na tone hata moja la ndevu, kidevu chake kidogo kimechongoka, macho yake ni madogo, asili ya Ashia, lakini makali yakikutazama, alitabasamu kidogo alipowatazama wageni wake alafu akasema,
"Kazi yenu imekuwa njema sana!" Kisha akavuta droo ya meza yake, humo akatazama na kutoa macho yake upesi, mkono wake wa kushoto ukatoa bahasha ndogo ya kaki, bahasha hiyo ilikuwa imejaa almanusura kupasuka, akamkabidhi Dr. Lambert,
"Mimi ni mtu wa kupenda cash, samahani kama n'takuwa nimekukwaza," alisema akijiegemeza kwenye kiti chake, naye Dr. Lambert akatazama ndani ya bahasha hiyo, kulikuwa na fedha kedekede, akashindwa kujizuia kutabasamu, akamtazama Jennifer alafu akamtikisia kichwa.
"Huo ni mwanzo kama tulivyokubaliana," akasema bosi mkubwa, "lakini kadiri mtakavyokuwa na manufaa kwangu ndivyo n'takavyozidi kutoa, nadhani mnajua mimi na nyie biashara yetu haijakoma."
"Ndio," Dr. Lambert akaitikia kwa furaha na hawakukaa tena hapo kwa muda, bwana aliyewaleta akaja kuwachukua tayari kwaajili ya kuwapeleka hotelini kwa mapumziko. Bosi mkubwa aliwatazama wakiwa wanaenda zao, amesimama kando ya dirisha kubwa la kioo lililopo katika ofisi yake, mikono yake imo mifukoni, gari lilipopotea mbele ya macho yake akageuka kumtazama bwana yule wa miraba minne, akamwambia,
"Siku ya leo haitakuja kusahaulika milele katika ardhi ya Taiwan. Siku halisi ya ukombozi."
Bwana yule wa miraba hakusema jambo, alikuwa anatazama tu akisimama pasipo kupepesuka, ni kana kwamba alikuwa amesimikwa hapo na programu maalumu, bosi akaendelea kusema,
"Kaka yangu huko alipo atakuwa na furaha isiyokuwa na kifani, hatimaye haki yake imefuata mkondo na hakika atafurahi zaidi haja yetu itakapokamilika!"
Akasimama akiutazama ukuta kana kwamba kuna kitu anakiona, kitu kinachomfurahisha, akatikisa kichwa chake kisha akaketi kwa kujibwaga kwenye kiti.
"Na vipi kuhusu wale mabwana?" Kwa mara ya kwanza bwana yule wa miraba minne akazungumza, bado alikuwa amesimama akitazama mbele huku akiwa ametulia tuli, bosi mkubwa akafyonza meno yake chonge akiwa anatazama kwa uyakinifu, alikuwa anapanga jambo kichwani mwake, baada ya sekunde chache akasema,
"Nina mpango nao. Ngoja tuone mambo yatakavyowiwa."
"Mpango huo ni pamoja na kuwamaliza?" Bwana wa miraba minne akawahi kuuliza, alikuwa anafurahia sana hilo jambo, pengine alikuwa anapenda kuua watu kuliko hata kula, bosi mkubwa akamtazama pasipo kumjibu, naye akakaa kimya kana kwamba hakuna kilichotokea.
***
Taiwan, majira ya saa sita usiku...
"Bado hataki kula," bwana alisema akisimama, mbele yake alikuwapo mwenzake aliyeketi kwenye kiti kisichokuwa na meza, wote wamevalia kombati jeusi 'plain'.
"Kile chakula cha asubuhi kipo mpaka saa hii, hajagusa kabisa."
Bwana aliyeketi akatikisa kichwa chake akisonya, akasema,
"Jana hajala pia, sijui anataka kufa?"
Alisimama akanyoosha mgongo wake, mgongo ukalia kah-kah, akalalama kwa uchovu, kidogo akapiga mhayo akijiendea.
"Ngoja nikamtazame, kama hataki kula basi mimi nile chakula chake, nishachoka kumbembeleza." Kidogo akasimama, akageuka na kumtazama mwenzake kwa sura ya kubung'aa, akasema,
"Hiviii!" Akamsogelea mwenzake karibu, "kweli mkuu amelenga kumuua huyu?"
"Kwanini unauliza?" Mwenzake akahamaki.
"Kama wamelenga kumuua kwanini wanahangaika kumhudumia kiasi hiki?"
Wakatazamana kama matapeli wanaopanga 'kumpiga' mtu kisha kidogo bwana huyo akaendelea akisema,
"Anapewa chakula kizuri kuliko sisi. Bado mkuu amesema kuna daktari atakuja kumtazama na kumfanyia vipimo. Wewe unaona kawaida? Au wewe unaonaje?"
"Sitaki matatizo," mwenzake akamkatiza, "niliyonayo yananitosha, bwana, we nenda kamtazame alafu urudishe viungo vyako vya siri hapa. Acha kiherehere."
Bwana akamsonya alafu akaenda zake kumtazama mlengwa, kiunoni amening'iniza kadi inayotumika kufungulia milango, akaambaambaa na korido na si muda akawa mbele ya mlango mzito wa chuma ambao ilikuwa na dirisha la kioo, kioo kigumu, hapo akachungulia kwa ndani, akamwona mwanamke amesimama akiwa amempatia mgongo, anatazama ukutani, kutazama pembeni akaona sahani ya chakula na chakula chake kikamilifu, hakikuguswa hata tone, akaita,
"Wewe! Weweee!"
Mwanamke yule hakugeuka, akamuuliza,
"Kwanini hauli?"
Hakujibu wala hakumtazama, akasema,
"Wewe usile, unataka kufa kama yule mama enh?"
Mwanamke yule kusikia hivyo akageuka, alikuwa ni Mitchelle, nywele zake zilikuwa hovyo na sura yake imefura, akatazama mlangoni na kuuliza, "mwanamke gani?"
Yule bwana akatabasamu, hatimaye alipata 'attention' ya mtu wake, akajivuna kwa raha kabla hajajibu, "si yule Jennifer!"
"Jennifer?" Mitchelle akauliza akisogelea mlango.
"Ndio, kwani hawajakupa taarifa amefariki jana usiku?" Bwana akahamaki.
"Nini kimemuua?" Mitchelle akauliza.
"Sijui. Ninachofahamu ni kuwa amekufa. Hayo mengine sijui ... haya utakula ama utanipa hiko chakula?"
***