Tukibaki Hai, Tutasimulia

Tukibaki Hai, Tutasimulia

TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 11


Na Steve B.S.M



Mpelelezi bado hakuwa ameamka. Ni saa tatu na nusu ya asubuhi hivi sasa. Alikuwa anaugeuza mwili wake mzito huku na kule. Anagugumia na kukoromea usingizini.

Dirisha lake lililokuwa ubavuni mwa kitanda ndilo lilipitisha mwanga wa jua la asubuhi ukamchapa usoni. Aliuvumilia mwanga huo kwa muda kidogo akiukunja uso wake.

Akageukia upande wa pili.

Alijaribu kulala lakini mwili uligoma. Alifunga macho pakavu sasa. Akili yake ilimkumbusha majukumu yake, fahamu zake zikamuitikia. Upesi akaamka.

Aliketi kitako akijaribu kuwaza mambo. Uso wake ulikuwa umejawa na 'maramani' ya shuka. Kifua chake kilichokuwa wazi kilikuwa na chuchu nene na nywele kwa mbali.

Tumbo lake nene kiasi lilikuwa limeipokea bukta yake nyepesi ya kulalia kiunoni. Mikono yake minene ya wastani ilikuwa imezama ndani ya godoro kumpatia 'balansi' ya mwili akiwa ameketi.

Macho yake mekundu yalionyesha amezama ndani ya fikra. Kuna jambo alikuwa analiwaza. Sijui nini kilimkurupua, upesi akaitafuta simu yake kitandani.

Hakuiona.

Alitazama chini akaiona ikiwa hapo, uso wake unatazama chini. Upesi akainyanyua na kuitazama. Haikuvunjika kioo bali zilikuwa zimejaa 'notifications' lukuki kiasi cha kujaza kioo kizima.

Alikuwa amepigiwa si chini ya mara ishirini. Meseji nazo kedekede!

Alitoa 'lock' akapekua upesi, humo akakutana na 'missed calls' kama hamsini za mkuu wake wa kazi. Kama haitoshi 'messages' zake lukuki akimuuliza na kumuuliza, yuko wapi na yuko wapi?

Mbali na hizo, alikuwa amepokea 'notifications' tatu za vyombo viwili vya habari kuhusu jiji la New York. Alikuwa ame - 'subscribe' Chaneli hizo za habari anazoziamini.

Alizitupia macho kwa haraka akaona habari ziliomshtua. Habari za mlipuko na mauaji! Kutazama habari hizo zilirushwa saa ngapi, ni asubuhi ya mapema. Yalishapita masaa mpaka sasa.

Aisee!

Sasa alijua kwanini alitafutwa kiasi kile. Upesi alikimbilia bafuni, akaoga na kujiveka nguo, ilikuwa ni shati jeusi na suruali ya kaki. Hakuwa na muda wa kubrashi viatu, akavaa raba zake nyeupe na kulifuata gari.

Alipowasha na kushika njia ya kwenda ofisini, alipiga simu aliyoweka 'loudspeaker' na kuiweka kwenye kifaa maalumu pembeni kidogo ya usukani.

Simu iliita kwa muda mchache, ikapokelewa. Alikuwa ni mkuu wake wa kazi. Maramoja bwana huyo alipopokea, alimuwakia Mpelelezi kwa kupuuzia simu na 'messages' zake.

Mpelelezi hakupata hata wasaa wa kujitetea. Mkuu huyo wa kazi aliongea pasipo kumpa nafasi ya kuhema. Alipomaliza, alimsihi Mpelelezi amtafute bwana yule wa Usalama mara moja kisha akakata simu.

Hakuelewa. Si kwasababu hakupewa nafasi ya kuongea, bali kitendo cha mkubwa wake kumwelekezea kwa mtu mwingine juu jambo ambalo alitaraji watalizungumza.

Alijaribu kuwaza. Ni nini kimetokea. Bwana huyo wa usalama ni na -- ah-ah! Kidogo akakumbuka. Bwana huyu wa usalama alikuwa ni yule mwanaume aliyekutana naye kwenye uwanja wa kamari!

Alikumbuka sura yake, babyface, na namna alivyomjia kama mkombozi siku ile ya uvamizi.

Akakumbuka zaidi kuwa alimwona bwana huyo ofisini kwao akiwa ameambatana na mwenzie asiyemkumbuka kabisa. Ndio. Aliwakuta katika ofisi ya mkuu wake wa kazi.

Lakini baada ya hapo hakuwa anakumbuka kitu. Zaidi ya maumivu ya kichwa na hisia za uzito mwilini, kumbukumbu yake ilikuwa tupu kabisa!

Alijilazimisha kukumbuka namna alivyorudi nyumbani. Hakukumbuka kitu. Alijaribu kuukumbuka usiku wa kuamkia siku hiyo, hapo ndo' hakukumbuka chochote kabisa.

Alistaajabu ni nini kilichomkumba.

Akiwa katika zoezi hilo la kuwaza na kuwazua, akitafakari hapa na pale, ndipo alipobaini baadhi ya mambo ambayo sasa yalikuwa yanaleta maana fulani.

Alikumbuka kuhusu milango ya nyumbani kwake. Milango yote aliyopita ilikuwa wazi. Hivi ilikuaje? ... desturi yake ni kuifunga milango yote punde anapoingia ndani kujipumzisha. Ina maana aliisahau?

Lakini pia kama haitoshi, hata 'parking' ya gari yake haikuwa sawa. Si vile anavyoegesha gari hilo kila siku. Leo alilikuta likiwa kando kidofo na pale awekapo mara kwa mara. Huwa hata akilewa vipi, hajawahi kukosea zoezi hilo. Jana ilikuaje?

Alikuja kubaini, baada ya yote hayo, kwamba jana alirejea na mtu nyumbani. Mtu huyo ndo' aliyeendesha gari na kumuingiza ndani. Lakini mtu huyo ni nani? Na kwanini alimleta?

Hakuwa na majibu.

Alimpigia simu bwana yule wa usalama, wakaongea machache wakipanga pa kuonana hivyo baada ya dakika kadhaa wakawa wapo pamoja, ndani ya gari la Mpelelezi.

Kitu cha kwanza alichouliza bwana wa usalama kilikuwa ni;

"Unaendeleaje na hali yako hivi sasa?"

Swali hilo likampeleka mbali Mpelelezi. Upesi akili yake ikabaini kuwa bwana huyu ndiye aliyekuja naye nyumbani jana yake.

Sasa akatamani kujua ni nini kilitokea. Akamuuliza bwana huyo naye akamweleza yote, namna gani walivyokutana na kuadhimia kufanya kazi kwa pamoja.

Swala hilo likamstaajabisha kidogo Mpelelezi. Ilikuwa inawezekanaje? Alimuuliza 'babyface' kuhusu hilo swala, akamjibu kwamba waliridhiana na makubaliano yaliwekwa na sahihi zao wote. Akazidi kushangaa.

"Sahihi yangu?" Aliuliza. Babyface akamtolea nyaraka ile na kumwonyesha. Aliisoma asiamini anachokiona.

"Pengine maumivu ya kichwa yamekusahaulisha," alisema Babyface akimtazama Mpelelezi kwa tabasamu la mbali. Kidogo simu yake iliita, jina BIG, akaikata sauti na kuendelea na mambo yake.

Alirejesha nyaraka yake kwenye kabrasha lake dogo alafu akamweleza Mpelelezi juu ya kesi ya Ferdinand na yale yote yaliyotokea.

"Tukishindwa kuthibitisha kama Ferdinand yu hai basi huenda kesi hii ikafutwa," Babyface alimalizia kwa kusema hayo kisha akamwomba Mpelelezi ushauri na mawazo juu ya wapi wanapaswa kuanzia.

Lakini Mpelelezi hakuwa hapo. Yote aliyokuwa anaambiwa aliyasikia lakini kichwani akiendelea kutafakari kivyake. Akipanga na kupangua.

Alipoona amepata vya kutosha, hamna cha ziada, alimuaga Babyface akaenda zake. Hata mgeni wake alimpomsihi wazungumze zaidi, hakujibu. Hakuwa tayari.

Alielekea ofisini kwake moja kwa moja kuonana na mkuu wake wa kazi. Mwendo uliomchukua dakika arobaini na tano.

Alimkuta mzee huyo akiwa anakunywa kahawa yake nzito, mezani anapekua baadhi ya mafaili kandokando ya tarakilishi yake ya mezani.

"Umeshaonana na mwenzako?" Lilikuwa ni swali la kwanza. Alimuuliza Mpelelezi bila hata kumtazama. Macho yake yalikuwa 'busy' na kazi yake.

Mpelelezi alisonga akaketi kitako baada ya kusalimu salamu ambayo hakuitikiwa.

Akamtazama mkuu wake na kumuuliza kuhusu bwana yule wa Usalama. Alimuuliza ni kivipi wanafanya naye kazi na ni kwasababu gani kwani alikuwa anajiamini. Ni nini kilipwaya kiasi cha kupewa mwenza toka kitengo kingine cha usalama katika kazi ambayo ipo ndani ya uwezo wake?

Mkuu wake wa kazi aliendelea na alichokuwa anakifanya kana kwamba hajamsikia. Aliona ni upuuzi tu. Alimuuliza Mpelelezi kama amemaliza shida yake kwani ametingwa na kazi nyingi za kufanya.

Kisha akamwambia,

"Afisa, nadhani umetoka chuo muda mwingi sana kiasi cha kusahau amri ni nini katika jeshi, sivyo?"

Lilikuwa ni swali la kejeli lisilohitaji majibu, na huo ndo' ukawa mwanzo wa maongezi mafupi ya Mkuu wa kazi.

Akiwa bado anatazama kazi zake na kuzishughulikia, akamwambia Mpelelezi kuwa agizo hilo ni amri achilia mbali makubaliano rasmi yalishawekwa, hivyo badala ya kutangatanga kupoteza muda, ni vema akaanza kazi maramoja.

Mpelelezi akatupa swali lake la mwisho kabla hajaondoka.

Aliuliza,

"Ni kwanini kesi hii? ... Kuna ajenda gani ambayo nastahili kujua?"

Mkuu wake akamjibu hamna ajenda yoyote anayostahili kujua na ndo' maana hajajuzwa. Hapa Mpelelezi akawa hana tena cha kungoja. Hamna tena cha ziada.

Akajirudisha kwenye gari lake, humo alimokaa akitafakari mambo haya.

Kidogo akakata shauri.

Kwanza, alipita kwenye lile eneo ambalo Ferdinand alifia. Hapo akachukua wasaa wake kutazama na kukagua asipate kitu kikubwa cha maana. Vielelezo vyote vilishabebwa.

Hata na hivyo hakutarajia kupata kitu hapo. Alifika tu kwa lengo la kupata picha kamili ya tukio hilo alilolisikia kwenye vinywa vya wengine.

Akajiweka kwenye gari lake na kuanza safari aliyoamini huenda ikamfungulia milango ya kuanzia kwenye kesi hii.

Akiwa katika moja ya foleni, aliwasha redio yake, sauti ikiwa kwa mbali, akawa anasikiliza wimbo laini wa The Commodores, ngoma matata iliyowahi kutikisa dunia kipindi hicho kwa jina la 'Nightshift'. Wimbo huo ukawa unamliwaza akiwa anatafakari zake.

Taratibu sauti nyororo zikaukanda ubongo wake. Akahisi ahueni moja kubwa alipozama ndani ya melodi hizo tamu zisizokuwa na kinai.

Safari yhii ilikuwa ni ya kuelekea The Halletts Point. Huko aliamini atapata mawili matatu kuhusu Ferdinand na yule mwanamke mtuhumiwa wa mauaji. Kama upepelezi wake ule ulikuwa sawa, basi huko atapata vya maana.

Alifika mbele ya jengo hilo, akalitazama kwa urefu wake. Lilikuwa maridadi haswa. Linavutia kwa mwonekano na mpangilio wake. Kwa wazungu wangesema ni 'breath-taking building'.

Aliingia humo akaenda mara moja kwenye chumba cha ulinzi, chumba ambacho kilikuwa kinaongoza kamera zote, zaidi ya miamoja, zinazopatikana katika jengo hili maridhawa.

Huko alikutana na bwana mfupi aliyevalia shati jeupe na tai nyeusi. Nywele zake ameweka rangi ya 'pink', amevalia miwani ndogo ya jua.

Bwana huyo alikurupuka alipomwona Mpelelezi. Upesi akasimama toka kwenye kiti chake akamjia na kumuuliza ni namna gani anaweza kumsaidia.

Mpelelezi alitazama mazingira ya hapa. Kulijawa na video nyingi zilizokuwa zinapokea taarifa toka kwenye kamera zilizopo kila kona ya jengo hilo. Na kwa kupitia video hizo, aliona watu mamia, wakikatiza huku na kule.

Akajitambulisha kwa bwana huyu, yeye ni mpelelezi toka polisi na alikuwa hapo akihitaji msaada wa video fulani muhimu kwa ajili ya upelelezi.

Bwana huyo akatahamaki.

"Ala! Mara nyingine tena?"

Mpelelezi akamuuliza,

"Mara nyingine?"

Hapa ndo' bwana huyo akamweleza kwamba alishakuja mtu mwingine hapo akidai kitu hikohiko anachokidai yeye hivi sasa na alishampatia hivyo hana rekodi yoyote iliyobakia.

Swala hilo likamchanganya kweli Mpelelezi. Ni nani aliyepata wazo la kuja hapa kabla yake? Kwa maelezo ya bwana yule, aliyekuja hapa alikuwa ni bwana mtanashati mwenye mvuto wa sura. Naye alijitambulisha kama mwanausalama akiwa na kitambulisho chake.

Hapa Mpelelezi akaishiwa nguvu. Tayari kichwani kwake ilishakuja picha ya Babyface.

"Oh my! ... Oh my!"

Mara moja akataka kunana na mkurugenzi wa jengo hilo. Hapo akakutana na mwanaume mzee, nywele nyeupe na kitambi kidogo. Bwana huyo alikuwa mwakilishi wa mmiliki wa jengo hili.

Alimkaribisha vema Mpelelezi katika ofisi yake, akamuahidi kumpatia ushirikiano anaoutaka.

Mpelelezi, pasipo kupoteza muda, akaeleza shida yake ya kupata taarifa zote za wakazi wa eneo hilo, haswa za walengwa wake ambao ubaya hakuwa na picha yoyote aliyoongozana nayo kwani alitaraji kuzikutia hapa.

Kwasababu hiyo basi, alitaka kupitia taarifa zote za waliopanga hapa, mmoja baada ya mwingine.

Bila hiyana Mkurugenzi akampa fursa hiyo.

Aliketi kwenye tarakilishi ya mkurugenzi akatumia lisaa lizima hapo. Alipekua mtu baada ya mtu. Picha baada ya picha. Hakupata kitu. Hakuona chochote kile katika vile anavyovitafuta.

Akashusha pumzi ndefu akijiuliza ni wapi amekosea. Alipowaza kidogo ndo' akapata pia na wazo la kupitia wapangaji waliomaliza muda wao au kuutamatisha mkataba.

Huko alitazama kwa nusu saa, akaona kitu kilichokamata mazingatio yake. Ilikuwa ni picha ya mwanamke ambaye hii ni mara yake ya pili kumwona.

Mwanamke yule aliyeambiwa kuwa amefariki kwa kujinyonga kule chuoni.

Alikuwa ni mwanamke yuleyule ambaye alionekana kwenye usajili wa 'uber' wa mwanamke wanayemtafuta kwa mauaji ya The DL.

Sawa.

Ina maana mwanamke huyo ameshatimka?

Alitazama taarifa akaona mwanamke huyo aliondoka kwenye makazi hayo majuzi tu. Siku mbili toka sasa. Siku mbili nyuma ya tukio la mlipuko wa Ferdinand.

Mpelelezi akarudi kwenye gari lake na kutulia humo kwa kama nusu saa hivi.

Alitafakari ni namba gani Babyface alifahamu kuhusu eneo lile na hiyo misheni yake. Alijiuliza ni mangapi bwana huyo atakuwa anayafahamu nyuma yake?

Hakuwahi kutoa taarifa hizi hata kwa mkuu wake. Imekuaje akazipata? Au walifanya upelelezi wao binafsi? Kama ndio, mbona hakumshirikisha?

Alipotafakari hapo baada ya muda, akaona ni vema tu afunge safari kwenda kutafuta habari kuhusu mwanamke yule kwenye picha.

Ajue kweli yake.

Aokoteze chochote kile kinachomhusu mwanamke huyo kwani huenda kikampatia njia ya kwenda.

Alitekenya funguo ya gari, akaondoka.

Lakini, kwa mbali, kuna mtu alikuwa anamtazama.

***
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 12


Na Steve B.S.M




Queens, New York. Olympus Printing Press.

Richie alimtazama Hilda kwa muda kidogo kisha akanyanyuka kumfuata mwanamke huyo alipo.

Kwa macho yake ya nyama, Hilda hakuwa sawa na aliona kuna haja ya kumjulia hali yake kwa ukaribu.

Alimuuliza,

"Kuna tatizo?"

Hilda akatikisa kichwa kukataa, lakini sura yake ilimsaliti.

Richie akavuta kiti kilichokuwepo pembeni, akaketi karibu naye.

"Nini kinakusumbua, Hilda?"

"Nadhani ni njaa."

Hilda alisema akitabasamu. Alimtazama Richie machoni kwa kumkodolea.

"Usijali, hata hivyo nilikuwa nimepanga kukutoa lunch leo hii, lakini niko serious, Hilda. Nimekuona muda tu ukiwa umepoa sana."

Hilda akatikisa kichwa chake kwa mbali. Hakutaka kukiri hilo. Alinyanyuka akaendea mlango, akatazama nje na kurejea ndani.

Alimuuliza Richie aliyekuwa anamtazama,

"Vipi, boss aliongea na wewe?"

Richie akatikisa kichwa. Akasema hakujua bwana huyo alikuwa wapi kiasi kwamba hakufika kazini mpaka muda huo, kisha hapo ndo' akamuuliza Hilda kama ujio wa bwana huyo ndo' chanzo cha mawazo yake.

Hilda akajibu,

"Hapana."

Ila akaongezea swali, "vipi kama amekumbwa na tatizo?"

Kabla Richie hajajibu, mlango wa ofisi ukafunguliwa. Alikuwa ni Mr. Bryson.

Aliingia akiwa ameshikilia koti lake mkononi. Alikatiza kana kwamba hamna mtu hapa ndani lakini alipofika katika mlango wa kuingia ofisini mwake, akamwita Hilda.

Akamsihi aje ofisini kwake haraka.
Kidogo Hilda akawa ameungana naye, akiwa ametulia katika kiti cha mgeni.

Hapo ndo' Bryson akavuta kwanza pumzi kisha akamwambia Hilda kuhusu kazi yao ya siri.

Alisema,

"Kama nilivyokuwa nimekuambia, yule bwana aliyekuwa anatuletea kazi na pesa, amefariki katika ule mlipuko maarufu New York."

Akaongezea,

"Na kwa taarifa zilizosambaa bwana huyo alikuwa anahusika na shughuli za madawa ya kulevya, kwahiyo nadhani ushapata picha kamili."

Hapa Hilda alikuwa ametulia tuli kama maji ya mtungi lakini ndani yake alikuwa na hofu kubwa.

Alitaka kuongea lakini Bryson akamkatisha.

Alimuuliza,,

"Unakumbuka maagano yetu, Hilda?"

Hilda hakujibu kitu. Alinyamaza kimya kana kwamba hakusikia alichoulizwa.

Bryson akarudia kuuliza,

"Hilda, unakumbuka maagano yetu?"

Muda huu sauti yake ilikuwa kali na yenye uzito. Uso wake ulimaanisha kile alichokuwa anaongea.

Hilda akapapatuka.

Uso wake ukiwa umejawa uoga, akajibu,

"Ndio. Nayakumbuka."

Bryson akasema,

"Vema. Sasa ndo' muda wa kuyafanyia kazi."

Akamweleza mwanamke huyo kwamba wataendelea na kazi hiyo waliyopewa mpaka pale itakapokoma. Haitajalisha ni kitu gani kitakachotokea katikati.

Lakini katika hayo, Hilda akauliza,

"Sasa ni nani atakayekuwa anatuletea kazi kama bwana huyu amekufa?"

Bwana Bryson akamweleza kuwa alishaongea na mhusika mkuu. Kazi itaendelea kuja kama kawaida lakini hivi sasa wakitumia njia ya posta kwaajili ya usalama zaidi.

Baada ya hapo, bwana Bryson akamtaka Hilda akaendelee na kazi yake kwani ana shughuli kadhaa za kufanya.

Hilda akaamka. Kabla hajaanza hatua, mlango ukafunguliwa. Kutazama alimwona mwanamke mwenye sura nyekundu akiwa amesimama mlangoni.

Mwanamke huyo alikuwa amevalia gauni refu la kijani, mikono ya nyavunyavu. Kichwani mwake amebana nywele na kibanio cheusi kilichozunguka kichwa.

Alikuwa ni mke wa Bryson.

Aliuliza akimnyooshea kidole Hilda,

"Wewe ndiye Hilda, sio?"

Hilda asijibu akamtazama Bryson. Naye Bryson akamtazama mwanamke huyo kabla hajahamisha macho yake upesi kwa mkewe.

Hakuamini alichokuwa anakiona.

Alisimama upesi akamuuliza mkewe,

"Ina maana hukutosheka na ugomvi wa asubuhi?"

Hapa ndo' Hilda na Richie aliyekuwa mlangoni wakapata kufahamu kuwa Boss wao alikawizwa na ugomvi wa nyumbani.

Hilda akataka kutoka awapishe lakini mke wa boss akamzuia.

Alimtaka abaki hapo kwani kinachoendelea kinamhusu.

Bryson, kwa kutumia hekima, alimsihi Hilda atoke ofisini mwake lakini jambo hilo likakumbana na upinzani mkubwa toka kwa mkewe aliyekuwa anamshutumu Hilda kumwaribia mahusiano yake.

Mwanamke huyo alisema,

"Ni nini unaongea na mume wangu mara kwa mara? Ni nini unataka?"

Wakati anasema hayo, alikuwa ametoa macho yake kwa kadiri awezavyo.

Hilda akakosa cha kuongea.

Alihisi ulimi wake umekuwa mzito tani kadhaa. Alitetemeka asielewe kipi cha kufanya.

Baada ya nusu saa alikuwa ameketi kwenye kiti chake, ameshika kichwa chake anawaza. Muda mwingine alikuwa anashituka akisikia sauti kali toka ofisini kwa boss wake.

Alikuja kupata ahueni baadae, mwanamama huyo alipojiondokea.

Bryson akamfuata na kumwomba radhi. Alimwambia mkewe ni mtu wa wivu sana na yeye amekwishamzoea tabu zake.

Lakini akampatia ofa kwa kumwambia,

"Nitakutoa lunch kama tafadhali yangu. Sema unataka kula nini leo hii?"

Kauli hiyo ikachipua tabasamu kubwa kwenye uso mnene wa Hilda. Tumbo lake likanguruma kushangilia. Mate yakamjaa mdomoni ghafla alipowaza chakula kile akipendacho.

Alisikia harufu ya chakula hicho puani mwake.

Mwili ukamsisimka.

Jambo hilo lilikuwa bora zaidi kwa siku yake ya leo ambayo ilikuwa tenge. Japo alishapewa ofa na Richie lakini haikuwa ya uhuru wa kiasi hiki cha kuchagua akipendacho.

Akafanya kazi upesi.

Muda ulipofika, Richie akamfuata akimtaka waende kula naye chakula cha mchana. Bwana huyo, asijue kinachoendelea, alidhani bado ofa yake ipo mezani.

Hilda akamtazama kwa huzuni ya kuigiza.

Alimwambia boss amempatia ofa kubwa ambayo hawezi kuikataa.

Alisema,

"Imagine ameniambia nichague chakula chochote ninachokitaka. Chochote kile!"

Jambo hilo likamnyong'onyesha sana Richie.

Ni muda mchache nyuma alidhania angefaidika na sokomoko lililoibuka kati ya Bryson na mkewe kuhusu Hilda lakini imekuwa tofauti.

Akiwa anawaza kuongozana na mwanamke huyo kwenda mgahawani, pasipo kujali kuhusu ofa yake aliyotoa, mara Bryson akaingia akitokea ofisini mwake.

Akamwambia Hilda waongozane.

Walienda pamoja wakimwacha Richie nyuma amesimama anawatazama.

Hamu ya kula ya mwanaume huyo ikaisha 'hafla. Akaketi kitini kwake akiwaza namna gani tonge lilivyomponyoka karibia na mdomo.

Akafikiria sana.

Baada ya kitambo kidogo, kuna jambo akakubaliana na nafsi yake kulifanya.

Ulikuwa ni muda wa yeye kucheza karata yake bora.

***
Saa Moja Usiku.

Richie alisimama nje ya ofisi ya The Olympus akiwa ameegemea ukuta. Mikono yake miwili ilikuwamo mfukoni mwa suruali, macho yake yakiwa barabarani kutazamatazama.

Kidogo, Hilda akatoka ofisini akamwona bwana huyu.

Alimwambia,

"Nilidhani ushaondoka kitambo!"

Richie akatabasamu asiseme jambo. Wakaongozana wakielekea kusini mwa ofisi yao.

Ulikuwa ni mwendo wa dakika kadhaa kabla hawajaachana kila mtu kushika njia yake.

Richie alimtazama Hilda, akamuuliza,

"Hilda, kuna jambo gani linaloendelea baina yako na Boss?"

Hilda alishtuka. Ni kana kwamba jambo hilo lilikuwa geni kabisa masikioni mwake, ndo amepata kulisikia kwa mara ya kwanza.

"Mimi? Usiniambie na wewe unawaza kama yule mwanamke mwehu?"

"Hapana," Richie akamjibu. "Lakini naamini kuna kitu ambacho mnanificha. Kuna jambo linaendelea nyuma ya mgongo wangu. Sidhani kama ni sahihi ninyi kunifanyia hivyo."

"Hayo ni mawazo yako, Richie," Hilda akajipambanua. "Sijui kwanini unapenda kujipa mashaka kiasi hiko. Nakwambia hiki kitu sio mara ya kwanza na ninahisi inaweza ikawa si mara ya mwisho. Hamna chochote kile."

Richie hakukata tamaa. Akarusha tena ndoano yake,

"Huu ni mwaka wa pili tukiwa pamoja kazini. Kwa miaka yote hiyo sijawahi kuona ukibadilika kiasi hiki, kuwa na ukaribu kiasi hiko na boss. Achilia mbali ratiba tofauti na ilivyokawaida. Unataka kuniambia hayo yote ni kawaida tu?"

Hilda akatikisa kichwa kuridhia.

Alisema,

"Ndio. Kwangu sijaona cha ajabu. Labda ni wewe ndo' umebadilika. Hujawaza hilo?"

Wakaongea maongezi hayo yasiyokuwa na matunda mpaka pale walipofikia mahali pa kuachana kila mtu kushika njia yake.

Hapo ndo' Richie akatupa karata yake dume.

Alisema,

"Najua kila kitu, Hilda. Kila mara nakupa nafasi ya kukiri hilo lakini huioni. Pesa zimekufumba macho kiasi kwamba hujali hata uhai wako."

Aliposema hayo, akajiendea zake na njia tofauti. Hilda akamtazama kwa kitambo kidogo alafu naye akaondoka zake kufuata ya kwake.

Alitembea akiwaza kile alichokiskia toka kwa Richie.

Sauti moja ndani ya nafsi yake ikamwambia amrudie bwana huyo kumuuliza ni nini anafahamu lakini ya pili ikamkataza katukatu. Ilimwambia huenda hiyo ni janja tu ya Richie kumpekenyua.

Kadiri alivyokuwa anatembea ndivyo alizidi kusikia sauti hizo zikigombana ndani yake na hii inayomwonya ikizidi kupata nguvu zaidi.

Lakini atakuwa amejuaje? Hapana, hafahamu. Hapana, hafahamu kitu. Hapa-- akasita.

Alisimama akitoa macho yake. Ni kana kwamba alijiwa na akili timamu hivi sasa. Vipi kama kweli anajua?

Aliwaza mara ngapi bwana huyo alimuuliza kuhusu yeye na boss Bryson. Akakumbuka pia namna gani bwana huyo alivyokuwa anamtazama wakati anamuambia kwamba anajua kila kitu.

Akatia shaka.

Aligeuka upesi akakimbia kurudi nyuma alipotokea.

Kwasababu ya mwili wake mzito hakuweza kukimbia kwa upesi lakini alipambana vivyohivyo.

Alikimbia akisimama na kuhema. Alikimbia tena akasimama na kuhema. Pumzi ilimkata kabisa kifuani. Alihema kana kwamba hatohema tena kesho.

Miguu ilimuuma, kifua nacho kilimbana.

Akatoa simu yake mfukoni. Upesi akatafuta namba ya Richie na kuipiga.

Simu iliita bila kupokelewa. Ikakata.

Akarudia tena.

"Pokea, Rich. Pokea!"

Simu haikupokelewa.

Akapiga kelele.l za hasira.

***

Bronx, New York.

Saa nne ya usiku.


Babyface alivuta mkupuo wake wa mwisho wa sigara kisha akaitupa chini na kuisigina kuizima.

Akatema moshi kwa madaha. Moshi ukafunika uso wake na kupotelea mbali.

Bwana huyu alikuwa ameegemea gari, mkono wake mmoja upo mfukoni. Kama ilivyo mara nyingi, alikuwa amevalia suti na tai nyeusi. Nywele zake zimetengenezwa vema zikihakisi mwanga mkali wa mataa ya majengo marefu yaliyopo hapa.

Alitazama saa yake, akatoa simu yake mfukoni na kupiga namba ile aliyoitunza kwa jina 'BIG'. Kidogo tu simu ikapokelewa, Babyface akasema,,

"Unanichelewesha."

Akajibiwa na sauti tokea upande wa pili wa simu,

"Tazama kushoto kwako."

Akatazama na kumwona mwanaume mmoja akiwa anamjia. Akarejesha simu yake mfukoni na kungoja.

Kidogo mbele yake akawa amesimama bwana mmoja mnene. Nywele zake fupi, macho madogo. Shingoni amejaza mikufu na mkononi ana pete na bangili za dhahabu.

Bwana huyo alikuwa amevalia suti kachumbari iliyomkaa vema na mwili wake kama kisiki cha mbuyu.

Ukimtaza vema, utamkumbuka.

Alikuwa ni bwana yule aliyecheza kamari na Mpelelezi siku ile katika ukumbi wa Resorts World Casino. Mchezo ambao ulipelekea ugomvi na majanga.

Bwana huyo akamsalimu Babyface kwa kupeana mikono kisha wakafungua maongezi yao mafupi.

Katika maongezi hayo, BIG akamlaumu Babyface kwa yale yaliyotokea siku ile.

Alisema,

"Haikuwa na haja ya kutuponda kiasi kile, kaka. Mwili wangu mpaka sasa una maumivu na mmoja wetu bado yuko hospitali hapa tunapoongea. Amelazwa hoi."

Babyface akaomba samaha nyepesi kisha akazama mfuko wake wa nyuma akatoa pochi nene nyeusi.

Aliifungua pochi hiyo akatoa dola kadha wa kadha akamkabidhi BIG.

BIG akahesabu pesa hizo.

"Najua tulikubaliana kiasi hiki cha pesa lakini hasara kwetu ni kubwa sana, mkuu. Tafadhali lizingatie hilo."

Babyface akaongeza pesa maradufu kisha akasema,

"Nadhani inatosha, sio?"

BIG akatikisa kichwa kuridhia. Aliziweka pesa hizo mfukoni mwake akaaga akiwa amekubaliana na bwana huyo miadi mingine ya unywaji.

Babyface akaingia ndani ya gari lake. Kabla hajaondoka, simu ikaita. Akafura. Alidhani ni BIG aliyetoka kuteta naye.

Alipotazama akaona ni mwingine. Upesi akapokea akisema, "nipe ripoti."

Bwana wa upande wa pili akamweleza akisema,

"Mpelelezi ametua ndani ya jiji la San Fransisco,California."

Babyface akahamaki.

"Are you serious?"

Aliyatoa macho yake bora ya mshangao.

Alikata simu upesi, akawasha gari akiondoka haraka kama mwendawazimu.


**
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 13


Na Steve B.S.M



San Fransisco, California.

Saa tano usiku.

Mpelelezi alitazama saa yake ya mkononi kisha akatengenezea nywele zake kwa kiganja cha mkono wa kushoto. Nywele zilikuwa zimekaa vema.

Alikuwa amevalia suruali nyembamba nyeusi na viatu vyenye sori kubwa ngumu. Juu alivalia shati rangi ya machungwa na koti jeusi.

Ulikuwa ni wasaa wake murua huu. Wasaa wa kutumia pesa. Alikuwa amesimama karibia na sehemu ya kuegeshea magari, mkabala na jengo kubwa lenye maandishi makubwa meupe yaliyosomeka: San Pablo Lytton Casino.

Jengo hilo lilikuwa mahususi kwa michezo ya kamari. Humo ndani kulikuwa na mashine lukuki za michezo ya kubahatisha pamoja pia na watu wengi wakitumia fedha zao kwenye starehe.

Mpelelezi aliingia humo akatafuta sehemu ya kuketi, mbele ya mashine, kisha akaanza kucheza hapo akiwa anakunywa kahawa tamu na ya moto aliyoambatanishiwa na tiketi yake.

Alicheza na kunywa kidogo, akahisi simu yake inaita mfukoni. Akaipuuzia.

Aliendelea kucheza akiweka pesa kama mara tatu hivi, dude likizunguka na kuambulia patupu. Kabla hajaenda mzunguko wa mara ya nne, akachomoa simu na kutazama ni nani aliyekuwa anampigia.

Akakuta ni mkuu wake wa kazi. Tayari alishampigia mara mbili sasa.

Akawaza kidogo.

Akaendelea na mchezo wake akiipuuzia simu hiyo.

Alicheza kama michezo mitatu ya ziada, yote hakuambua kitu. Kila mashine ilipozunguka, ilikuwa ni patupu ikisimama.

Akashusha pumzi fupi. Hakuwa na mchezo mzuri hapa. Aliwaza huenda leo haikuwa siku yake ya bahati.

Basi akatoka hapo akielekea mahali kwanza apate kunywa kuweka kichwa chake sawa. Kiasi alichopoteza katika mashine hii kilikuwa kinatosha.

Alipanga akitulia kidogo, atarejea tena mchezoni japo kwa upande mwingine mbali na huu alotoka kuucheza sasa.

Aliagiza mvinyo akiwa amekaa mahali maalum ndani ya kumbi hii ya wastani, akawa anakunywa taratibu.

Taratibu huku akiipanga siku yake ya kesho pale patakapokucha.

Ilifikia muda akaacha kuwazawaza mambo ya kazi, akaamua kujipumzisha kwa kuiingiza akili yake katika starehe.

Akiwa anamalizia kinywaji chake, alibahatika kukutana macho kwa macho na mwanamke mrembo aliyekuwa amekaa kwenye moja ya meza ya kamari.

Mwanamke huyo alikuwa amevalia gauni jekundu lina vidotidoti vingi mithili vya almasi inayometameta.

Gauni hilo lilikuwa limemkaa vema katika 'English figure' yake matata.

Nywele zake zilikuwa ndefu nyeusi, kaziachia zikienda mpaka karibia na kiuno chake.

Macho yake, makubwa na malegevu, yalichorwa vema na msanii wa 'makeup'. Kope zake zilikolezwa rangi nyeusi na nyusi zake zilipunguzwa wingi zikitindwa kwa ustadi mkubwa.

lUso wake mwembamba ulipambwa na 'lips' zake zenye nyamanyama zilizometa kwa rangi ya 'pink'. Masikio yake yaliyochongoka yalitogwa na hereni murua yenye mikia mitatu iliyokuwa inaning'iniza vijitufe vidogo vyenye kumetameta.

Mwanamke huyo alikuwa amevalia viatu virefu vyeusi ambavyo havikuonekana mdomo wake kwani gauni lilikuwa refu.

Aliupandishia mguu mmoja juu ya mwingine alafu akapeleka uso wake pembeni, mbali na macho ya Mpelelezi.

Mpelelezi akamtazama mwanamke huyo kwa kitambo kidogo kisha naye akaendelea na yake. Akagiza kinywaji kilichofika si punde, akaendelea na ulabu wake wa wastani.

Muda kidogo, akayarudisha macho yake kwa mwanamke yule.

Hakuwapo.

Alirusha macho yake huku na kule pasipo kutumia nguvu. Hakumwona mwanamke yule. Akapuuzia na kuendelea kunywa. Kidogo akanyanyuka toka hapo akaendea meza moja waliyokaa wanaume wawili wakicheza kamari ya karata.

Akaungana na wanaume hao waliowekeana madau ya kawaida katika mchezo wao, haikuzidi dola hamsini kwa kila mtu. Wakacheza mchezo wa kwanza, Mpelelezi akashinda.

Alifurahi kurudisha kiasi fulani cha pesa yake aliyopoteza hapo awali. Alitumai kwa mchezo huu atarejesha hasara yake yote na faida juu.

Hapa ndipo anapendea kamari.

Wakacheza mchezo wa pili, akashinda tena. Moyo wake ukafurahi. Usoni mwake ungeona tabasamu pana, meno yote nje kana kwamba anafanya 'promo' ya mswaki.

Kabla hawajaanza mchezo wa tatu, mtu fulani akaja na kuketi pembeni yake. Mtu huyo alikuwa ameongozana na harufu tamu mno ya kuvutia.

Mpelelezi akashindwa kujizuia. Aligeuza shingo yake upesi kutazama.

Uso kwa uso akakutana na mwanamke yule aliyevalia gauni jekundu. Hakujua kwanini lakini alijikuta akisisimka. Ubaridi wa kipekee ulimpitia toka kichwani ukashukia mpaka miguuni.

Mwanamke yule akawa kama amejua hilo. Akatabasamu. Akazidi kuongeza uzuri wake maridhawa.

Mpelelezi akasema,

"Habari yako, mrembo?"

Mwanamke yule akajibu,

"Nzuri. Naona usiku wako ni mwema leo," alisema akitazama karata na pesa mezani.

Mpelelezi akatabasamu.

Alimjibu,,

"Naam. Natumai utakuwa usiku mzuri."

Mwanamke yule akatikisa kichwa na kumpongeza.

Alisema,

"Wewe si mtu wa San Fransisco."

Mpelelezi akamuuliza amejuaje hilo? Mwanamke huyo akamweleza kuwa ni mara yake ya kwanza kumwona katika ukumbi huo wa starehe.

"Ni kweli," Mpelelezi akakiri na kuongezea, "lakini mimi huwa najihisi mwenyeji popote pale ninapokuwa katika kumbi hizi. Haijalishi mji gani."

Mwanamke akastaajabu kiustaarabu.

"Kweli?"

"Ndio, kweli," Mpelelezi akamjibu kwa uhakika. Basi mwanamke huyo akamtaka aungane naye katika mchezo unaofuata. Alikuwa na hamu ya kuona uwenyeji wa Mpelelezi huyo.

Mchezo ukaanza.

Kila mtu alipata karata zake akiamini akizicheza vema basi ataweza kuibuka kinara, kazi ikabakia kwenye 'timing' na matumizi ya akili binafsi.

Kila mtu akacheza karata yake ya mzunguko wa kwanza. Kwa tahadhari tena, kila mmoja akacheza mzunguko wake wa pili.

Macho yalikuwa yanazunguka, kila mmoja akimtazama mwenzake usoni. Kila mmoja akijaribu kusoma saikolojia ya mwenziwe.

Kwenye hilo, Mpelelezi alikuwa bora zaidi, hata yeye mwenyewe aliamini hivyo.

Kwa kupitia macho ya kila mmoja, aliweza kubaini kinachoendelea katika vichwa vyao akapanga karata zake vema.

Wakaenda mzunguko wa tatu, sasa ikabakia mizunguko miwili ya mwisho. Mizunguko ya kuamua mshindi. Hapo Mpelelezi akapiga mahesabu yake kuwa kila kitu kipo sawa. Anachongoja ni muda tu ufike.

Muda ulipowasili, akajikuta akipigwa na butwaa. Hakuamini macho yake. Mwanamke yule mrembo alimaliza mchezo kwa karata yenye nguvu dhidi ya ile aliyokuwa ameishikilia kwa matumaini.

Akajiaminisha huenda ni bahati.

Wakacheza mchezo wa nne. Mwanamke akashinda. Wakacheza wa tano, mwanamke akashinda tena. Kila mara Mpelelezi alipojitahidi, kusoma akili ya mwanamke huyo alifanikiwa.

Lakini kila unapofika mwisho wa mchezo ndipo anajikuta alijidanganya. Hakujua kitu. Alichezewa shere.

Mwisho wa siku, akajikuta anapoteza pesa za kutosha. Kila alipotaka kucheza ajirejeshe mchezoni, akajikuta anapoteza zaidi.

Kuja kufahamu hamna matumaini tayari alishakawia.

Alimtazama mwanamke yule, asiamini yaliyotokea mbele ya macho yake. Hakuwahi kuchakazwa kiasi hiki. Achilia mbali kuchakazwa na mwanamke.

Alimuuliza mwanamke huyo,

"Wewe ni nani?"

Mwamamke akatabasamu. Akamkumbusha Mpelelezi kuhusu ugeni wake ndani ya jiji la San Fransisco. Alimuambia kama angekuwa si mgeni basi angeshamwepuka kucheza naye tangu mapema.

Mpelelezi akataka kujua nini siri ya mafanikio ya mwanamke huyo. Alijawa na hamu iliyoambatana na mshangao. Alisihi sana.

Mwanamke akamtazama na kumweleza kuwa kama angetaka hilo, basi waonane hapo kesho yake.

Majira kama hayo.

Baada ya hapo, akabusu hewa akimlenga Mpelelezi, alafu akaenda zake.

Ama!

Mpelelezi akamsindikiza kwa macho mpaka alipoyeya katika mboni zake.

**

Queens, New York. Olympus Printing Press

Saa Moja Asubuhi.

Hilda alitazama nyuma yake alafu akainamia meza ya Richie. Macho yake ameyakodoa. Uso wake umeparamiwa na mashaka.

Akauliza,

"Richie, hukuona 'calls' zangu zote?"

Richie, ambaye muda wote huo alikuwa anatazama tarakilishi yake kana kwamba hajamwona Hilda, akasafisha koo na kutengenezea tai shingoni.

Leo alikuwa amejinyonga koo.

Shati lake pana na jeupe lenye mikono mifupi lilimfanya aonekane kama mtu aliyeongezeka uzito.

Alisema,

"Niliziona lakini sikuona haja ya kupokea."

Hilda akatazama tena nyuma yake alafu akamsogelea Richie kwa ukaribu. Alivuta kiti akaketi.

Akasema,

"Richie, ungejua ni namna gani nilivyohangaika jana wala usingesema hayo maneno. Nilitaka kweli kuongea na wewe."

Richie akamtazama na kumwambia:

"Kama ungelitaka, tungeliongea tulipokuwa njiani. Nilikusihi lakini haukutaka. Hata nilipokugusia jambo lako bado ulienda. Nini kimekufanya ukabadili mawazo yako?"

Hilda akamshika mkono Richie.

Richie akas'kia baridi kali limempitia. Hakuelewa baridi hilo limetokea wapi kwa ghafla namna hiyo. Ni kana kwamba mikono ya Hilda ilitokea kwenye jokofu kuu la kisasa.

Hilda akasema taratibu,

"Richie, hamna chochote nilichofanya kwa lengo la kukuumiza. Laki ... Lakini, Richie, ulijuaje kuhusu haya mambo yote? Au kukulipia kwangu huduma ya 'speech-language pathologists' ili kurekebisha kigugumizi ulichonacho ndo' kulikushtua?"

Richie akatabasamu.

Akamweleza Hilda kuwa hilo sio jambo kubwa japokuwa lilizidi kumwaminisha juu ya upataji mkubwa wa pesa wa mwanamke huyo.

Akamweleza kuwa maongezi yote baina yake na boss amekuwa akiyasikia hivyo hamna cha kuficha. Anajua kila kitu.

Kwa kumwaminisha hilo, akamweleza Hilda mambo kadha wa kadha ambayo ana ufahamu nayo. Hilda akaondoa shaka kabisa juu ya ufahamu wa bwana Richie. Aliamini kwa dhati bwana huyo anajua kila jambo hivyo sasa anaweza kuwa huru mbele yake.

Hilda, akiwa amenyong'onyesha sura, akamweleza Richie kuwa jana usiku hakupata kulala kabisa. Hata kuna muda akiwa mwenyewe anapatwa na milipuko ya hofu.

Alisema,

"Richie, nahisi vibaya. Sikuwahi kukutana na mtu ambaye kazi yake nilikuwa naifanya. Nakuja kupata taarifa ni kifo chake tena akihusishwa na madawa ya kulevya. Kama haitoshi, bado naambiwa kazi itaendelea kama kawaida. Kazi ambayo hata sielewi haya ninayoyaandika na kunakili. Vipi tukija kuonekana ni washirika wa wahalifu?"

Macho ya Hilda yaligeuka kuwa mekundu na mabichi. Uso wake ulianza kubadirika rangi kufanania na nyanya iliyokwiva.

Aliendelea kuongea kidogo, mlango ukafunguliwa akaingia Bryson. Bwana huyo alikuwa amebebelea mkoba mkononi, mwilini kuna shati na suruali ya kitambaa rangi ya bluu.

Alisalimu akapita zake. Hilda alikuwa amempa mgongo hivyo hakupata nafasi ya kumwona usoni.

Kwasababu ya ujio huo basi, maongezi yao yakaishia hapo wakiahidiana kuonana baadaye.

Hilda akamtumia Richie baadhi ya kazi alizofanya, na mwanaume huyo katika nafasi yake akawa anazipitia.

Alipitia kazi hizo asielewe ni nini kilichokuwa kinalengwa. Taarifa nyingi zilikuwa za kisayansi zikiwa zimeambatana na michoro mingi ya kuonyesha 'chemical compositions'.

Michoro ambayo kwa Richie ilikuwa ni vitu vigeni.

Alifikiria na kutengeneza nadharia tofautitofauti kuhusu taarifa hizo lakini bado hakuona tija.

Mwishowe, baada ya masaa kadhaa, akapata mawazo mawili ya kuyatazama kwa jicho la tatu.

Moja, alifikiria huenda taarifa hizo za kikemia zinahusu mifumo ya utengenezaji wa madawa ya kulevya. Wazo hilo lilimjia sababu ya kutazama mahusiano ya mhusika, yaani Ferdinand, na kazi yenyewe.

Pili na mbaya zaidi, akawaza kutafuta majibu ya taarifa zile kwa kutumia watu wa nje. Yaani, watu baki ambao wana maarifa na nyanja hii ambayo kazi imetokea. Kumaanisha wanakemia.

Akiwa anawaza hili, picha ya mmoja wa rafiki zake aliosoma nao shule ya upili ikamjia.

Aliamini huyo atamsaidia kufungua hizi 'code' ili ajue kama yaliyomo yamo.

**
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 14


Na Steve B.S.M



Brookhaven, New York.

Saa tano asubuhi

Dr. Lambert aliufungua mlango akaingia ndani ya ofisi. Ndani humo kulikuwa na meza tano, kila moja ikiwa na kiti chake na tarakilishi zenye visogo bapa.

Akaendea meza moja, upande wake wa kusini, akatundika koti lake jeupe katika mgongo wa kiti kisha akaketi kwa kuutupa mwili.

Akashusha pumzi ndefu.

Akaunyoosha mgongo wake, ukalia kah-kah-kah kisha akashusha pumzi tena.

Alikuwa amechoka. Umri nao ulichangia. Kama si serikali kumwomba aongeze mwaka mmoja katika mkataba wake kwasababu ya umuhimu wake kazini basi angekuwa kijijini huko akitazama ng'ombe na kula pensheni, ama amekaa nyumba tulivu akicheza na wajukuuze.

Alibofya kibodi, tarakilishi ikawaka. Upesi akachezesha vidole vyake kunakili taarifa fulani katika mashine hiyo.

Vidole vilikuwa na wepesi sana. Macho yake yakitazama kioo, vidole hivyo vikachapa taarifa iliyotoka kichwani pasipo kusoma popote pale.

Akiwa anaandika hayo, mlango ukafunguliwa wakaingia wanaume wawili waliokuwa wamevalia makoti meupe kama lile la Dr. Lambert.

Wanaume hao walikuwa wanateta mambo yao lakini punde walipoingia ndani, kila mmoja akajigawa kuendea meza yake.

Mmojawao alikuwa ni kijana wa makamo ya miaka thelathini ya mapema wakati mwingine akiwa wa makamo ya miaka arobaini hivi. Ndevu zake amezichonga 'O' na kichwa chake hakina nywele hata moja.

Waliketi kukawa kimya. Kidogo, mmoja akaja na kuungana nao. Alikuwa ni bwana mfupi sana, mzee wa makamo ya miaka hamsini hivi. Nywele zake zilikuwa mchanganyiko wa nyeusi na nyeupe. Alisalimu kisha akaketi naye katika sehemu yake.

Bwana huyo alipokaa tu, mjadala ukaibuka.

Ulikuwa ni mjadala kuhusu mazingira yao mapya ya kazi baada ya taarifa ile ya kuvuja kwa data kutuhumiwa kutoka maabara hii.

Walijadili namna gani kazi ilivyokuwa ngumu wakisimamiwa kila eneo, lakini pia namna gani kamera zilizopachikwa kila mahali zinavyowanyima faragha zao.

Walienda mbali wakajadiliana juu ya mhusika wa hayo yote. Waliongea wakimwonea huruma bwana huyo punde atakapokamatwa.

Wakiwa katika mjadala huo, Dr. Lambert alikuwa kimya sana. Macho yake yalikuwa yanatazama tarakilishi huku vidole vikichapa kazi mfululizo.

Ni kana kwamba alikuwa katika dunia yake ya pekee. Hakuskia wala kujali kilichokuwa kinaendelea hapa.

Kidogo simu yake ikaita. Watu wote waliokuwa wanaongea wakanyamaza kutazama. Simu iliwakatisha. Dr. Lambert aliitoa simu yake mfukoni akaangalia nani anapiga.

Namba ngeni.

Mojamoja akili yake ikampeleka kwa mwanamke Mitchelle kwani ndiye mtu pekee ambaye ana hizi namba zake anazozibadili mara kwa mara. Kiuhalisia, mwanamke huyo ndiye anayempatia namba hizo hivyo kumtafuta ni jambo la wakati tu.

Hakupokea, alichofanya alizima sauti kisha akairejesha simu mfukoni. Mazingira hayakuruhusu.

Simu ikaendelea kuita kwa kunguruma huko mfukoni mpaka ikakata. Wale wengine ndani ya ofisi wakaendelea na shughuli zao, kila mmoja akiwa na yake.

Simu ikaita kwa mara ya pili. Muda huu ni Dr. Lambert pekee ndiye alikuwa anajua kwani sauti haikutoa. Simu ilitetemeka ndani ya mfuko wake akivumilia kana kwamba hamna kitu kinachotokea.

Alivuta muda kidogo, kama dakika tatu, kiendelea na kazi yake alafu ndo' akaamka na kuelekea zake nje.

Akiwa anakatiza, bwana yule mfupi aliyekuwa wa mwisho kuingia ofisini alimtazama akamuuliza kama kila kitu kipo sawa. Dr. Lambert akatikisa kichwa.

Alisema,

"Hamna shaka."

Akafungua mlango na kwenda zake.

Akatembea upesi kuimaliza korido, ndani ya muda mfupi akawa amefika mbele ya mlango wa choo. Akatazama kushoto na kulia kwake, kulikuwa salama. Hakukuwa na mtu hapo ispokuwa kamera tu.

Akaingia ndani.

Humo ndo' palikuwa sehemu pekee ambamo hamna kamera.

Dr. Lambert akaingia ndani ya kijsehemu kidogo cha kujisaidia haja kubwa, huko akatoa simu yake mfukoni na kupiga.

Alijiaminisha humu yu salama.

Simu ikaita kidogo kisha ikapokelewa. Ilikuwa ni sauti ya kike kwa upande wa pili. Sauti ya Mitchelle.

Mwanamke huyo alimkumbusha Dr. Lambert kuhusu makubaliano yao ya msingi. Alimtaka dokta amtumie dawa na nyaraka muhimu haraka iwezekanavyo. Afanye atakavyojua lakini siku hiyo ama ijayo isipite pasipo yeye kupata mahitaji yake.

Lakini atazipataje?

Dokta alisema,

"Sifahamu ulipo. Uliniambia utanitaarifu lakini ukakaa kimya."

Mitchelle akampatia anwani yake, pia akamsihi autume mzigo huo kwa njia ya DHL. Aliamini ataupata kwa upesi na kwa usiri anaoutaka.

Dokta akaridhia kila jambo, lakini ndani yake alikuwa na shaka. Alihusha pumzi fupi, akasema,

"Mazingira yangu ya kazi yamekuwa magumu sana hapa karibuni, Mitchelle. Ulinzi umekuwa mkubwa sana kuingia na kutoka. Hata humu ndani, hamna kinachofanyika pasipo kuonekana na kamera lukuki.

Kule nyumbani napo walibeba kila kitu muhimu nilichokuwa nahitaji, hivyo utakapoona nasuasua basi fahamu mazingira ni magumu."

Mitchelle hakutaka kuelewa.

Alisema,

"Dokta, unakumbuka makubaliano yetu ya kazi? Tulikubaliana kazi itafanyika kwa namna yoyote ile, kiangazi ama masika, na hiko ndo' kinanifanya nikulipe maelfu ya madola kila uchwao. Unavyoniambia mazingira magumu, nashindwa kukuelewa, dokta. Kwahiyo mimi naishije?"

Dokta akakosa cha kujitetea. Akabakia kimya, moyo wake ukiwa unaenda kwa kasi. Uso wake umeparamiwa na mashaka na maulizo.

Mitchelle akamalizia kwa kusema,

"Nangoja. Kaa ukijua namaanisha hilo."

Kisha akakata simu.

Dr. Lambert akafuta jasho kwenye paji lake la uso. Akaketi juu ya choo cha kukaa kilichokuwa pembeni yake.

Akaketi akiwaza.

Mazingira ya hapa yalikuwa yako kimya sana. Dokta alipotelea kwenye mawazo akitazama namna gani anaweza kufanya.

Kila alichowaza kichwani kiligoma na kuishia kufeli. Hakuona njia kwa sasa. Kila alipofikiria ulinzi ule wa kamera na wana usalama, alichoka kabisa. Alihisi kichwa kinapasuka.

Alinyanyuka na kutoka humo alimo, akaufuata mlango wa kutoka ndani ya choo.

Akaukuta mlango ukiwa wazi.

Alisimama hapo akajiuliza kama mlango huo hakuufunga alipoingia ndani. Hakukumbuka vema lakini hisia zake zilimweleza kuwa aliufunga mlango huo. Hakuwahi kuingia ama kutoka chooni akauacha mlango wazi.

Kwa ukimya uliopo ndani ya vyoo, aliamini hakukuwa na mtu aliyeingia wala aliyekuwamo humo isipokuwa yeye mwenyewe tu.

Akaelekea ofisini upesi.

Humo akakakuta wenziwe wote kasoro mmoja. Yule mwanaume mfupi hakuwapo. Moyo wake ukamjaa shaka.

Akauliza,

" Ameenda wapi huyu jamaa?"

Hakuna aliyekuwa anajua. Walijibu hapana wakiendelea na kazi zao. Walionyesha kutingwa na kazi nyingi.

Dokta akiwa amesimama hapo, kidogo mlango ukafunguliwa akaingia bwana aliyekuwa anamuulizia.

Akamuuliza,

"Ulikuwa wapi?"

Bwana huyo akastaajabu na hilo swali. Aliyatoa macho yake akimtazama dokta.

Akamuuliza,

"Bwana, kuna tatizo?"

Dr. Lambert akamtazama pasipo majibu. Wakatazamana kwa kama sekunde tano kama majogoo waliohitilafiana.

Bwana huyo akasema akiwa anaendea kiti chake,

"Niliitwa na mkuu ofisini."

Akaketi na kumtazama dokta.

Akamuuliza,

"Ulikuwa una shida na mimi?"

Dokta hakujibu. Alifuata meza yake akaketi.

Alitazamatazama hapo kwa muda mchache kabla hajashika tena tarakilishi yake kuendelea na kazi. Muda si mrefu akawa amemaliza.

Akatoka kwenda kujipatia chakula cha mchana.

***

San Fransisco, California. Chuo kikuu cha Stanford.

Saa saba mchana

Mpelelezi alikuwa amekaa kwenye moja ya viti vya chuma vilivyokuwa nje ya ofisi ya 'Dean of Students' wa chuo hiki.

Mkononi mwake alikuwa ameshikilia simu, akiipekua taratibutaratibu kusogezea muda.

Bwana huyo alikuwa amevalia suruali nyeusi, ile aliyovaa jana yake, kiatu kilekile lakini juu akiwa amebadilika. Alivalia shati la kahawia la mikono mifupi, mkononi ana saa yake ya kila siku.

Kidogo, bwana mmoja, mtu mzima wa makamo ya miaka thelathini na tano, akatokea akijia ofisi hii. Bwana huyo alikuwa katika mwendo wa ukakamavu. Juu amevalia shati na kizibao cha sweta rangi ya damu ya mzee.

Uso wake wa wastani ulibebelea miwani safi ya macho. Pua yake ndefu, mdomo wake una 'lips' nyembamba.

Kwa kumtazama, Mpelelezi akaamini kuwa huyu ndiye aliyemfuata. Upesi akanyanyuka na kumsalimu kisha akajitambulisha.

Dean akamkaribisha ofisini kwake.

Waliingia, Mpelelezi akahudumiwa kwa kahawa nzito ya moto kusindikizia maongezi yao.

Pasipo kupoteza muda, Mpelelezi akaeleza haswa kilichomleta hapo. Mguu wake ulilenga kupata taarifa kumhusu mwanamke ambaye alisoma hapo akaishia kujiua.

Alimkabidhi Dean picha ya mwanamke huyo pamoja na majina yake matatu. Akamwambia ampatie yale yote anayoyajua kumhusu mlengwa huyo.

Dean alipotazama picha na kuskiza alichoambiwa, akatengenezea kwanza miwani yake usoni. Akatulia kidogo kabla hajafunguka kumwambia Mpelelezi kuwa mwanamke huyo alipata kusoma hapo miaka mingi iliyopita lakini hakumaliza masomo yake akajiua.

Mwanamke huyo kwa sifa alikuwa ni mtu wa kujitenga akibahatika kuwa na rafiki mmoja tu. Rafiki ambaye wengine walistaajabu kumwona ni namna gani alifaulu kuwa karibu na mwanamke huyo.

Mbali na hayo, Dean akamwambia Mpelelezi namna gani mwanamke huyo alivyokuwa mwerevu mno darasani. Ingawa alikuwa ni mtu wa kujitenga sana, akijiepusha na makundi ya majadiliano, bado alama zake zilikuwa juu mno.

Alimpatia Mpelelezi rekodi ya kitaaluma akaitazama na kukiri yale anayoambiwa ni kweli. Mitihani pekee ambayo mwanamke huyo alifeli, ilikuwa ni kwa kupata alama B. Mengine yote yalikuwa ni A na A+.

Dean akasema,

"Kwa mwanafunzi mwenye alama hizi katika kozi yake hii, ana 'future' ya kuaminika. Ni ajabu mtu kama yeye kuyatoa yote sadaka kwa kujiua."

Mpelelezi akauliza,

"Kuna kingine cha ziada?"

Dean akamwambia hana jambo la zaidi ya hayo, mengine anaweza kuyapata kwa msimamizi wa hostel ambamo binti huyo alikuwa akiishi.

Akampatia mawasiliano yake, Mpelelezi akaelekea huko. Ndani ya muda mchache akawa yu pamoja na mwanaume aliyevalia kapelo nyekundu yenye chapa ya chuo cha Stanford.

Bwana huyo mzee mwenye kijitambi kilichoshikiliwa na 'form six' nyekundu yenye chapa ya chuo, alikuwa na masharubu meupe na mwanya mpana.

Alimkaribisha Mpelelezi akimweleza amepata taarifa zake toka kwa Dean. Akamwahidi kumpa ushirikiano wake wa dhati.

Akamweleza Mpelelezi juu ya namna alivyomjua mlengwa wao kisha akamsaidia kupata namba ya simu ya yule ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu. Aliamini huko atapata vya ziada ambavyo wao hawavifahamu.

"Lakini," bwana huyo alisema, "kifo cha huyu binti kilinigusa sana. Namna alivyokuwa anaishi na wenzake, hakuwa mtu wa makuu na kujivuna, na sikuona akiuchukulia upweke wake kama ulemavu. Naamini alikuwa anafurahia kuwa peke yake zaidi. Nina mwanangu mwenye sifa hizo.

Yeye hupenda kujitenga akiutumia muda wake mwingi chumbani. Mwanzo nilikuwa na mashaka sana lakini nilikuja kugundua kuwa, kwa upande wake alikuwa sawa kabisa."

Bwana huyo akamalizia akisema,

"Mara kadhaa nilikuwa namwona akitabasamu awapo mwenyewe au awapo na kitabu. Tabasamu lile la dhati. Lakini ilikuwa aghalabu kumwona akifanya hivyo akiwa na watu wengine isipokuwa rafiki yake tu."

Mpelelezi akamalizana naye na kuondoka zake.

Aliita Uber ikaja ndani ya muda mfupi. Akajiweka viti vya nyuma, safari ikaanza.

Akiwa humo, akajaribu kupiga simu ya mwanamke yule rafiki wa mlengwa wake. Simu ikaita kisha ikapokelewa.

"Nani?"

Sauti ya kiume ilimuuliza, akastaajabu.

Alikata akaitazama namba hiyo kwa uhakiki. Akabaini ilikuwa sawa kabisa. Akapiga tena.

"Wewe nani?"

Sauti ya kiume ikamuuliza. Sauti ileile ya mwanzoni.

**
 
Back
Top Bottom