TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 12
Na Steve B.S.M
Queens, New York. Olympus Printing Press.
Richie alimtazama Hilda kwa muda kidogo kisha akanyanyuka kumfuata mwanamke huyo alipo.
Kwa macho yake ya nyama, Hilda hakuwa sawa na aliona kuna haja ya kumjulia hali yake kwa ukaribu.
Alimuuliza,
"Kuna tatizo?"
Hilda akatikisa kichwa kukataa, lakini sura yake ilimsaliti.
Richie akavuta kiti kilichokuwepo pembeni, akaketi karibu naye.
"Nini kinakusumbua, Hilda?"
"Nadhani ni njaa."
Hilda alisema akitabasamu. Alimtazama Richie machoni kwa kumkodolea.
"Usijali, hata hivyo nilikuwa nimepanga kukutoa lunch leo hii, lakini niko serious, Hilda. Nimekuona muda tu ukiwa umepoa sana."
Hilda akatikisa kichwa chake kwa mbali. Hakutaka kukiri hilo. Alinyanyuka akaendea mlango, akatazama nje na kurejea ndani.
Alimuuliza Richie aliyekuwa anamtazama,
"Vipi, boss aliongea na wewe?"
Richie akatikisa kichwa. Akasema hakujua bwana huyo alikuwa wapi kiasi kwamba hakufika kazini mpaka muda huo, kisha hapo ndo' akamuuliza Hilda kama ujio wa bwana huyo ndo' chanzo cha mawazo yake.
Hilda akajibu,
"Hapana."
Ila akaongezea swali, "vipi kama amekumbwa na tatizo?"
Kabla Richie hajajibu, mlango wa ofisi ukafunguliwa. Alikuwa ni Mr. Bryson.
Aliingia akiwa ameshikilia koti lake mkononi. Alikatiza kana kwamba hamna mtu hapa ndani lakini alipofika katika mlango wa kuingia ofisini mwake, akamwita Hilda.
Akamsihi aje ofisini kwake haraka.
Kidogo Hilda akawa ameungana naye, akiwa ametulia katika kiti cha mgeni.
Hapo ndo' Bryson akavuta kwanza pumzi kisha akamwambia Hilda kuhusu kazi yao ya siri.
Alisema,
"Kama nilivyokuwa nimekuambia, yule bwana aliyekuwa anatuletea kazi na pesa, amefariki katika ule mlipuko maarufu New York."
Akaongezea,
"Na kwa taarifa zilizosambaa bwana huyo alikuwa anahusika na shughuli za madawa ya kulevya, kwahiyo nadhani ushapata picha kamili."
Hapa Hilda alikuwa ametulia tuli kama maji ya mtungi lakini ndani yake alikuwa na hofu kubwa.
Alitaka kuongea lakini Bryson akamkatisha.
Alimuuliza,,
"Unakumbuka maagano yetu, Hilda?"
Hilda hakujibu kitu. Alinyamaza kimya kana kwamba hakusikia alichoulizwa.
Bryson akarudia kuuliza,
"Hilda, unakumbuka maagano yetu?"
Muda huu sauti yake ilikuwa kali na yenye uzito. Uso wake ulimaanisha kile alichokuwa anaongea.
Hilda akapapatuka.
Uso wake ukiwa umejawa uoga, akajibu,
"Ndio. Nayakumbuka."
Bryson akasema,
"Vema. Sasa ndo' muda wa kuyafanyia kazi."
Akamweleza mwanamke huyo kwamba wataendelea na kazi hiyo waliyopewa mpaka pale itakapokoma. Haitajalisha ni kitu gani kitakachotokea katikati.
Lakini katika hayo, Hilda akauliza,
"Sasa ni nani atakayekuwa anatuletea kazi kama bwana huyu amekufa?"
Bwana Bryson akamweleza kuwa alishaongea na mhusika mkuu. Kazi itaendelea kuja kama kawaida lakini hivi sasa wakitumia njia ya posta kwaajili ya usalama zaidi.
Baada ya hapo, bwana Bryson akamtaka Hilda akaendelee na kazi yake kwani ana shughuli kadhaa za kufanya.
Hilda akaamka. Kabla hajaanza hatua, mlango ukafunguliwa. Kutazama alimwona mwanamke mwenye sura nyekundu akiwa amesimama mlangoni.
Mwanamke huyo alikuwa amevalia gauni refu la kijani, mikono ya nyavunyavu. Kichwani mwake amebana nywele na kibanio cheusi kilichozunguka kichwa.
Alikuwa ni mke wa Bryson.
Aliuliza akimnyooshea kidole Hilda,
"Wewe ndiye Hilda, sio?"
Hilda asijibu akamtazama Bryson. Naye Bryson akamtazama mwanamke huyo kabla hajahamisha macho yake upesi kwa mkewe.
Hakuamini alichokuwa anakiona.
Alisimama upesi akamuuliza mkewe,
"Ina maana hukutosheka na ugomvi wa asubuhi?"
Hapa ndo' Hilda na Richie aliyekuwa mlangoni wakapata kufahamu kuwa Boss wao alikawizwa na ugomvi wa nyumbani.
Hilda akataka kutoka awapishe lakini mke wa boss akamzuia.
Alimtaka abaki hapo kwani kinachoendelea kinamhusu.
Bryson, kwa kutumia hekima, alimsihi Hilda atoke ofisini mwake lakini jambo hilo likakumbana na upinzani mkubwa toka kwa mkewe aliyekuwa anamshutumu Hilda kumwaribia mahusiano yake.
Mwanamke huyo alisema,
"Ni nini unaongea na mume wangu mara kwa mara? Ni nini unataka?"
Wakati anasema hayo, alikuwa ametoa macho yake kwa kadiri awezavyo.
Hilda akakosa cha kuongea.
Alihisi ulimi wake umekuwa mzito tani kadhaa. Alitetemeka asielewe kipi cha kufanya.
Baada ya nusu saa alikuwa ameketi kwenye kiti chake, ameshika kichwa chake anawaza. Muda mwingine alikuwa anashituka akisikia sauti kali toka ofisini kwa boss wake.
Alikuja kupata ahueni baadae, mwanamama huyo alipojiondokea.
Bryson akamfuata na kumwomba radhi. Alimwambia mkewe ni mtu wa wivu sana na yeye amekwishamzoea tabu zake.
Lakini akampatia ofa kwa kumwambia,
"Nitakutoa lunch kama tafadhali yangu. Sema unataka kula nini leo hii?"
Kauli hiyo ikachipua tabasamu kubwa kwenye uso mnene wa Hilda. Tumbo lake likanguruma kushangilia. Mate yakamjaa mdomoni ghafla alipowaza chakula kile akipendacho.
Alisikia harufu ya chakula hicho puani mwake.
Mwili ukamsisimka.
Jambo hilo lilikuwa bora zaidi kwa siku yake ya leo ambayo ilikuwa tenge. Japo alishapewa ofa na Richie lakini haikuwa ya uhuru wa kiasi hiki cha kuchagua akipendacho.
Akafanya kazi upesi.
Muda ulipofika, Richie akamfuata akimtaka waende kula naye chakula cha mchana. Bwana huyo, asijue kinachoendelea, alidhani bado ofa yake ipo mezani.
Hilda akamtazama kwa huzuni ya kuigiza.
Alimwambia boss amempatia ofa kubwa ambayo hawezi kuikataa.
Alisema,
"Imagine ameniambia nichague chakula chochote ninachokitaka. Chochote kile!"
Jambo hilo likamnyong'onyesha sana Richie.
Ni muda mchache nyuma alidhania angefaidika na sokomoko lililoibuka kati ya Bryson na mkewe kuhusu Hilda lakini imekuwa tofauti.
Akiwa anawaza kuongozana na mwanamke huyo kwenda mgahawani, pasipo kujali kuhusu ofa yake aliyotoa, mara Bryson akaingia akitokea ofisini mwake.
Akamwambia Hilda waongozane.
Walienda pamoja wakimwacha Richie nyuma amesimama anawatazama.
Hamu ya kula ya mwanaume huyo ikaisha 'hafla. Akaketi kitini kwake akiwaza namna gani tonge lilivyomponyoka karibia na mdomo.
Akafikiria sana.
Baada ya kitambo kidogo, kuna jambo akakubaliana na nafsi yake kulifanya.
Ulikuwa ni muda wa yeye kucheza karata yake bora.
***
Saa Moja Usiku.
Richie alisimama nje ya ofisi ya The Olympus akiwa ameegemea ukuta. Mikono yake miwili ilikuwamo mfukoni mwa suruali, macho yake yakiwa barabarani kutazamatazama.
Kidogo, Hilda akatoka ofisini akamwona bwana huyu.
Alimwambia,
"Nilidhani ushaondoka kitambo!"
Richie akatabasamu asiseme jambo. Wakaongozana wakielekea kusini mwa ofisi yao.
Ulikuwa ni mwendo wa dakika kadhaa kabla hawajaachana kila mtu kushika njia yake.
Richie alimtazama Hilda, akamuuliza,
"Hilda, kuna jambo gani linaloendelea baina yako na Boss?"
Hilda alishtuka. Ni kana kwamba jambo hilo lilikuwa geni kabisa masikioni mwake, ndo amepata kulisikia kwa mara ya kwanza.
"Mimi? Usiniambie na wewe unawaza kama yule mwanamke mwehu?"
"Hapana," Richie akamjibu. "Lakini naamini kuna kitu ambacho mnanificha. Kuna jambo linaendelea nyuma ya mgongo wangu. Sidhani kama ni sahihi ninyi kunifanyia hivyo."
"Hayo ni mawazo yako, Richie," Hilda akajipambanua. "Sijui kwanini unapenda kujipa mashaka kiasi hiko. Nakwambia hiki kitu sio mara ya kwanza na ninahisi inaweza ikawa si mara ya mwisho. Hamna chochote kile."
Richie hakukata tamaa. Akarusha tena ndoano yake,
"Huu ni mwaka wa pili tukiwa pamoja kazini. Kwa miaka yote hiyo sijawahi kuona ukibadilika kiasi hiki, kuwa na ukaribu kiasi hiko na boss. Achilia mbali ratiba tofauti na ilivyokawaida. Unataka kuniambia hayo yote ni kawaida tu?"
Hilda akatikisa kichwa kuridhia.
Alisema,
"Ndio. Kwangu sijaona cha ajabu. Labda ni wewe ndo' umebadilika. Hujawaza hilo?"
Wakaongea maongezi hayo yasiyokuwa na matunda mpaka pale walipofikia mahali pa kuachana kila mtu kushika njia yake.
Hapo ndo' Richie akatupa karata yake dume.
Alisema,
"Najua kila kitu, Hilda. Kila mara nakupa nafasi ya kukiri hilo lakini huioni. Pesa zimekufumba macho kiasi kwamba hujali hata uhai wako."
Aliposema hayo, akajiendea zake na njia tofauti. Hilda akamtazama kwa kitambo kidogo alafu naye akaondoka zake kufuata ya kwake.
Alitembea akiwaza kile alichokiskia toka kwa Richie.
Sauti moja ndani ya nafsi yake ikamwambia amrudie bwana huyo kumuuliza ni nini anafahamu lakini ya pili ikamkataza katukatu. Ilimwambia huenda hiyo ni janja tu ya Richie kumpekenyua.
Kadiri alivyokuwa anatembea ndivyo alizidi kusikia sauti hizo zikigombana ndani yake na hii inayomwonya ikizidi kupata nguvu zaidi.
Lakini atakuwa amejuaje? Hapana, hafahamu. Hapana, hafahamu kitu. Hapa-- akasita.
Alisimama akitoa macho yake. Ni kana kwamba alijiwa na akili timamu hivi sasa. Vipi kama kweli anajua?
Aliwaza mara ngapi bwana huyo alimuuliza kuhusu yeye na boss Bryson. Akakumbuka pia namna gani bwana huyo alivyokuwa anamtazama wakati anamuambia kwamba anajua kila kitu.
Akatia shaka.
Aligeuka upesi akakimbia kurudi nyuma alipotokea.
Kwasababu ya mwili wake mzito hakuweza kukimbia kwa upesi lakini alipambana vivyohivyo.
Alikimbia akisimama na kuhema. Alikimbia tena akasimama na kuhema. Pumzi ilimkata kabisa kifuani. Alihema kana kwamba hatohema tena kesho.
Miguu ilimuuma, kifua nacho kilimbana.
Akatoa simu yake mfukoni. Upesi akatafuta namba ya Richie na kuipiga.
Simu iliita bila kupokelewa. Ikakata.
Akarudia tena.
"Pokea, Rich. Pokea!"
Simu haikupokelewa.
Akapiga kelele.l za hasira.
***
Bronx, New York.
Saa nne ya usiku.
Babyface alivuta mkupuo wake wa mwisho wa sigara kisha akaitupa chini na kuisigina kuizima.
Akatema moshi kwa madaha. Moshi ukafunika uso wake na kupotelea mbali.
Bwana huyu alikuwa ameegemea gari, mkono wake mmoja upo mfukoni. Kama ilivyo mara nyingi, alikuwa amevalia suti na tai nyeusi. Nywele zake zimetengenezwa vema zikihakisi mwanga mkali wa mataa ya majengo marefu yaliyopo hapa.
Alitazama saa yake, akatoa simu yake mfukoni na kupiga namba ile aliyoitunza kwa jina 'BIG'. Kidogo tu simu ikapokelewa, Babyface akasema,,
"Unanichelewesha."
Akajibiwa na sauti tokea upande wa pili wa simu,
"Tazama kushoto kwako."
Akatazama na kumwona mwanaume mmoja akiwa anamjia. Akarejesha simu yake mfukoni na kungoja.
Kidogo mbele yake akawa amesimama bwana mmoja mnene. Nywele zake fupi, macho madogo. Shingoni amejaza mikufu na mkononi ana pete na bangili za dhahabu.
Bwana huyo alikuwa amevalia suti kachumbari iliyomkaa vema na mwili wake kama kisiki cha mbuyu.
Ukimtaza vema, utamkumbuka.
Alikuwa ni bwana yule aliyecheza kamari na Mpelelezi siku ile katika ukumbi wa Resorts World Casino. Mchezo ambao ulipelekea ugomvi na majanga.
Bwana huyo akamsalimu Babyface kwa kupeana mikono kisha wakafungua maongezi yao mafupi.
Katika maongezi hayo, BIG akamlaumu Babyface kwa yale yaliyotokea siku ile.
Alisema,
"Haikuwa na haja ya kutuponda kiasi kile, kaka. Mwili wangu mpaka sasa una maumivu na mmoja wetu bado yuko hospitali hapa tunapoongea. Amelazwa hoi."
Babyface akaomba samaha nyepesi kisha akazama mfuko wake wa nyuma akatoa pochi nene nyeusi.
Aliifungua pochi hiyo akatoa dola kadha wa kadha akamkabidhi BIG.
BIG akahesabu pesa hizo.
"Najua tulikubaliana kiasi hiki cha pesa lakini hasara kwetu ni kubwa sana, mkuu. Tafadhali lizingatie hilo."
Babyface akaongeza pesa maradufu kisha akasema,
"Nadhani inatosha, sio?"
BIG akatikisa kichwa kuridhia. Aliziweka pesa hizo mfukoni mwake akaaga akiwa amekubaliana na bwana huyo miadi mingine ya unywaji.
Babyface akaingia ndani ya gari lake. Kabla hajaondoka, simu ikaita. Akafura. Alidhani ni BIG aliyetoka kuteta naye.
Alipotazama akaona ni mwingine. Upesi akapokea akisema, "nipe ripoti."
Bwana wa upande wa pili akamweleza akisema,
"Mpelelezi ametua ndani ya jiji la San Fransisco,California."
Babyface akahamaki.
"Are you serious?"
Aliyatoa macho yake bora ya mshangao.
Alikata simu upesi, akawasha gari akiondoka haraka kama mwendawazimu.
**