Na. Mohammed Said
Mwaka wa 1951 wakati Dossa na wenzake wapo katika juhudi za kuipa uhai mpya TAA Dossa aliandikiwa barua na V.M. Nazerali aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria akimuomba Dossa aunge mkono juhudi zake na za Ivor Byaldon na Brig. Scupham za kutaka kuunda chama cha siasa kitachowashirikisha watu wa rangi zote. Bayldon na Brig. Scupham walikuwa kama alivyokuwa Nazerali, wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria.
Wanasiasa wengine walioombwa kuunga mkono juhudi hizi walikuwa Chifu Kidaha Makwaia, Liwali Yustino Mponda wa Newala, Dr. Joseph Mutahangarwa, Chifu Abdieli Shangali wa Machame, Chifu Thomas Marealle wa Marangu, Chifu Adam Sapi Mkwawa, Chifu Harun Msabila Lugusha, Dr. William Mwanjisi, Abdulkarim Karimjee, Dr. Vedas Kyaruzi, Liwali Juma Mwindadi, H.K.Viran, Stephen Mhando, Ally Sykes na Abdulwahid Sykes. Dossa na wenzake waliikataa ghilba hii kwa kuwa lengo lao lilikuwa ni kuanzisha chama cha siasa cha Waafrika wa Tanganyika kwa minajili ya kudai uhuru.
Mwalimu Nyerere alipofika Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka wa 1952 kama mwalimu wa shule ya St. Francis' College, Pugu hakuna mtu aliyekuwa anamjua au kupata kusikia habari zake katika ulingo wa siasa. Kassela Bantu ambaye alikuwa akijuana na Nyerere kwa siku nyingi alimchukua Nyerere kwa Abdulwahid Sykes kumtambulisha. Wakati ule Abdulwahid alikuwa Rais wa TAA. Nyerere mara moja akajiunga na baraza la siasa lililokuwa likifanyika Mtaa wa Mbaruku nyumbani kwa Dossa. Ikawa kila Jumapili Nyerere anakuja kutoka Pugu kuja kumtembelea Dossa.
Ilikuwa katika baraza hii ndipo Nyerere alipokutana na wanasiasa wengi wa wakati ule kama Ramadhani Mashado Plantan aliyekuwa anamiliki gazeti lililokuwa likijulikana kama Zuhra, John Rupia, Dunstan Omari, Zuberi Mtemvu na wanasiasa wengine. Fikra za Nyerere za kudai uhuru zilisikika kwa mara ya kwanza kupitia kalamu ya Mashado Plantan na gazeti lake la Zuhra lililokuwa likitoka kila siku ya Ijumaa. Fikra za Nyerere ziliingiza msisimko mpya katika baraza lile na haukuchukua muda mwaka 1953 uongozi wa ndani ukampendekeza agombee urais wa TAA.
Dossa anasema ingawa wao kwa kuwa karibu na Nyerere walikuwa wamekiona kipaji chake cha uongozi, wanachama wengi hawakumkubali mara moja na ndiyo maana katika uchaguzi wa TAA uliofanyika Arnautouglo Hall tarehe 17 Aprili, 1953 kati ya Abdulwahid aliyekuwa Rais na Nyerere aliyekuwa anagombea dhidi yake, Nyerere alishinda uchaguzi ule kwa taabu sana. Haukupita muda chama kikaanza kuzorota na mwisho kikafa. Dossa anakumbuka kuwa yeye alikuwa anawapitia viongozi kwenda kwenye mkutano. Akipiga honi ili mtu atoke waende mkutanoni kiongozi alimtuma mkewe atoke nje na aseme kuwa hakuwepo nyumbani.
Dossa anasema ilikuwa baada ya kushauriana na Abdulwahid, Makamu Rais wa TAA ndipo lilipokuja wazo kuwa ni lazima wapate nguvu ya wazee wa Dar es Salaam ili kukifufua chama.Hivi ndivyo TAA katika miaka ya mwisho ya uhai wake ilipokuja kupata kuungwa mkono na wazee wa Dar es Salaam na kupelekea kuundwa kwa Baraza la Wazee wa TANU mwaka 1955 chini ya mwenyekiti wake Sheikh Suleiman Takadir. Nyerere amepata kusema kuwa alikuwa Dossa ndiye aliyemfahamisha aache kuvaa kaptula kwa kuwa sasa atakuwa akitoka mbele ya watu wazima na hiyo si adabu nzuri.
Dossa alikuwa kati ya wale wazalendo watano, Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, John Rupia na Julius Nyerere waliokutana ndani ya ofisi ya TAA new Street (sasa Lumumba Street) katika miezi ya mwisho ya 1953 na kwa pamoja wakapitisha azimio la siri la kuibadili TAA kuwa chama cha wazi cha siasa na kukipa chama hicho jukumu la kuiongoza Tanganyika katika kudai uhuru wake. Hili ndilo lililokuwa azimio la kwanza la busara katika historia ya Tanganyika. Azimio la pili la busara ni lile la Tabora la mwaka 1958.
Tarehe 7 Julai, 1954 wazalendo hawa wafuatao wakakutana Dar es Salaam kubadili Katiba ya TAA ili kuanzisha chama cha TANU: Dossa Aziz, Abdulwahid na Ally Sykes, Tewa Said Tewa, Patrick Kunambi, Kasella Bantu, John Rupia, Julius Nyerere, C.O. Millinga,Germano Pacha, Joseph Kimalando, Japhet Kirilo; Abubakar Ilanga, L.M.Bugohe, Saadan Abdu Kandoro, S.M. Kitwana na L.M. Makaranga. Dossa Aziz kadi yake ya TANU ni namba 4 iliyotolewa na kusainiwa na Ally Sykes.
Haukupita muda mrefu TANU ikampeleka Nyerere Umoja wa Mataifa. Tarehe 17 Februari, 1955 Nyerere aliondoka Dar es Salaam na kwenda New York kuhutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa na ndani ya mkoba wake hakuwa na hotuba nyingine ila yale mapendekezo aliyopewa Gavana Edward Twinning mwaka wa 1950 na uongozi wa TAA.Nyerere aliporudi nchini alikuta umati mkubwa wa wananchi unamsubiri uwanja wa ndege. Haikuwezekana kwake kutoka nje ya uwanja jinsi umati wa watu ulivyojazana kumlaki.. Walinzi wa kikoloni walimruhusu Dossa aingize gari yake hadi chini ya mlango wa ndege. Nyerere akashuka na kupokelewa na swahiba wake Dossa na akaingia ndani ya gari la Dossa.