Ukweli ni kwamba wewe na wenzako ndani ya ccm kuikubali ama kutoikubali Tume ya Katiba hakumsaidii mtu yeyote anayeujua ukweli wa dhiki, shida na kero zinazotokana na mapungufu yaliyomo kwenye katiba tuliyo nayo sasa. Wananchi wamechoka kuona wanaendelea kuishi maisha yaliyojaa ufukara na yasiyo na mwelelekeo wala dira wakati watu wachache wanafaidika. Kero za wananchi sasa hivi ni kama jua la asubuhi, kila kukicha linachomoza. Kuanzia Lindi na Mtwara, kwenda Kigoma, Arusha na Manyara, Zanzibar ndiyo basi tena, juzi juzi tumesikia mpaka Dodoma wananchi wameandamana dhidi ya fisadi CDA. Kila wanapopita viongozi wa nchi (watawala) wanakutana na mabango na hata wananchi wakizuiwa kuonyesha mabango basi wanakutana na wananchi wanaowaeleza kuhusu shida zao! Kuanzia migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, wananchi kunyang'anywa ardhi na wawekezaji, kukosa huduma muhimu kama afya, elimu, barabara, maji, umeme n.k. Suala la haki za binadamu zinavunjwa mchana kweupe na wanaozivunja wanalindwa mfano mzuri ni kauli ya Waziri Mkuu kusema 'wapigwe'. Suala la Muungano ambalo limeanza kuzungumziwa miaka mingi sana na walio madarakani wakajifanya wametia pamba masikioni hawasikii la mtu. Haya yote ni mapungufu yaliyomo kwenye katiba hii ya sasa!
Tufanyeje? Lazima tupate katiba mpya ambayo itakuwa dira ya kutuonyesha njia ya kutufikisha huko tuendako. Tuache kuongozana kama vipofu bali tunahitaji msaidizi angalau atakayekuwa macho yetu kwenye safari hii. Ndipo Tume hii iliposimamia. Kwa kuwa sasa inaonekana dhahiri ya kuwa zile kero za wananchi, hata kama si zote, zimeanza kumulikwa, na ukweli wa namna ya kuziondoa unaelekea kutafutwa, lazima kuna watu kama wewe na wenzako ndani ya chama na serikali ambao mnapata kizunguzungu na hofu kuu. Kwamba sasa ile 'mirija' aliyoikata Mwalimu ambayo mliweza kuiunga upya sasa inaelekea kuwa na uwezekano wa kukatwa upya. Huenda sasa katiba mpya ikipatikana basi si 'mirija' tu itakayokatwa, bali hata mizizi yote ya unyonyaji itang'olewa, ili matunda ya Tanzania huru yaweze kufaidiwa na kila mtanzania, na si yule tu ambaye ana baba, mjomba, shemeji, mume ama mke aliye kwenye sehemu yenye nafasi ya kuwanyonya wananchi.
Ukweli unawauma na unawatisha. Siku zenu zinahesabika. Waeleze wenzako ya kwamba tunakuja, na tunaitaka nchi yetu!!!