2 Samweli 6:12-22
Mbona Daudi alicheza kwa nguvu mbele ya Mwenye enzi MUNGU mpaka mavazi yakaanguka.
Ndugu
Donatila , soma andiko lifuatalo nimelitoa mahali.
Moja ya mambo ambayo wahamasishaji wa uchezaji uliokithiri makanisani kwa kisingizio cha kumsifu Mungu wanayatumia kutetea mwenendo huu ni kwa kile kinachodaiwa Daudi alicheza mbele za Bwana Mpaka nguo zikamuanguka. mara nyingi maneno haya yametumiwa kuhamasisha kuingiza michezo ya kidunia inayosukumwa na kuongozwa na tamaa za mwili ndani ya kanisa. Imefika wakati wakristo nao wameanzisha kitu kinaitwa Disko la Kilokole ambapo hukutana na kuweka mazingira kama ya klabu za kawaida za kidunia kisha huweka muziki unaodhaniwa kuwa ni wa kilokole na kucheza usiku kucha. Mambo haya pia yanaonekana kwa namna mikesha ya kusifu na kuabudu inavyoendeshwa gizani au kwenye mazingira ya giza na mwanga unaotumika kwenye club za kawaida za kidunia. Yote haya yanaanza na upotoshaji wa maandiko ikiwemo habari ya kucheza kwa Daudi alipohamisha sanduku la Agano kutoka nyumbani mwa Obedi Edomu kulileta mjini mwa Daudi.
UHAMISHAJI WA SANDUKU LA AGANO
Miongoni mwa mambo ambayo nimejifunza katika kutafiti kwangu juu ya habari ya Daudi alivyohamisha sanduku la agano na matendo yake pamoja na reaction ya Mikali ni kama ifuatavyo;
1. Ni vigumu kuelewa reaction ya Mikali kwa Daudi pasipo kuelewa Mikali alikuwa ni nani na Historia ya maisha yake kabla na baada ya kuolewa na Daudi
2. Huwezi kuielewa habari ya Daudi alivyokuwa akicheza kwa kuitazama katika 2 Samuel 16:14 Pekee, lazima kuiangalia habari hii pia katika 1Nyak15:25-29 ambako maelezo ya ziada ya kilichokuwa kikitendeka yametolewa
3. Huwezi kuielewa habari ya Daudi alivyoonekana kama huelewi desturi za wafalme na namna yao ya kuonekana mbele za watu wao
4. Ili kuelewa vema habari hii ni Muhimu kujaribu kuiangalia katika tafsiri mbali mbali za maandiko ikiwemo tafsiri za kiingereza.
MIKALI NI NANI?
Mikali alikuwa ni Binti ya Mfalme Sauli. Moja ya ahadi alizokuwa ametoa mfalme Sauli mwa mtu atakayemuua Goliathi ni pamoja na Kumtajirisha mtu huyo, kumwachia huru yeye na ukoo wake pamoja na kumwoza binti yake (1Sam 17:25). Ikawa Daudi alipomuua Goliathi, Merabu Binti Sauli aliyepaswa kuozwa kwa Daudi hakumpenda Daudi na alichagua kuozwa kwa mwanamume mwingine aitwaye Adrieli. Badala yake, Binti mwingine wa Mfalme Sauli aitwaye Mikali alimpenda Daudi na kukubali kuolewa naye (1Sam 17:20, 17:28). Daudi alikubali kumwoa na akatimiza sharti alilopewa na Mfalme la kumlipa mahari ya Govi 200 za wafilisti ikiwa ni mbinu ya sauli kutaka kumwangamiza Daudi kwa mkono wa wafilisti. lakini Daudi alifanikiwa akamletea mfalme hesabu kamili ya govi 200 kama mahari. Sauli akamwoza Mikali kwa Daudi. Utafiti mdogo nilioufanya unaonesha Mikali ndiye alikuwa mke wa kwanza wa Daudi. Ni muhimu kufahamu mambo makubwa mawili kuhusu mikali
1. Mikali alikuwa ni Binti mfalme, aliyelelewa katika nyumba ya kifalme, aliyejua desturi zote za wafalme na namna yao ya kuenenda, na junsi ambavyo mfalme alipaswa kuuchunga mwenendo wake mbele za watu wake wote.
2. Mikali alikuwa binti Sauli, ambaye alikuwa mfalme anayejali sana watu wanavyomuona kuliko Mungu anavyomuona. Udhaifu mkubwa sana aliokuwa nao Sauli ni kwamba alipenda zaidi kusikiliza watu kwa kiasi kwamba alipuuza hadi maagizo ya Mungu kwa kutaka kuwapendeza watu ili tu aonekane mzuri (Rejea 1Sam 15:24), vita yake yote ya kumuua Daudi hali akijua kabisa kwamba Roho ya Mungu iko pamoja na Daudi ilichochewa na watu (1Sam 22:6, 23:19-25, 24:1, 26:1-3)
3. Malezi ya Mikali katika nyumba ya mfalme ndiyo yaliyompa tabia kama ya Baba yake, kujali watu wanamuonaje kuliko Mungu anamuonaje.
4. Mikali kutokuwa na mtoto haikuwa kwa sababu alimdharau Daudi, ila ni kwa sababu Mungu alimkataa Sauli na nyumba yake yote asiwe mfalme juu ya watu wake Israel. Mikali kama mke wa kwanza wa Daudi angezaa maana yake ni kwamba Damu ya Sauli bado ingekuwa na nafasi katika Ufalme mpya wa Israel, kwa kuwa mwana wa mikali ndiye angekuwa aliyestahili kurithi kiti cha Daudi kama mzaliwa wa kwanza wa Mfalme. Hivyo Mungu alimfunga tumbo lake asizae ili uzao wa Sauli uliokataliwa usiendelee katika ufalme wa Israel.
KUCHEZA KWA DAUDI NA NGUO ALIZOVAA
Habari hii ukiiangalia katika 2Samuel 6:4 inachoeleza tu ni kwamba Daudi alicheza Mbele za Mungu kwa nguvu zake zote na alikuwa amevaa Naivera ya Kitani. kwa haraka inaweza kusababisha ukaona kama vile Daudi Hakuwa na Nguo nyingine zaidi ya Naivera ya Kutani na hivyo kufikiri kwamba nguo zilianguka akabakia uchi. Lakini ukiiangalia habari hii katika 1Nyakati 15:25-29 unapata maelezo zaidi ya habari hiyo kama ifuatavyo;
1. Siku ya uhamishaji wa sanduku Daudi, Walawi na Waimbaji wote walikuwa na yunifomu maalum waliyovalia. kwa sababu hiyo Daudi Hakuvaa vazi lake la utukufu, yaani vazi la kifalme kama ilivyo desturi ya wafalme wanapotokea mbele ya watu
2. Daudi alikuwa amevaa Joho la kitani Safi (Fine Linen) lenye rangi ya Buluu, vazi ambalo ndilo lilikuwa limevaliwa na Makuhani waliolichukua sanduku, Juu ya Joho hilo Daudi alivaa Naivera (Ephod) ya Kitani safi
3. Joho la Buluu na Naivera ya kitani yenye miraba ya buluu, zambarau, nyekundu na dhahabu yalikuwa ni mavazi matakatifu yaliyovaliwa na makuhani tu kwa mujibu wa sheria ya Musa kwa habari ya makuhani na mavazi yao
DESTURI ZA WAFALME
Wafalme wana desturi zao ambazo huongoza familia ya kifalme wakati wote na mfalme wakati wote alikuwa na wajibu wa kuhakikisha watoto wake hasa mrithi wake anafundishwa desturi za kifalme ili aweze kuenenda sawa na matarajio ya jamii. miongoni mwa desturi hivyo ni kama ifuatavyo;
1. Mfalme haruhusiwi kusimama mbele za watu wake bila vazi rasmi la kifalme linalomtambulisha. Vazi la kifalme lilikuwa ni ishara na sehemu ya utukufu na fahari ya mfalme inayomfanya atambulike popote anapokuwa
2. Mfalme alikuwa haruhusiwi kurukaruka na kucheza hovyo hovyo mbele za watu wake na vijakazi wake
3. kwa mfalme kusimama mbele za vijakazi bila vazi lake la kifalme ni sawa na kutembea uchi, ni kujivunjia heshima, ni kujilinganisha na kujiweka sawa na watu wa kawaida au watu wa chini kabisa wasio na hadhi yeyote.
Kwa Mikali, Binti Sauli, aliyekuwa akielewa desturi za wafalme, Kitendo cha Daudi kutoka nje na kuwa na watu bila vazi lake la kifalme ilikuwa ni kitendo cha kujidharaulisha, ukizingatia pia kwamba Daudi alikuwa akicheza na kurukaruka kama watu wengine kwa macho ya Mikali ilikuwa ni kujivunjia heshima yake kama mfalme mbele ya vijakazi wake na kujifanya kuwa kama mmoja wa watu wa chini kabisa wasio na hadhi yeyote, na kwa hilo alimdharau na kuamua kumkemea
Kitu ambacho mikali hakukielewa ni kwamba Daudi aliamua kuacha vazi lenye utukufu wa kifalme na kuvaa vazi lenye utukufu wa kiungu zaidi lililovaliwa na makuhani tu ili apate kukaa mbele za Bwana. Daudi alitambua kwamba Mbele ya Mfalme wa wafalme yeye ni kama mmoja wa watumwa tu na hakuhitaji utukufu wake wa kifalme... akavaa kama ambavyo watumishi wengine wa Mungu walivaa ikiwemo makuhani na waimbaji wote pamoja na kiongozi wa waimbaji... akacheza kama ambavyo watumishi wengine wa Mungu walicheza mbele za Bwana... Akafurahi kama ambavyo watumishi wengine wa Bwana walifurahi... LAKINI HAKUNA NGUO ILIYOMUANGUKA... WALA HAKUWA UCHI.
Source: The Greater Light of Glory.