Kyoma:
Nashukuru kwa michango yako mizuri. Nashauri uihariri itoke kama makala kwenye magezeti ya nyumbani ili watanzania wengi zaidi waisome. hata kama utatumia pen name. Mazenge kwa mfuga mbwa kumeanza kubadilika. Kutabadilika zaidi kama utakuwa wakala wa mabadiliko unayotaka kuyaona. Najua unanielewa nikizungumza hii lugha ya kiubungo ubungo.
JJ
Mnyika, heshima yako mkuu,
Sijamalizia huu mjadala wa Sokoine. Mzee Jokakuu alinishauri kuwa mapande yangu ni marefu mno, hivyo, nimetoa muda wa kuyameza na kuruhusu maswali pamoja na uchangiaji kutoka kwa wanabodi. Ni kweli, kuna umuhimu wa kuwa na idadi kubwa ya wanabodi ambao watajitolea kuchukua kurasa katika magazeti ya nyumbani na kuandika makala ili kuwashirikisha watanzania wengi katika kuchanga bongo. Huu utakuwa mkakati mmojawapo wa Jambo Forums katika harakati za kuwafikia walengwa, ambao ni watanzania wote.
Nilijaribu kuwasiliana na baadhi ya vyombo vya habari ili nipate fursa ya kuchangia makala kila wiki. Hata hivyo, juhudi zangu hazijafanikiwa mpaka sasa. Manyika, umekwisha ona michango yangu sehemu nyingine nikitumia jina langu, hivyo sioni tatizo kutumia jina langu katika makala zote. Ningefurahi, kuzihariri makala zangu zote nilizozituma Jambo Forums ili ziandikwe kwenye magazeti. Pia naweza kuchangia makala kila wiki bila malipo. Masharti yangu ni kuwa, makala zangu zote, pamoja na kuwa zitachapishwa magazetini, iwe ni haki yangu, kwa maana kuwa, hata siku za usoni nikitaka kuzikusanya na kuziweka katika mfumo wa kijarida au kitabu, isiwepo songombingo ya nani anamiliki hizo makala.
Pili, natambua kuwa magazeti yana wahariri, na wengine wangependa kuzichapisha makala kwa mtindo unaoshabihiana na misimamo ya vyombo vyao. Nisingependa kuona kuwa hoja zilizobeba msingi wa makala zinatolewa, au kuongezwa hoja nyingine kwa kisingizio cha uhariri. Ningependelea uhariri kwa maana ya kusaihisha lugha na uumbaji wa sentensi, au kuiandika upya makala kwa kutumia lugha wanayoipenda bila kubadilisha maana ya ujumbe wangu.
Bado natafuta, na nikifanikiwa kupata chombo cha maana, nitatekeleza wajibu huu. Kama unaweza kusadia upatikanaji wake, unakaribishwa kwa moyo mkunjufu.