Mzee Mkandara na Mzee Machumo, heshima zenu kwa mpigo
Mzee Machumo, sidhani kama naweza kunyamazishwa kwa mtindo huu usio na kichwa wala miguu. Ingawa sio jambo la busara kuwapuuza hawa watu, lakini ni vema kuwadhalau. Mzee Mkandara, acha utani! Sijuhi nisisitize vipi mpaka unielewe kuwa kutofautiana kihoja ndiko kunaniweka Jamii Forums. Usipoona mchango wangu, basi ujue kuna jambo la msingi. Hata hivyo, nitamalizia viporo vyangu vyote kama nilivyoahidi.
Labda kwa leo nikatishe mchango wangu katika hii mada ya Sokoine, ili nitoe masikitiko yangu kuhusu tathmini ya hali ya uchumi iliyotolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Daudi Balali, na kuwasilishwa kwenye kamati ya fedha na uchumi ya Bunge (Habari leo Mei 29, 2007). Tathmini ya Gavana imegusia jambo ambalo tumelijadili kwa ufasaha ndani ya mjadala huu wa Sokoine. Huu utakuwa ushahidi tosha kwa Mzee JokaKuu aliyechokonoa mjadala wa IMF na WB. Binafsi, nadhani Gavana Daudi amewapotosha wabunge kwa kutokuongea kiini cha sababu za kushuka kwa thamani ya shilingi na chanzo cha mfumuko wa bei.
Pia, siamini kuwa Gavana wetu ni mjinga kiasi cha kutokujua njia za kurekebisha tatizo la kushuka kwa thamani ya shilingi au kupunguza mfumuko wa bei. Naamini kuwa mapendekezo yake yanalenga katika upotoshaji na wala sio utatuzi wa tatizo lenyewe. Eti ili kuondoa mfumuko wa bei, anawashauri watanzania wathamini bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. Eti ili shilingi isishuke thamani, watanzania waache kusomesha watoto wao nje ya nchi, hivyo kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.
Gavana anawatoa kafara wananchi kwamba ndio wanasababisha mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi. Mbona hajawakumbusha watawala wetu kuthamini hospitali na madaktari wetu wanaozalishwa Muhimbili? Mbona hajawaambia viongozi waheshimiwa waache au wapunguze safari za nje zisizo na manufaa kwa nchi yetu? Au hizo hazipunguzi matumizi ya fedha za kigeni?
Lakini ni watanzania wangapi wanasomesha watoto wao nje ya nchi kwa kutumia fedha za kigeni? Ni kweli, kuna watoto wa kitanzania wanaosoma Kenya na Uganda. Hata hivyo, idadi yao ni ndogo sana kiasi kwamba haiwezi kulitikisa taifa kwa kushusha thamani ya shilingi. Pengine, wengi wao wanatumia fedha za madafu zinazobadilishwa mpakani kwa fedha ya Kenya na Uganda. Fedha ya Kenya na Uganda, haiwezi kutikisa fedha yetu kama zifanyazo Dola, Paundi au Euro. Hivi ni visingizio vyenye lengo la kulikimbia tatizo la kweli.
Gavana lazima atambue na amshukuru Mungu kuwa kuna watanzania wanaoishi katika nchi zinazotumia fedha yenye thamani kubwa duniani. Wengi kama sio karibu wote, hawasomeshwi na wazazi wao, bali wanajisomesha wenyewe kwa kuchakalika. Niliwahi kuandika mahala kuwa naheshimu sana watanzania walioshindwa darasa la saba na kidato cha nne, alafu wakaamua kutimua na kuchakarika katika nchi zinazoitwa tajiri duniani. Hawa kwangu mimi ni majemedari wa taifa letu. Wangekuwa pale nyumbani, ungekuwa ni msalaba mkubwa kwa wananchi. Wengi wao wangekuwa ni vibaka au mashine za kusambaza ukimwi.
Gavana lazima atambue kuwa idadi ya hawa majemedari ni kubwa na hawapati msaada wa fedha kutoka nyumbani bali wanachakarika kuzisaidia familia zao zilizoko nyumbani. Wanatuma dola au paundi ishirini, mia moja, miatano, mpaka elfu moja. Hizi fedha kutoka kwa kila mmoja wao, zikijumlishwa kwa ujumla wake kwa kipindi cha miaka michache, zinakuwa maelfu kama sio mamilioni ya dola au paundi.
Wakati viongozi wetu wanahujumu uchumi wa nchi yetu kwa kusaidia utoroshaji wa fedha za kigeni kwenda nje ya nchi, hawa majemedari wanasaidia uchumi wetu kwa kuingiza nchini fedha za kigeni. Vilevile, fedha wanazotuma zinawasaidia ndugu zao katika mapambano dhidi ya umasikini uliokithiri, zinasaidia kuanzisha miradi midogomidogo, kuwasomesha ndugu zao, kuajiri mafundi kwa ujenzi wa vibanda vyao vya kufikia, kununua bidhaa kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya familia zao n.k. Fedha inayotoka nje kwa mtindo huu, inazunguka ndani ya jamii ya watanzania. Mzunguko wa fedha ndani ya nchi, ni neema kwa taifa letu.
Mchango wa mtu mmoja katika uchumi wa namna hii hautoi taswira halisi ya umuhimu wa hawa majemedari katika kukuza uchumi wa nchi yetu. Hata hivyo, ujumla wa watanzania wote walioko nje wanaotoa mchango wa namna hii, unaweza kutoa picha nzuri kwa wale waliodhamilia kufanya tathmini ya kweli. Waswahili wanatukumbusha kuwa haba na haba ujaza kibaba.
Hoja za kiini cha kushuka kwa thamani ya shilingi na kinachosababisha mfumuko wa bei kwa nchi yetu tumezijadili kwa undani katika hii mada ya Sokoine. Kama Gavana wa Benki na wengi wa wabunge wetu wangekuwa washiriki wa mijadala ndani ya Jamii Forums, wasingethubutu kudanganyana kwa tathmini zisizokuwa na mbele wala nyuma. Wasiwasi wangu ni kuwa, hata Raisi wetu anapewa tathmini hizi za ubabaishaji.
Nimetoa kiambatanisho (pdf format) cha habari inayohusu tathmini ya Gavana wetu kama ilivyoandikwa na gazeti la habari leo. Nachukuwa fursa hii kutoa onyo kwa wote wanaotubeza kuwa Jamii Forums ni mahala pa gumzo au porojo. Kama wadau wanavyosema, hapa "tunakata issues". Tunatabiri mambo kabla hayajatokea. Utabiri wetu sio wa kutumia majini kama ule wa Profesa maji marefu au Yahaya. Utabiri wetu umelalia katika kuzichambua issues kama unavyochamabua karanga. Tuna-argue kwa logics, tuna evidenced evidence, na mifano tele.
Gavana wetu analipwa fedha kwa kazi yake. Amefanya tathmini ya hali ya uchumi ambayo ameipeleka kwenye kamati husika ya Bunge. Wabunge nao wanalipwa fedha (posho) kukaa vikao ili kuisoma hiyo tathmini. Lakini tathmini yenyewe ni ya upotoshaji, ubabaishaji, na uongo. Hailisaidii taifa letu.
Nimenukuu baadhi ya paragrafu kutoka katika mabandiko yangu ndani ya hii mada ya Sokoine zinazohusu vipengere vya tathmini ya Gavana kwa wabunge wetu. Hii inamaana kuwa Jamii Forums tulikwisha fanya tathmini yetu kwa njia ya mijadara na kujua kuwa fedha yetu itaendelea kushuka thamani. Pia, tulikwisha jua kuwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi yetu zitaendelea kukumbwa na dhoruba ya mfumuko wa bei. Tulitoa sababu na mifano hai ya kwa nini mambo hayo yatatokea. Habari nzuri kwa wadau wote ni kuwa mambo yanatokea, na yataendelea kutokea kama tulivyotabiri. Habari mbaya ni kuwa, taifa letu linaendelea kuegemea katika ukingo wa shimo la giza.
Yafuatayo ni baadhi ya maelezo yangu niliyoyatoa wakati namjibu JokaKuu kuhusu majangiri wa IMF na WB. Ukimaliza kuyasoma, yachungulie maelezo mafupi yaliyotolewa na Gavana wa Benki Kuu katika kiambatanisho (pdf format). Nikipata ripoti nzima ya Gavana nitaituma pia.
Binafsi, naona kuna tofauti kubwa kati ya Masharti na Sera. Masharti si Sera, na wala Sera si Masharti. IMF na WB hawana Sera, bali wana Masharti ya mikopo. Nchi yoyote ikikubali na kuyatekeleza hayo masharti, inakuwa kama vile umeonja Ganja, au Cocaine. Itaendelee kuwa tegemezi wa ile mikopo. Nchi ikiwa "addicted" na kitanzi cha Cocaine ya mikopo, ni vigumu kujinasua kutoka katika hicho kitanzi. Ndio maana IMF na WB wanakuja na Cocaine, kwa maana ya masharti yatakayotudumaza na kuendelea kutufanya mafukara wa mawazo, au tegemezi wa fedha. Tutaendelea kukopa kwa kuamini kuwa bila Ganja, yaani fedha za mikopo, hatuwezi kutatua matatizo yetu. IMF na WB wataendelea kutukopesha fedha mpaka siku ya kiama chetu. (labda tuazime busara za Venezuela)
Kumbuka kinachotutia umasikini sio riba ya hiyo mikopo bali ni masharti yanayoambatana na hiyo mikopo. Mfano, masharti tunayopewa ni kwamba, tukitaka kuongeza kiwango cha bidhaa zinazouzwa nje (export), na kupunguza kiwango cha bidhaa tunazonunua kutoka nje (import), yatupasa kuifanya fedha ya nje iwe na thamani kuzidi fedha ya ndani ya nchi yetu. Tunaaminishwa kuwa hii nadharia itakatisha tamaa manunuzi ya bidhaa kutoka nje. Hivyo, tunatakiwa kushusha thamani ya fedha ya nchi yetu, mfano kama tulivyofanya kushusha thamani ya shilingi ya Tanzania, na thamani ya dola, paundi au euro inapanda.
Hata hivyo, kwasababu tunakwenda kichwakichwa, hatukumbuki kuwa viwango vya uzalishaji katika jamii zetu ni vya chini sana. Tunategemea malighafi kutoka nje ili tuweze kuzalisha. Mfano wa bidhaa za lazima zitokazo nje ni Mafuta, Vitabu, Madawa, na Mbolea. Bidhaa zote hizi zinanunuliwa kwa fedha za kigeni. Thamani ya fedha ya nchi yetu inaposhuka na ile ya fedha za kigeni kupanda, gharama za uzalishaji zinakuwa juu na kusababisha mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. (Tathmini ya Gavana imekwepa sababu hii ambayo ni ya msingi. Mfumuko wa bei haupo kwasababu watanzania hawathamini bidhaa zinazozalishwa ndani, bali kwasababu hizo bidhaa ni za ghari. Sababu za bidhaa kuwa ghari nimezitaja)
Mfano mwingine wa hayo masharti ni kwamba, fedha wanazotukopesha, kamwe, haziwezi kutumika kuwasaidia wakulima au wafugaji wetu ili kupunguza makali ya uzalishaji (subsidize). Hata hivyo, Serikali zao, zinawasaidia wakulima wao ili kupunguza makali ya uzalishaji. Wanataka tufungue milango kwa maana kuwa bidhaa za wakulima wao ambazo ziko subsidized, zishindane na bidhaa za wakulima wetu ambazo haziko subsidized katika mfumo wa kitu kinachoitwa soko huria. Mwalimu aliwahi kusema Kirimanjaro hotel 1995, kuwa bingwa wa ngumi wa uzito wa juu hawezi kuingizwa ulingo mmoja na yule wa uzito wa kati. Alisema Burkina Faso and German haziwezi kuwekwa kwenye ulingo mmoja. (Tahmini ya Gavana inasema mfumuko wa bei wa Tanzania umefikia asilimia 7 wakati mfumuko wa bei wa nchi ambazo Tanzania inafanyanazo biashara ni kati ya asilimia 2.5 na 3. Hakuzitaja hizo nchi. Wakati viongozi wetu wanasalimu amri kwa hayo masharti, walitubeza kuwa uchumi wa kisasa unaendeshwa kwa nguvu ya soko. Sasa hizi ghiliba zinatoka wapi? Leo Gavana anatuletea takwimu za kushindwa kwetu zinazoonyesha kuwa German na Burkina Faso haziwezi kuwa katika ulingo mmoja)
Ingawa hizo nchi hazikutajwa, lakini baadhi ya nchi anazozisema Gavana kuwa tunafanyanazo biashara, mojawapo ni Marekani. Serikali yetu iliwekewa masharti na IMF na WB kuwa isiwape fedha (subsidize) wakulima wa Pamba. Hata hivyo, nchi ya Marekani inasaidia kupunguza makali ya uzalishaji ya wakulima wake wa Pamba kwa kuwapa fedha (subsidize). Wakulima wetu wanatumia majembe ya mkono na wale wa Kimarekani wanatumia Mashine za kisasa. Hata hivyo, Pamba inayotoka Marekani na ile ya Tanzania inauzwa kwa mashindano katika soko la pamoja bila kuangalia upendeleo katika njia za uzalishaji. Haya ndio masharti ya IMF na WB, yaliyojumlishwa katika mfumo wa uchumi wa Soko huria au utandawazi, ambapo njia zote zinazoweza kuinua viwango vya maisha ya wakulima na wazalishaji wa watu wa nchi yetu zinapigwa mweleka na haya majinamizi. (Tathmini ya Gavana inaeleza kuwa mauzo ya bidhaa zetu kwa nje ni kidogo ukilinganisha na mahitaji yetu, lakini haelezi kwa nini. Hii ndio sababu kubwa).
Matokeo ya hizi ghiliba za IMF na WB, bidhaa zinazoingia nchini kwetu kutoka nje zinauzwa kwa bei ndogo kwa sababu mbili, mosi, njia za uzalishaji katika nchi zenye nguvu za kiuchumi ni za kisasa, kwa maana ya kutumia mashine, wakati sisi tunatumia majembe ya mpini. Pili, Uzalishaji wa bidhaa zao unapata msaada wa fedha kutoka katika serikali zao kwa lengo la kupunguza makali ya uzalishaji. Kitu wanachotukataza sisi tusifanye kwa wakulima na wazalishaji wetu. (Tathmini ya gavana inawatoa kafara wananchi kwamba hawapendi bidhaa zinazozalishwa ndani. Huo ni uongo wa mchana. Tatizo haliko kwenye mapenzi, bali ni liko katika umasikini wa mawazo wa viongozi wetu kukubali masharti ya soko huria na utandawazi. Kamwe tatizo la mfumuko wa bei haliwezi kutatuliwa kimapenzi, bali ama kubadili sera au kuwang'oa wote wanaotubebesha huu msalaba. Ikibidi, yatupasa kuanza upya na mawazo mapya).
Nasisitiza kuwa sikubaliani na nia ya mataifa yenye nguvu za kiuchumi duniani, ingawa kwa nje wanaonekana kuazima sera za utu za kutufutia madeni. Haya mataifa hayawezi kumpinga shetani upande mmoja kwa kutufutia madeni, alafu wakahalalisha shetani upande wa mwingine kwa kukataa kuondoa mifumo ya uchumi duniani isiyo ya haki. Tumefutiwa madeni, lakini mifumo iliyo ndani ya nchi yetu na nje ya nchi yetu ambayo ilituingiza kwenye madeni, bado iko palepale. Tunachokifanya ni kuzunguka duara, na mwishowe tunarudi palepale.
Ndio maana baada ya kifo cha Sokoine na Nyerere, uchumi wa nchi yetu unaendeshwa na mataifa ya nje kwa kutumia mitambo ya ukopeshaji inayoendeshwa na mashirika ya fedha ya kimataifa IMF na WB, hivyo kuondoa dhana nzima ya matumaini na ndoto za kujitegemea.
Bahati mbaya wabunge wetu nao ndivyo hivyo kama tunavyojua. Hawawezi kumwambia Gavana wetu kuwa takwimu ulizozitoa ni za kweli, lakini sababu na suluhisho ni vya uongo. (fungua attachement)