Kama huna sababu mhimu sana inayokuzuia kukusanya habari za marehemu Sokoine na kuziweka kwenye kitabu, basi inafaa ufikirie kuifanya kazi hiyo.
Sababu ya wewe kuwa mdogo wakati huo sio ya msingi. Si lazima uandike peke yako, lakini unaweza kuwa chachu na mshiriki imara kati ya kundi la watu kama akina Mawado mnaoweza kuendesha na kuifanikisha shughuli mhimu kama hiyo.
Baadhi ya matatizo yetu mara nyingi ni haya ya kutegeana. Kumsubiri mtu mwingine afanye.
Kalamu, heshima yako mkuu,
Naona unanichokoza kwa kunifanya nianze kuboronga mjadala huu wa Sokoine kwa kupenyeza mada nyingine ya utamaduni wa kuandika na kujisomea. Nakiri kuwa mjadala wa Sokoine utatusaidia kutafakari mambo mengine ya msingi kwa taifa letu ambayo naona ni bora baadae tukayaanzishia mada yake. Nakubaliana na hoja yako kuwa wale wanaomjua au waliofanya kazi na Sokoine hawawajibiki peke yao kuandika vitabu vinavyohusu historia yake. Huu ni wajibu wa kila mtanzania. Hoja yako ni muhimu sana kwasababu tumekuwa na kasumba ya kuamini kuwa Tanzania hakuna wasomaji wa vitabu. Dhana hii imewafanya waandishi wa kusadikika kulala usingizi mzito wa fofofo kwa kisingizio kuwa, hata wangeandika vitabu, hakuna ambaye angevisoma.
Hivyo, kwa mawazo yao, kuandika vitabu ni kupoteza muda, kwani havitasomwa, na badala yake vitaishia mitaani kufungia Chapati, Maandazi, na Balagala. Hata hivyo, wadadisi wanaamini kuwa nchi yetu ina wasomaji tele wa vitabu, lakini waandishi ndio haba. Mjadala huu, wa kutafuta visingizio vya kuhalalisha uvivu wa kuandika na kusoma, naufananisha na ule wa kuku na yai ni kipi kilianza. Hii ina maana kwamba, waandishi wanasubiri upatikanaji wa wasomaji ili waweze kuandika vitabu, wakati, wasomaji wa kusadikika nao wanasema wanasubiri vitabu viandikwe ili waweze kuvisoma.
Wengine wanadai kuwa vitabu vichache vilivyopo mitaani, vina lugha ya kiwango cha juu ndio maana vinatumika kama nyenzo huko msalani. Dawa ni kama ulivyosema, tuache tabia ya kutegeana. Kazi ya mwandishi ni kuandika na wala sio kuhofia uhaba wa wasomaji. Sijuhi hii hofu huwa inatoka wapi, kwani sijawahi kuona mwandishi mzuri ambaye si msomaji mzuri. Yawezekana tatizo la nchi yetu sio ukosefu wa wasomaji au waandishi, bali ni tatizo la mawasiliano baina ya kundi dogo la wasomi ambao wanatarajiwa kuwa waandishi, lakini wamefunzwa kwa lugha tofauti isiyoeleweka vema miongoni mwa kundi kubwa la jamii ya Tanzania linalo mudu lugha isiyo ya wasomi.
Tatizo hili limejumuishwa katika mfumo wetu wa elimu wa Kiswa-Nglish. Naona Mzee Mwanasiasa amegonga msumari kwenye mfupa kwa kuanzisha mada ya mfumo wa elimu, na mimi nimekwisha weka mawazo yangu huko. Wale wachache waliofanikiwa kupata elimu ya juu na kuongea lugha ya kisomi, kwa maana ya Kiingereza, wanapata kigugumizi kuelezea utaalamu wao kwa njia ya maandishi ambayo yataeleweka miongoni mwa watu waliowengi lakini waliachwa katika kituo cha Saranda na treni letu la mfumo wa elimu. Hawa waheshimiwa wanamudu lugha yao inayodhalauliwa na wasomi, kwa maana kuwa wasomi wakitumia lugha ya waliowengi ambao hawajasoma, wote wataonekana kundi moja, yaani hawakusoma.
Mathalani, majuzi tu, wakati wa sakata la Rada, Prof. Mwesiga Baregu pamoja na mdau mwenzetu Mzee Mwanakijiji walitoa mitizamo yao kuhusu mtafaruku mzima wa ununuzi wa Rada. Matamko yote mawili yako humu ukumbini na kila mmoja wetu anaweza kuyapitia kwa lengo la kuwianisha. Nilibahatika kuongea na ndugu yangu kijijini Kitendagulo, Bukoba, ambaye naye ni miongoni mwa wale walioachwa Saranda na treni letu la elimu. Niliduwaa alipoanza kunisimulia sakata zima la Rada kwa kinaga ubaga. Alinishauri nitafute makala ya mtu anaitwa Mwanakijiji kwani yeye ndipo alipopata hizo busara alizonimegea. Nilimwambia nilikwisha isoma.
Hata hivyo, ujumbe nilioupata, ni kuwa lugha aliyotumia Mwanakijiji imewafikia wengi walio vijijini na wakaelewa na kuthubutu hata kuwasimulia akina Kyoma kama vile bibi yangu alivyokuwa ananisimulia hadithi za kale. Lugha aliyotumia Prof. Mwesiga Baregu ni ya wachache, kwa maana ya wale wanojiita wasomi. Hivyo basi, naamini wasomaji wapo, ila daraja linalounganisha wasomaji na waandishi, ndilo linahitaji kufanyiwa ukarabati, kwa maana ya kuwa lugha tunayotumia kuandika iwe ni lugha ya waliowengi.
Ni nadra kuona mtadao unaosomwa na watu wengi wenye viwango tofauti vya uelewa, na wanaotoka katika matabaka tofauti kama Jambo forums. Inawezekana pia ipo mitandao mingine yenye wadau wengi, lakini angalia tofauti ya lugha inayotumika kwa kulinganisha na mitandao yenye wadau wachache. Nakumbuka vitabu vya James C. Vilikuwa vinasomwa na watu wachache katika shule za Sekondari, lakini vitabu vya Msiba, Willy Gamba, vilisomwa Sekondari, shule za msingi, maofisini, vijijini, na mijini. Msiba alichofanya ni kunukuu yale ya James lakini kwa lugha ya watu wengi.
Niliwahi kusoma makablasha ya uzazi wa mpango yaliyoandikwa na waganga wetu mjini Dar-es Salaam. Nia ya hiyo NGO ilikuwa kusambaza ujumbe kwa wanawake mijini na vijijini. Kibaya zaidi makablasha yaliandikwa kwa kimombo. Kana kwamba haitoshi, lugha yenyewe ilikuwa ni medical terms, ambayo kwa mawazo yangu, ilibidi iwe translated into plain language, hata kama kingekuwa kimombo kilekile. Kuna dosari gani kwa mfano kutumia neno cant get pregnant badala ya neno infertility? au neno stopping periods, change of life badala ya neno Menopause au hata period badala ya Menses.
Ukija kwenye masuala ya kijamii au siasa, utabaki hoi bin taaban. Angalia kitabu cha Mwalimu, The Influence of Nyerere, au kile cha Who votes in Tanzania, and why cha Maliamkono. Utajiuliza hivi walengwa ni akina nani? Lakini soma kitabu cha Mwalimu cha Uongozi na Hatima Yetu, ndipo utatambua kuwa tatizo letu sio wasomaji, au waandishi bali ni ubovu wa daraja linalounganisha wasomaji na waandishi.
Nyumbani tuna utamaduni wa kupenga makamasi kwa mikono, alafu tukikutana na mtu, tunasalimiana kwa kutumia mikono. Mtu anashika uchafu wa aina mbalimbali, alafu akirudi nyumbani kwa sababu ya uhaba wa maji, familia nzima wanatumia sufuria moja kunawa mikono kabla ya kula. Vijidudu vya kuleta magonjwa vinasambazwa kwa kila mwanafamilia. Vijijini vyombo vinaanikwa chini bila kuwekwa kwenye chanja, hivyo Konokono wanapata vitanda vya chee kwa ajili ya kujamihiana. Mtu analazwa hospitali kwa sababu ya Malaria, lakini anakufa kwa ugonjwa mwingine alioupatia pale pale hospitali kutokana na wadudu wanaoishi kwenye mazingira ya uchafu pale hospitalini.
Serikali ingetenga fedha za madafu, tena kidogo sana, tukawapa waganga wetu waliohitimu pale Muhimbili, wakaenda KIUTA na kutuchapishia vikablasha vidogovidogo vyenye lugha inayoongewa na wengi, kwa lengo la kutoa elimu kwa Umma. Tungeokoa maisha ya watu wetu waliowengi wanaokufa kwa magonjwa ya kuhara, kipindupindu, na mengine yanayofanana na hayo. Badala yake, Serikali inakwenda kukopa mabilioni ya dola ili kununua madawa. Hata hivyo, wajanja wanazitumia hizo fedha kununua madawa hewa, huku wakiacha watu wanateketea.
Umuhimu wa kujenga utamaduni wa kuandika na kujisomea bila visingizio visivyokuwa na kichwa wala miguu vya kutegeana, unaweza kutuepusha na majanga yanayotukabili sasa hivi. Wakati mwingine hatuhitaji mabilioni ya fedha za mikopo kutatua matatizo yetu, we only need twelve lines of an exercise book. Hivi ndivyo Waganda walivyofanya kugeuza kasi ya kuenea kwa ugonjwa wa ukimwi. Uganda ilikuwa ni nchi ya kwanza duniani kufanya namba za maambukizo ya ukimwi duniani zianze kurudi nyuma. Yalikuwa ni mawasiliano ndani ya wanajamii kwa kutumia mistari kumi na miwili ya daftari la majaribio na sivinginevyo. Wazungu walipoona takwimu za Uganda zinaishangaza dunia, wakamwaga fedha kwa mabilioni. Nimesoma ripoti ya umoja wa mataifa ya mwaka jana, kuwa zile namba sasa zinayakimbiza mabilioni, kwa maana ya kwenda juu, na sio chini tena. Ukimwi umeanza kuenea kwa kasi kupiku idadi ya fedha zinazoingizwa.