KNKU,
Kyoma,
Sasa kama nilivyoeleza, hoja yako ni ndefu, pia umeitetea kwa data, hivyo ninahitaji kuvuta pumzi kabla sijaijibu.
Mzee JokaKuu,
Nitasubiri majibu yako kwa hamu, lakini wakati unapata pumzi, mimi niendelee na huu mjadala kwa kumalizia kiporo kilichobakia. Ukisha nijibu, ndipo tuanze mjadala wa nguvu kuhusu haya Majangiri. Kumbuka pia kuwa tofauti kubwa kati ya Sokoine, Nyerere na viongozi wetu wa sasa, ni kuwa Sokoine na Nyerere hawakuhujumu uchumi wa nchi yetu, bali viongozi wa sasa wanahujumu uchumi kwa kushirikiana na IMF na WB.
Saihisho, katika paragrafu ya nyuma, niliandika kuwa June 8, 2004 Serikali ya Tanzania ilipata mkopo wa dola za kimarekani milioni 43.8 kutoka katika Benki ya Dunia kwa sababu ya mpango wa dharura wa kupunguza makali ya mgao wa umeme uliokuwa ukilikabili taifa letu. Hata hivyo, kadili ya Ripoti iliyotolewa na (Transparency International), Serikali ya awamu ya tatu iliridhia na kukubali Tanesco isaini mkataba wa kuilipa IPTL dola za kimarekani 2.5. Isomeke kuwa Tanesco inailipa IPTL dola za kimarekani Milioni 2.5 kila mwezi, wawe wanazalisha umeme au hapana. Hivyo, tunakopa dola milioni 43.8 ambazo tunatakiwa kulipa pamoja na riba, lakini wakati huohuo, tunamlipa dola milioni 2.5 kwa kitu kilekile ambacho tunakopea fedha, hata kama hiyo kampuni haizalishi hicho kitu. Huku ndiko kuhujumu uchumi na kuwatia wananchi kilema cha umasikini. Hii ni biashara kichaa.
Anyway, tuendelee, Mei 9, 2006 Benki ya dunia WB ilitoa Press Release Washington kuwa iliikopesha Serikali ya Tanzania dola za Kimarekani Milioni 200 kwa ajili ya mpango wa kuondoa umasikini wa (Mkukuta). Serikali imetoa dola milioni 25 ambazo ni sawa na wastani wa Tshilingi bilioni 25 na kuziita fedha za Kikwete. Zilizobaki, yaani dola milioni 175 wanafanyia shangwe. Juzi tumesoma ripoti magazetini kuwa matumizi ya Ikulu yamekuwa mara mbili ya bajeti yake kwa kipindi ambacho hata mwaka haujaisha. Ripoti ya Mkaguzi mkuu wa Serikali ndio kwanza imetoka, hatujuhi mauzauza yaliyomo ndani. Nimesoma habari kuwa Raisi wetu alikuwa Zanzibar anafanya matanuzi hotelini. Kuna dosari gani na utamaduni aliouanzisha Nyerere na Sokoine wa Viongozi wetu wa kitaifa kufikia Ikulu ndogo?
Hata zile dola milioni 25 (maalufu kwa fedha za Kikwete), tunawakopesha watu kufanya miradi midogomidogo ya kuuza vitumbua, maandazi, maji ya miwa, na bamia sokoni (Refer; Waraka wa Mtei). Huwezi kurudisha dola milioni 200 + Fees + Riba kutoka katika miradi ya kuuza Sambusa, tena kwa fedha za madafu. Dola milioni 175, wanafanyia party, posho wakati wa vikao vya viongozi, na safari za nje zisizoisha. Kila unayemuuliza, anasema Tanzania watu wanafedha bwana! Lakini hatujiulizi fedha zinatoka wapi? Wananchi wanafurahia fedha za Kikwete, lakini hawajuhi kuwa watatakiwa kuzilipa hizi fedha mpaka jasho la kamshange liwatoke.
Kama umasikini ungekuwa unaondolewa kwa kukopa fedha, basi wananchi wetu wangekuwa matajiri. Mfano, Septemba 8, 2005 Benki ya dunia ilitoa Press Release Washington, kuwa imeikopesha Tanzania dola za Kimarekani Milioni 150 kwa ajili ya (Mkukuta). Hata kabla ya hapo, Julai 30, 2004 benki ya dunia iliikopesha serikali ya Tanzania dola za Kimarekani Milioni 60 (Poverty Reduction Support). Mei 29, 2003, Benki ya Dunia ilitoa Press release kuwa imeikopesha Tanzania dola za Kimarekani Milioni 100 (Poverty Reduction Supporty). Viongozi wetu wanakopa fedha kwa mgongo wa umasikini, alafu wanaishia kuzifuja.
Pamoja na mikopo yote hiyo, mbona umasikini miongoni mwa watu wetu unazidi kuongezeka? Mkukuta kwanza si Sera yetu, bali ni matokeo ya vikao vya mataifa makubwa, ambayo imechomekwa ndani ya mpango wa Umoja wa Mataifa kinyemela, kwa kusimamiwa na wajuba wa IMF na WB. Hivyo Sera zinazoongoza nchi yetu zinatoka nje. Ndio maana viongozi wetu wanatalii, kwasababu sera zinaagizwa nje kama bidhaa. Siku hizi sera imekuwa bidhaa, inaagizwa nje. Si biashara soko huria. Kumbuka Nyerere na Sokoine, walikuwa na mpango wa kuondoa umasikini ambao uliwashirikisha watanzania wote. Mfano, walitambua umuhimu wa kuwapa watu wote elimu kwa kumtokomeza adui ujinga. Hawakukaa Paris, Rome, au Washington, bali walikaa Musoma na kuja na Azimio la Musoma-Elimu.
Azimio la Musoma, linajulikana kwa matendo kuliko maneno, kwa maana kwamba, msisitizo uliwekwa katika Elimu kwa wote. Mkazo ulilenga kukuza maarifa ya ufundi na Sayansi. Pia, elimu na kazi vilitakiwa kwenda pamoja. Pamoja na matatizo yote tuliyoyapata miaka ya sabini, hata tukapigana vita na Nduli Amin, ambayo kwa kiasi kikubwa tuliigharamia sisi wenyewe, bado tuliweza kuwapeleka watoto wetu shule, tukawanunulia vitabu, Madaftari ya majaribio, vifaa vya Mahabara, Chaki za kufundishia, na chakula ili wapate lishe bora wasije wakashindwa mitihani kwa kusingizia njaa. Tuliwalipia nauli (unakumbuka TMO?). Nchi yetu ilikuwa mfano wa kuigwa, kwa maana kwamba tunaweza kupigana vita wakati huohuo tukawapeleka watoto wetu shule kwa kuwafanyia yote niliyoyaeleza. Wamarekani pamoja na utajiri wao, wanatoka makamasi. Hawawezi kuwafanyia raia wao kama tulivyofanya wakati wa vita.
IMF na WB walitushauri tupunguze bajeti za mipango mashuleni ambayo kwa mitizamo yao ilikuwa haitusaidii sisi watanzania. Walisema sisi ni masikini hivyo, hatuwezi kuwalipia shule watu watu. Viongozi wetu walisalimu amri. Wakaacha kuwalipia watu shule, wakapiga kwanja masomo ya ufundi, na kusitisha masomo ya michezo, kwa kuondoa mashindano ya michezo mashuleni. Eti wanadai Umiseta ni gharama. Ni gharama gani? Vijana walikuwa wanakula Ugali na Maharage wakati wa mashindano ya mashule. Walikuwa wanalala kwenye madarasa ya mashule ambapo mashindano hayo yalikuwa yanafanyikia. Kwani walitakiwa kupelekwa Brazil kwa mazoezi? Uliwahi kusikia wanafunzi wa umiseta wanataka kulala mahotelini?
Lakini IMF na WB, wanazunguka nyuma na kutukopesha fedha za kuwalipa makocha wa timu ya taifa, timu ya taifa ya vijana, na eti daktari wa viungo wa timu ya taifa. Eti hizo sio gharama. Mishara ya hawa waheshimiwa watatu kwa mwezi, ni tosha kuandaa mashindano ya umiseta kwa miaka kumi. Tunasahau kuwa mipango ya michezo mashuleni iliwanufaisha wote na sio kundi la wapenda soka tu. Miongoni mwa walionufaika ni wasichana, wavulana, vilema, wanariadha, wanakambumbu, mipira ya nyavu, tenesi, vikapu, karate, kuruka vihunzi, kwaya, michezo ya alaiki, na mengineyo. In fact, hii michezo ilikuwa inadumisha utamaduni wetu, na kujenga uzalendo miongoni mwa vijana. Sasa hivi tumewatenga wote hawa, kana kwamba sio sehemu ya jamii. Tumebweteka kushangilia ujinga wa kukopa fedha kwa ajili ya kuneemesha familia za wabraziri. Eti huku ndiko kupenda michezo.
Hata haya hatuna, tunasema Nyerere na Sokoine hawakupenda michezo. Tumesahau busara za wahenga kuwa Samaki mkunje angali mbichi. Kwasababu ya ulimbukeni, bado tunamstahi kocha kutoka Brazil, lakini kwasababu pia nchi yetu imejengwa na mashabiki wengi wa mpira kuliko walivyo wapenzi wa mpira, tukipata vipigo vingine huko mbeleni (kitu ambacho kitatokea), tutaanza kuchapana makonde wenyewe kwa wenyewe, na kusahau hii misifa kemkem tunayowamwagia viongozi wetu wanaotumia njia ya mkato kuiangamiza michezo nchini kwetu. Hata tukichapana makonde, tusisahau kuwa tutatakiwa kulipa hii mikopo.
Nyerere na Sokoine, walitumia fedha za misaada kujenga viwanda na kuanzisha mashirika ya Umma. Pamoja na kazi hiyo iliyowakabili, hawakusitisha huduma za jamii. Zilijengwa dispensari vijijini, na zilikuwa na madawa. Watoto walisoma wakiwa na siha na afya njema. Siku hizi pamoja na mabilioni tunayokopa, hatujengi viwanda, hatuanzishi mashirika ya Umma, hatuwezi kuwasomesha watoto wetu, na Hospitali zetu hazina madawa. Fedha hizo zinakwenda wapi? Mzee Mkandara juzi ameandika ujumbe kutoka Tanzania kuwa watu wanafedha kichizi. Angalia mabangaloo, maghorofa, twin tower, magari, na nguo wanazovaa viongozi na familia zao. Eti hayo ndio maendeleo. Toka lini maendeleo yakalenga vitu badala ya watu? Eti majengo, wakati ndani hakuna umeme na maji ya kunywa, au ya kutumia msalani. Huko ndiko fedha tunazokopa zinapoishia. Nasema zamani tulikopa fedha kujenga viwanda, lakini sasa hivi tunakopa fedha kubinafsisha hivyo viwanda.
December 15, 1999 benki ya dunia ilitoa press release kuwa imeikopesha serikali ya Tanzania dola za Kimarekani milioni 45.9 (Privatization and Private Sector Development Project). Yaani tulikopa fedha kubinafsi mashirika kama Shirika la ndege, ATC. Juzi huyu marehemu wetu ATC, amerudishwa mikononi mwa serikali. Hata hivyo, kitendo hicho hakisamei deni. Tutatakiwa kulipa fedha tulizokopa kwa ajili ya kulibinafshisha hilo shirika, hata kama ubinafshishaji wake umeshindikana. Yaani hasara juu ya hasara. Tuliijenga benki ya taifa ya biashara bila kutumia mikopo, lakini tumekopa fedha kuiuza. Mimi nadhani unapouza kitu, unapata faida, sasa kwa nini ukope fedha ili kuuza kitu, tena kwa bei ya kuokota? Huwezi kudharau mapambano aliyoyaongoza Sokoine ya vita dhidi ya wahujumu Uchumi. Uchumi wetu sasa hivi unahujumiwa na Magenge ya viongozi, wakishirikiana na makampuni makubwa ya kimataifa, chini ya usimamizi wa IMF na WB.
Mei 28, 2003 Benki ya dunia ilitoa press release kuwa imeikopesha Tanzania dola za Kimarekani Milioni 61.50 (Dar Es Salaam Water Supply and Sanitation Project). Shirika la Oxfam international, lilibaini kuwa mkopo tuliopewa, unafanana na ule waliopewa Ghana na hiyohiyo benki ya dunia kwa masharti ya kubinafsisha sekta ya maji (Refer: Oxfam international submission to world Bank review of conditionality, May 2005). Wote tunajua kilichotokea. Tulitapeliwa, lakini wananchi wanatakiwa kulipa hizi fedha, riba, pamoja na fees. (hii nitaielezea kwa undani zaidi wakati nachambua tofauti kati ya Lowasa na Sokoine).
Waghana waliingia mitaani kupinga ubinafsishaji wa sekta ya maji uliosimamiwa na benki ya dunia kwa kuanzisha taasisi za wananchi kama National cap of water in Ghana. (Refer: Privatization tidal wave IMF/World Bank water policies and the price paid by the poor by Sara Grusky). Sisi wabongo tumelala fofofo, huku viongozi wetu wanagawana fedha na makampuni ya kitapeli, alafu baadae, eti wanayafukuza hayo makampuni nchini ili kufuta ushahidi. Tunasema huko ndiko kuchapa kazi, na tunawapandisha vyeo. Kila siku tunasoma habari za jinsi watu wanavyotaabika na maji pale Dar-es Salaam, hasa akina mama na watoto.
Wanasema sikio la kufa halisikii dawa. February 13, 2007, Benki ya dunia imetoa press release kuwa imeikopesha serikali ya Tanzania dola za kimarekani milioni 200 kwa ajili ya (Water sector Support Project). (File attached). Tunarudi palepale. Sasa badala ya Net Group, sijuhi nani atapewa hizi dola milioni 200, alafu akafukuzwa kwa mikwara isiyokuwa na kichwa wala miguu.
Mashirika mengi ya kimataifa yamepiga kelele kuwa kwa kipindi kifupi kuanzia mwaka 2005 mpaka 2007 mwanzoni, deni la nchi yetu Tanzania, limekwisha fika pale tulipokuwa kabla ya kusamehewa madeni. Hata wabunge katika kikao kilichopita, wamelalamikia kasi ya ongezeko la deni la taifa. Mikopo karibu yote tunayoikopa, hakuna fedha zinazokwenda ku-generate hard cash. Tutazirudisha vipi hizo fedha? Kwa miaka miwili na robo, tumekopa kiasi cha fedha kinacholingana na fedha tulizokopa toka tupate Uhuru mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 2004.
Mimi nilitegemea mikopo yetu yote iwe katika sekta zinazo-generate hard cash. Mathalani, Agricultural Sector Development Projects. Lakini tunakopa kulipa posho na mauzauza mengine ya kuimalisha miundo. Mfano, May 15, 2006 benki ya dunia ilitukopesha dola za Kimarekani Milioni 15 (Finacial Sector Project). Hii ni fedha inaishia kwenye matumbo ya watu. Tutazirudisha vipi hizi fedha? Mfano mwingine, Juni 15, 2006 benki ya dunia ilitukopesha dola za Kimarekani Milioni 98 (Local Government Support Project), Januari 24, 2006 Benki ya dunia ilitukopesha dola za Kimarekani Milioni 184.02 (East Afrika Trade and Transport Facilitation Project). Kila mkopo hapo juu unajitegemea. Kadiri ya Benki ya dunia, makubaliano ya kila mkopo niliyoiongelea hapo juu ni pamoja na ada ya uazimaji (commitment fee) asilimia 0.35, gharama ya kuhudumia mkopo (service charge) asilimia 0.75 kwa kipindi chote cha miaka 40 ya ukomavu (maturity) na kipindi cha madahiro (grace period) cha miaka 10. Hivi ni viwango vya Jumuia ya Maendeleo ya Kimataifa (IDA).