Kwanza nitamke mwanzoni kabisa kuwa nami pia ni Wakili.Hivyo,sina upande. Kuhusu hawa wawili,wote ni Mawakili Wasomi mahiri kulingana na mashauri wanayoyawakilisha. Ndiyo maana wanaaminiwa. Hatahivyo, Mawakili hawapaswi kupambanishwa au kulinganishwa kwa namna hii. Kazi ya Wakili Mahakamani ni pamoja na kusaidia kutafsiri sheria ili Mahakama itende haki.
Kutokana na kwamba Mahakama ni chombo huru kimaamuzi, tafsiri ya Wakili Msomi yeyote yaweza kuchukuliwa na Mahakama kama ni sahihi. Hakuna upenyo wa Wakili Msomi kuilazimisha Mahakama kukubaliana naye. Na tafsiri iliyokataliwa katika kesi hii yaweza kukubaliwa katika kesi ile.
Kimsingi, umahiri wa Wakili Msomi hujitokeza katika namna ya uwasilishaji wake wa hoja akichagiza na nyaraka,vifungu vya sheria na kesi zilizokwishaamriwa. Pia, utambuzi wa haraka na kukwepa makosa ya kisheria yanayoweza kujitokeza na kupelekea kuharibiwa kwa ladha ya kesi nzima. Hata saini yaweza kuangamiza kesi nzima.
Itoshe kusema kuwa kiuzoefu na kiubobezi, Wakili Msomi Tundu Antipas Mughwai Lissu ni zaidi ya Wakili Msomi Albert Gabriel Msando. Lakini, wote wanabaki kuwa Mawakili Wasomi wazuri na wa kupigiwa mfano.