TUSIPOJITUMA TUTATUMWA: Ukweli Mchungu Kuhusu Mustakabali wa Afrika.
Kuna jambo la kutisha linaloendelea sasa hivi: Vijana wa Kitanzania na Waafrika kwa ujumla wanalegezwa taratibu na mambo yasiyo na tija. Kamari, uraibu wa michezo bila uzalishaji, na anasa za muda mfupi zimekuwa kipaumbele kuliko ujenzi wa uchumi wa mtu mmoja mmoja. Inasikitisha zaidi kuona hata baadhi ya wasomi, ambao tulitegemea watumie elimu yao kutatua changamoto za jamii, nao wamezama kwenye wimbi hili la upotezaji wa muda.
Wakati sisi tukiwa tumelala, kuna mkakati wa wazi unaoendelea barani Afrika. Kwa sasa, wengi wanafurahia ujio wa wafanyabiashara wa kichina wakiamini wanapata bidhaa kwa bei rahisi. Hata hivyo, tunasahau kuwa huu ni mtego wa muda mrefu; miaka michache ijayo, biashara na mnyororo mzima wa thamani utamilikiwa na wao.
•Hatari ya Kuwa Vibarua Katika Nchi Yako Tusipoamka sasa, hali itakuwa mbaya sana. Tutageuka kuwa watumishi na vibarua ndani ya nchi yetu wenyewe kwa sababu hatuna viwanda wala udhibiti wa soko letu. Tutabaki na jukumu la kuuza malighafi (raw materials) kwa bei ya kutupwa, kisha tutalazimika kununua bidhaa zilizokamilika kwa bei watakayopanga wao. Huu ndio utumwa wa kisasa wa kiuchumi.
•Usiilaumu Sera, Amka Mwenyewe
Jambo pekee litakalotutoa kwenye mtego huu ni mtu mmoja mmoja kuamka kwa hiari. Ingawa sera za kiuchumi sio rafiki kwa sasa, huu si muda wa kuendelea kuilaumu serikali pekee. Hata kukiwa na sera nzuri kiasi gani, serikali haitakufuata nyumbani kwako kukuletea fursa mkononi.
Inashangaza kuona mgeni anatoka kwao maelfu ya maili na kuona fursa hapa nchini kwetu, wakati sisi tulioko hapa miaka nenda rudi tunazichukulia fursa hizo kama mazoea. Hawa watu hawaji kwa kubahatisha; wameshafanya utafiti wa kina katika kila mkoa wa Tanzania na wanajua fursa zilizopo. Ni wakati wa sisi kuamka na kuchukua hatua.
HATMA YA UCHUMI WETU IKO MIKONONI MWETU, SIYO MIKONONI MWA WAWEKEZAJI.
TUSIPOJITUMA, TUTATUMWA.
Uchaguzi ni wako.