Mwanamume aliyefungwa jela miaka 17 amemaliza kifungo chake na amemkuta mkewe akiwa mwaminifu akimsubiri amalize adhabu yake waendeleze maisha.
“Nimefurahi sana kwa sababu mume wangu ameachiwa huru baada ya miaka 17 ya kifungo jela. Nimekuwa nikimsubiri kwa miaka yote. Nimevumilia sana, lakini sasa yuko hapa,” ni kauli ya Joyce Njenga aliyoitoa baada ya mumewe Joseph Njenga kumaliza kifungo jela.
Joyce amesema imani yake kwa Mungu ndio imemfanya awe mwaminifu kwa mumewe huyo katika kipindi chote cha miaka 17 aliyokuwa kifungoni.
Joseph Njenga alihukumiwa kifungo cha miaka 17 jela mwaka 2007 baada ya Mahakama kumkuta na hatia ya wizi wa kutumia nguvu na kukutwa na mali ya wizi.
Hata hivyo, Joseph aliendelea kudai kutokuwa na hatia akidai kilichomtokea hadi kufungwa jela ni bahati mbaya iliyosababishwa na marafiki zake.
Joseph alipotoka nje ya geti la gereza, alimkuta mkewe Joyce akimsubiri kumpokea kwa mikono miwili. Wanandoa hao walikumbatiana kwa muda mrefu kulikoambatana na furaha baada ya miaka mingi ya kutokuwa pamoja huku mkewe Joyce alikuwa pamoja na mtu wa Mungu ambaye aliwaombea walipokuwa wakirudia viapo vyao vya ndoa nje ya gereza.
Mwananchi