Julai 18 kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela, na pia ni siku ya kuzaliwa kwa mwanasiasa huyo mkongwe wa Afrika Kusini, aliyepigania kuondoa aina zote za ubaguzi wa rangi na kuleta usawa kwenye nchi yake.
Mwaka huu ni wa 101 tangu kuzaliwa kwa Mandela. Wengi tunafahamu historia yake na jinsi alivyojitoa kuikomboa nchi yake kutoka kwenye ubaguzi wa rangi. Alifungwa jela katika gereza la Robbin Island kwa miaka 27 kutokana na harakati zake za kupigania usawa na kuondoa ubaguzi wa rangi. Mei 10 mwaka 1994, Mandela aliapishwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, na alidumu madarakani kwa awamu moja tu, kama alivyosema awali, na nafasi yake kuchukuliwa na Thabo Mbeki Juni mwaka 1999.
Mandela alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobeli mwaka 1993, pamoja na rais wa zamani wa Afrika Kusini F.W. de Klerk, ambaye aliondoa zuio la chama cha ANC na kumuachia huru Nelson Mandela kutoka kifungoni. Kwa pamoja walishirikiana kuliondoa taifa hilo kutoka katika utawala wa kibaguzi na kuwa nchi ya kidemokrasia.
Hivi sasa dunia bado inakabiliwa na ubaguzi wa rangi, ukosefu wa usawa, na hata chuki dhidi ya raia wa kigeni bado zinaonekana nchini Afrika Kusini. Kutokana na mambo hayo, tunabaki kujiuliza, ni wapi tumekosea? Kwa nini mambo haya bado yanaendelea mpaka zama hizi?
Mwezi Mei nchini Marekani kuliibuka vurugu kubwa baada ya askari polisi mzungu kumkandamiza kwa goti Mmarekani mwenye asili ya Afrika George Floyd kwa zaidi ya dakika nane, na kusababisha kifo chake. Maandamano ya kudai haki kwa watu weusi nchini Marekani yamefanyika kuanzia wakati huo, na Nchi nyingine za Ulaya nazo kuunga mkono maandamano hayo.
Haya yote yanaonyesha kuwa bado jamii haijaamua kimsingi kuondokana na dhana ya ubaguzi wa rangi, bado kuna watu wanaojiona ni bora kuliko wengine, na wanastahili kupewa heshima kuliko wengine. Lakini binadamu wote ni sawa, haijalishi rangi ya ngozi yako.
Watunga sera wanapaswa kusimamia haki sawa kwa wote, bila kujali rangi, dini wala kabila. Elimu pia inapaswa kutolewa kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi ili kuweka msingi imara utakaowajenga katika siku za baadaye, kuwa haijalishi rangi ya ngozi, watu wote ni sawa na wana haki sawa katika sekta zote.
Wakati tunapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela, tunapaswa kusimamia kimsingi yale ambayo Madiba aliyasimamia na kupigania katika maisha yake, haki, usawa, kuondoa ubaguzi wa rangi, na kuishi kwa amani na watu wote.