Watanzania wengi hatuna ufahamu wa jinsi tulivyobarikiwa. Malalamiko mengi yanatokana na upungufu wa uelewa wa utajiri tulionao, siku zote tunajiona wadogo tu na wanapokuja raia wa mataifa yanayofundisha watoto wao maana ya kuhangaikia mkate wao wa kila siku kwa kutoka jasho huwa wanatudharau na kutumia fursa tulizonazo ambazo hatujui kama ni fursa tukiwa tumemezwa na akili za malalamiko.
Eneo zima la Tanzania lenye kutumiwa na uhfadhi wa wanyama lina kilometa za maraba 362,000 ni kubwa kuliko nchi kama tano za Ulaya ukiziunganisha pamoja, lakini hatuelewi maana ya utajiri huu tuliopewa bure na Mungu tunakuwa ni watu wa kupiga siasa nyepesi kila mara.
Hao wamasai wamepelekwa wakaishi Handeni mahali walipowekewa miundo mbinu ya kisasa na kujengewa na nyumba kabisa na malipo ya kuhamishwa kwa maana ya fidia wamelipwa pia. Na vyombo vyao vimesafirishwa na usafiri uliolipwa na serikali.
Lengo ni hizo kilomita za mraba 1500 zitunzwe ili maliasili isije kupotea kabisa. Kwani ikipotea watakaolaumu miaka kumi au ishirini ijayo wataikosoa serikali hawatamlaumu mwingine yoyote yule.
Mkuu, umeandika mengi ninayoweza kukubaliana nawe, hasa hayo uliyoeleza katika aya ya kwanza. Tanzania tumebahatika sana, lakini wenyewe, na hasa viongozi wetu hawatambui neema aliyotujaalia Mwenyezi Mungu.
Nisipokubaliana nawe ni katika hilo la matunzo, maendelezo na matumizi ya raslimali hii tuliyojaliwa., siyo katika swala hili la Ngorongoro pekee, lakini hata katika raslimali nyingi nyingine hapa nchini, mfano kama madini, na mazao ya misituni- karibu misitu yetu yote tumeiteketeza, lakini huwezi kuona popote tulipofaidika na miti iliyokuwa ikivunwa.
Swala la Loliondo wa kulaumiwa ni serikali (viongozi). Unaeleza hapa kwamba Masaai wamejengewa nyumba , na mengine kadhaa, na kwa upande wa pili kwa hiyo unawatupia lawama hao ambao wanasita kuhama kwa sababu mbalimbali, zikiwemo za kuchochewa (of course) na wanaofaidika na uwepo wao huko Loliondo.
Serikali ilipashwa kujiandaa vyema na kuwaanda wananchi kwa muda mrefu wa kutosha, kuwapa elimu. Hili haliwezi kufanywa kuwa kama jambo la dharura.
Unataka kumhamisha mwananchi aliyeishi miaka na miaka sehemu aliyoizoea. Kaa naye mweleze kinagaubaga yote na kumjengea uelewa wa hali iliyopo. Huwezi kwenda kumvamia, miezi sita unamwambia unbataka ahame, na wala humpi maelezo ya kutosha.
Serikali inapofanya mambo kuwa kama ya hiana, siri, na kuonekana kusema uongo, hali hiyo haimpi mwananchi utulivu na kuamini inachokisema serikali. Hili linakorezwa zaidi na historia ya kutokuwa wazi kwa serikali katika mambo iliyowahi kufanya katika maeneo ya aina hiyo.
Kwa hiyo, katika jambo hili, serikali ilipashwa kuwa na subira nyingi, na kutumia wakati wa kutosha kushirikiana na wananchi ikiwaeleza na kuwaelimisha kinachotakiwa kufanyika.
Kosa inalofanya serikali yetu, na hasa viongozi hawa, ni kujiona kuwa kwa kuwa wao ni serikali wanaweza kuamru na kutumia nguvu wakati wowote ili kutimiza malengo yao. 'Mentality' ya namna hii ni ya kikoloni.
Jambo la pili ninalotaka kukueleza ni hili. Je, serikali ilishawahi kujiridhisha kwamba hakuna njia bora inayoweza ku'manage' eneo hilo bila ya kuhamisha watu wote walioko huko, na bado sehemu hiyo ikaendelea kuwa katika hali yake nzuri? Hakuna njia kabisa za kufanya hivyo, kukawa na watu kiasi kinachoweza kubebwa na eneo hilo, na bado ustawi wa wanyama na uasili wa eneo ukaendelea kustawi?
Kwa nini serikali hupenda kurukia tu mambo yanayoonekana kuwa rahisi kufanyika huku ikiumiza wananchi wake, badala ya kuangalia uwezekano mbadala kama upo?
Kuna hili suala la mifugo kuwa mingi katika eneo hilo na kusababisha uharibifu. Hili kweli ni gumu kulidhibiti?
Kama kuna mifugo inayotoka nchi jirani inayoletwa eneo hilo kwa ajili ya malisho, hili nalo ni swala la kuwaumiza wananchi wako, badala ya kudhibiti hiyo mifugo isiingie kutoka huko kwingine?
Mwisho, nimalizie kwa hili linalosemwa na linalokera zaidi kama ni jambo la ukweli.
Kama wananchi wa nchi hii wanapewa usumbufu mkubwa, na hata upotevu wa maisha kwa sababu za kutaka kunufaisha wageni kwa kisingizio cha uwekezaji, kama hii ndiyo sababu inayoweka msukumo juu ya swala hili la wananchi kuhamishwa makazi yao, hapa nitasema uhuru wetu hauna maana yoyote. Na kama hivyo ndivyo wanavyoliona jambo hili viongozi wetu, basi wananchi wanayo haki ya kupigania uhuru wao unaopotea.