CCM yaikingia kifua serikali kwa ufisadi
Faraja Mgwabati, Tarime
Daily News; Sunday,September 21, 2008 @20:06
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema serikali yake inalishughulikia suala la ufisadi kwa vitendo tofauti na wapinzani ambao wamekuwa wakipiga kelele tu, lakini hawachukui hatua yoyote.
Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Pius Msekwa alisema hayo jana wakati akihutubia mamia ya wakazi wa Kata ya Nyanungu katika Kijiji cha Itiryo wakati wa uzinduzi wa kampeni za ubunge wa Jimbo la Tarime ambazo zilianza Jumapili iliyopita.
Msekwa alisema wapinzani wamekuwa wakikituhumu chama hicho kuwa kina ufisadi wakati wao, pia wana ufisadi ndani ya vyama vyao na akasema bora CCM inapambana na ufisadi kwa vitendo, lakini wapinzani hakuna wanalofanya.
'Kama alivyosema Rais bungeni, fedha za EPA… zinarudishwa ni sawa na jambazi akiiba ng'ombe, zinarudishwa kwanza ng'ombe ndipo jambazi anashughulikiwa," alisema Msekwa.
Katika mkutano ambao ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa chama hicho wakiwamo mawaziri, Msekwa alisema baadhi ya vyama vya upinzani kuna ufisadi mkubwa, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa, lakini badala yake wanabaki kulalamika ufisadi, ufisadi, ufisadi.
Msekwa ambaye naye aliungana na viongozi wengine wa CCM kwamba walifanya makosa mwaka 2005 kwa kumsimamisha mgombea asiyekubalika, alisema safari hii CCM itashinda kwa sababu chama hicho kina wanachama wengi kuliko wapinzani.
Alisema kama wanachama wote watakipigia chama hicho kura, wapinzani hawatakuwa na chao hivyo ushindi wao unategemea CCM. Alisema sasa wamemleta Ryoba Kangoye, mgombea ubunge ambaye amechujwa na chama hicho na anakubalika.
Aliahidi kutatua kero wanayopata wananchi wanaoishi karibu na mbuga ya Serengeti ambao wamekuwa wakikamatwa na kutozwa faini kubwa wanapoingiza mifugo eneo la hifadhi hiyo.
Naye Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba alianza kwa kusema wananchi wasifanye makosa ya kumlinganisha Katibu wa CCM na wa Chadema (Dk. Wilbroad Slaa) kwa sababu yeye ni katibu wa chama tawala, ni vitu viwili tofauti.
"Msinifananishe mimi na Dk. Slaa, mkifanya hivyo ni sawa na kufananisha mlima na kichuguu, sisi ndiyo tunaongoza serikali na hao wana nini," aliuliza na kuendelea, "Wala msimfananishe Mwenyekiti wa CCM (Rais Jakaya Kikwete) na wa Chadema (Freeman Mbowe)."
Alisema katika kumchagua mgombea, inabidi wananchi hao waangalie sifa nne ambazo ni chama anachotoka mgombea, elimu, asiyependa ukabila na awe mcha Mungu.
"Msimchague Mbunge ambaye hata Ikulu hakujui, Rais hamjui na hata kwenda Ikulu anaona aibu," alisema Makamba na kushangiliwa na viongozi wa chama hicho.
Viongozi waliohudhuria uzinduzi huo ni Mbunge wa Serengeti na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. James Wanyancha, Mkuu wa Mkoa wa Mara ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya CCM Mkoa, Issa Machibya, Mbunge wa Rorya, Profesa Sarungi, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Ofisa wa Idara ya Propaganda Tambwe Hiza na Mbunge wa Afrika Mashariki, Didas Masaburi.
Wengine ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Christopher Gachuma, John Komba na Profesa Samwel Wangwe ambaye ni kaka wa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, marehemu Chacha Wangwe.
Naye Mjumbe wa NEC, Stephen Wassira alizungumza kwa hisia kwamba wananchi hao wasifanye makosa ya kuchagua Chadema kwa sababu ni chama cha watu wawili, Edwin Mtei na Philemon Ndesamburo.
Aliwaambia wakazi hao kuwa mwaka 2005 Tarime walimpigia kura Mbowe wa Chadema kwa kura 30,000, lakini hawajapewa hata kiti kimoja cha ubunge maalumu, bali wabunge wote wa Viti Maalumu wamepewa kutoka Mkoa wa Kilimanjaro.
"Mnajua kilichotokea Kenya baada ya umoja kwisha? Wenzetu walipigana na hatutaki hapa umoja uishe," alisema Wassira na kuongeza kuwa anashangaa kuna watu wanajiita wapo upinzani kata hiyo.
"Msimchague mtu anayetangatanga na hana jipya, kazi yake kulalamika tu. Lazima mjue kwamba mtu mnayemchagua atawaletea maendeleo na huyo ni Kangoye."
Mgombea wa ubunge, Kangoye alielezea mambo mengi ambayo ameshafanya kama vile kuchangia vifaa vya hospitali vyenye thamani ya Sh milioni 600, elimu na akaahidi kusaidia kuleta umeme katika kata hiyo.
"Naomba tarehe 12 mwezi ujao, mnikopeshe kura zenu niwalipe maendeleo," alisema na kuongeza kuwa atashirikiana na serikali kutatua tatizo la wananchi wanaokaa karibu na mbuga endapo atachaguliwa.
Katika mkutano huo, pia mdogo wake, marehemu Wangwe, Keba Wangwe aliendelea kutoa shutuma za kwamba Chadema wanahusika na kifo cha kaka yake.
Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, alifariki dunia usiku wa Julai 28, mwaka huu kwa ajali ya gari katika eneo la Pandambili Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma; katika kifo ambacho hadi leo mazingira yake yanaendelea kukoroga vichwa vya watu wengi nchini.
Wanachama 50 wa vyama vya upinzani walirudisha kadi na 157 wapya walipewa kadi mpya za uanachama.