MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Rebu wilayani Tarime amekamatwa kwa tuhuma za kuuza shahada tano za kupigia kura ikiwemo ya kwake mwenyewe.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Polisi cha Oparesheni Maalumu, Naibu Kamishna wa Polisi, Bw. Venance Tossi katika mkutano na waandishi wa habari ilisema mwanafunzi huyo aliyejulikana kwa jina la Mahemba Daudi (1 alikamatwa saa nne asubuhi alipokwenda kuuza shahada hizo katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Tarime.
Bw. Tossi alisema baada ya vijana wa CCM kumkamata, walimfikisha kituo cha Polisi ambako alifunguliwa shitaka la jinai la kutaka kuuza shahada kinyume cha sheria.
"Tumemhoji mtuhumiwa kujua shahada zimemfikiaje, mpaka sasa nimeshatuma timu ya wapelelezi kufuatilia ili tujue nani walimtuma au kama zimeibwa," alisema Kamanda Tossi na kuongeza kwamba "Endapo itabainika, basi yeye pamoja na watakaohusishwa na tukio hilo watapelekwa haraka mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria."
Alipoulizwa kuwa kijana huyo ni mfuasi wa chama gani, Kamanda Tossi alijibu kuwa kazi ya Jeshi la Polisi si kujua hilo bali kwa vile shahada si mali ya chama chochote, ila cha muhimu ni kuwakamata watu wote wanaofanya biashara hiyo ya kuziuza kwani ni kosa la jinai.
"Anayeuza shahada na anayenunua wote wanafanya kosa la jinai, wakikamatwa watachukuliwa hatua za kisheria, hivyo tunatoa mwito kwa wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi endapo watamwona yeyote akiuza shahada," alisema Kamanda Tossi.
Kamanda Tossi alisema kabla ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilikuwa halijapata taarifa kutoka chama chochote kulalamikia biashara ya uuzaji shahada.
Naye George John anaripoti kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bw. Zitto Kabwe amedai kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara) Bw. Pius Msekwa na Katibu Mkuu wa CCM, Bw, Yusuf Makamba wanachofanya Tarime ni usanii kwani chama hicho hakina rekodi ya maendeleo wilayani humo kwa zaidi ya miaka 40 tangu nchi ipate uhuru.
Akihutubia mkutano wa kampeni jana kwenye uwanja wa Shule ya msingi Nyamisangura, Bw. Kabwe alisema miaka miwili ambayo CHADEMA imeongoza halmashauri ya wilaya hiyo imekuwa na mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupata hati safi.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kutolewa elimu bure ,kuimarishwa miundombinu ya barabara, zahati na mambo mengine.
" Makamba anapaswa ajibu fedha wanazolipiwa wanafunzi leo zimetoka wapi wakati huu wa CHADEMA na wakati wa CCM zilikuwa wapi?" Alihoji Bw. Kabwe.
Alieleza kusikitishwa na sera za CCM alizodai zimewafanywa Watanzania kukalia madini lakini yananufaisha watu wa nje kutokana na mikataba mibovu.
Alisema CHADEMA na wabunge wengine wa upinzani hawakubaliani na hali hiyo na wako tayari kufa ili Watanzania wanufaike na rasilimali zao.
"Wananchi wa Tarime kutupa moyo, chagueni upinzani ili uzidi kushughulikia EPA, Buzwagi na ufisadi mwingine," alisema Bw. Kabwe.
Katika mkutano huo, Bw. Kabwe alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Saidi Mwema kumkamata mara moja, Bw. Makamba kwa kauli yake kwamba ameandaa vijana kushughulikia CHADEMA .
Alisema kauli hiyo ni sawa na kuanzisha jeshi ndani ya nchi. Alidai CCM imekuwa ikiwatumia Polisi lakini inasikitisha kwamba askari hao wanalipwa mishahara midogo kuliko nchi yoyote duniani huku viongozi wakizidi kuneemeka na kupanuka pengo kati ya masikini na matajiri.
Alilitaka Jeshi la Polisi pia kumkamata Mchungaji Mtikila kwa kile alichodai kueneza uongo kuwa CHADEMA ilihusika na kifo cha Wangwe.
Pia Bw. Zitto alimtaka Spika wa Bunge kuunda tume kuchunguza kifo hicho kwani alidai pamoja na uchunguzi wa Polisi kuhusu kifo hicho, CCM imezidi kuing'ang'ania CHADEMA kuwa imehusika na kifo hicho na kutumia suala hilo kama 'kete'muhimu katika kampeni zake.