Kampeni Tarime: CCM wageukana
na Kulwa Karedia, Tarime
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
TIMU ya kampeni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyoko Tarime imeanza kusambaratika baada ya mmoja wa makada na viongozi wa chama hicho kuwageuka na kuwashambulia wenzake hadharani.
Hatua ya kada huyo ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana Mkoa wa Tanga, Mwita Mwikwabe Waitara, imesababisha kuibuka kwa hali ya kutoaminiana miongoni mwa viongozi wa chama hicho walioko hapa kwa ajili ya kampeni za ubunge na udiwani.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya G Five jana, Waitara alieleza kushangazwa kwake na propaganda za baadhi ya wanasiasa wanaotumia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Chacha Wangwe kama turufu ya kupata ushindi.
Huku akijua kwamba, kifo cha Wangwe kimekuwa kikitumia na chama chake na baadhi ya viongozi wa upinzani kama Christopher Mtikila, katika kujinadi, Waitara alisema wananchi wa Tarime wanahamu ya kusikia sera ambazo zitawasaidia kuwaletea maendeleo.
Mbali ya hilo, kada huyo wa CCM alieleza kushangazwa kwake pia na juhudi zinazofanywa na chama fulani cha siasa ambacho hakukitaja za kutumia vitisho na nguvu za Jeshi la Polisi na fedha kuwatisha raia kwa lengo la kumhalalishia mgombea wao ushindi.
Waitara ambaye alionekana moja kwa moja kukilenga chama chake, aliwataka viongozi wa kisiasa walioko Tarime kupiga kampeni na kuwapa uhuru wananchi wa jimbo hilo kuchagua mgombea wanayemtaka bila ya kutumia shinikizo lolote.
"Siridhishwi na mwenendo wa kampeni zinazoendelea katika uchaguzi huu mdogo hapa Tarime, ambako kunaonekana kuwepo na ushawishi wa chama fulani lazima kishinde kwa kutumia fedha na nguvu za Jeshi la Polisi, hatua ambayo itawaathiri zaidi wananchi wa Tarime na si mtu mwingine yeyote," alisema Waitara.
Akizungumza kwa kujiamini huku akisisitiza kwamba yuko tayari kukabiliana na matokeo yoyote kutoka ndani ya chama chake, Waitara alisema anaamini kuwa mshindi wa ubunge lazima awe yule mwenye uwezo wa kusimama na kuwatetea wana Tarime bila kujali anatoka CCM au Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Katika hatua nyingine, mwana CCM huyo alifikia hatua ya kuwaonya makada wenzake wa chama hicho waliopo Tarime kumnadi mgombea ubunge wa chama hicho, akisema wanapaswa kufanya hivyo wakijua kwamba wananchi wa jimbo hilo si kama wale wa Dar es Salaam na kwingineko, kwani wanao uelewa mkubwa wa mambo.
"Kuna timu ya wana CCM ambao wamekuwa hapa kwa ajili ya kuwanadi wagombea wao, napenda kuwatahadharisha kwamba siasa za Tarime si kama zile za Dar es Salaam...hapa watu wanauelewa mkubwa wa hali ya hapa Tarime," alisema Waitara.
Kada huyo wa CCM ambaye hivi karibuni alikuwa miongoni mwa viongozi wa UVCCM waliosimama kidete kumtetea Nape Nnauye ndani ya Baraza Kuu la jumuiya hiyo ya CCM, alieleza pia kusikitishwa kwake na hatua ya chama hicho kumuondoa katika eneo kubwa la kampeni na nafasi yake kuchukuliwa na Tambwe Hizza.
Kuhusu uamuzi huo, Waitara ambaye alieleza kushangazwa na uamuzi huo ambao alidai ulichukuliwa kwa maelezo kwamba, Tambwe, mmoja wa makada vipenzi wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Yussuf Makamba, alikuwa na uwezo mkubwa wa kujieleza kuliko yeye.
"Huu ni mkakati wa kutaka kunimaliza kisiasa, kwani haiwezekani nikashushwa kwenye gari na nafasi yangu kupewa Hizza, kwa madai kuwa eti anajua kujieleza vizuri. Sasa nimehamishiwa Kata ya Nyandoto kwa ajili ya kupiga kampeni," alisema Waitara kwa masikitiko.
Katika hatua ambayo inaonyesha dhahiri kukerwa na mwenendo wa ndani wa CCM, Waitara aliwahimiza wananchi wa Tarime kutoyumbishwa na kumchagua mbunge ambaye atakuwa mstari mbele kutetea mambo yote yaliyokuwa yanapiganiwa na marehemu Chacha Wangwe, kwani kufanya hivyo kutakuwa njia pekee ya kumuenzi.
"Napenda kuwaambia kwamba jambo kubwa ambalo sasa linawakabili wana Tarime ni kumchagua mbunge ambaye atasimama kidete kutetea na kulinda mambo yote aliyotetea marehemu Wangwe, yakiwamo ya wananchi kufukuzwa kwenye mgodi wa dhahabu wa Nyamongo, wananchi kukamatwa ovyo na kupigwa na wafanyabiashara katika mpaka wa Sirari," alisema Waitara.
Katika hatua nyingine, CHADEMA imemtaka Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Tarime (OCD), Constantine Massawe, kumhoji Mkuu wa Wilaya ya Tarime Stanley Kolimba kuhusu matamshi yake kwamba chama hicho kimeingiza vijana wa kundi la Mungiki kutoka nchini Kenya kwa nia ya kuvuruga uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 12.
Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa, amewaambia waandishi wa habari baada ya kikao cha viongozi wa chama hicho na Jeshi la Polisi mjini hapa kilichofanyika ofisini kwa OCD, kuwa Kolimba anawajibika kutoa ufafanuzi wenye maelezo ya kutosha juu ya matamshi hayo.
"Huyu mtu anaonekana amekurupuka katika matamshi yake ya juzi, ikiwa ni pamoja na kuamuru kukamatwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa chama chetu Zitto Kabwe, na hili la kuwepo kundi la Mungiki ambalo anaonekana kufahamu mahali lilipofikia na shughuli linayofanya mjini hapa," alisema Mtemelwa.
"Ameagiza pia kukamatwa kwa Zitto huku akitambua fika kuwa hana mamlaka hayo kwa mujibu wa sheria na kumuonya kuwa asiingilie uchaguzi," aliongeza Mtemelwa.
Kikao hicho kati ya OCD na viongozi wa CHADEMA, kiliwashirikisha pia mgombea ubunge wa CHADEMA, Charles Mwera na Mkurugenzi wa Oganaizesheni wa chama hicho, Benson Kigaila, ambapo undani wa kilichojadiliwa hakikuweza kujulikana mara moja