Date::10/15/2008
Chadema yamuunga mkono Msekwa kupinga matumizi makubwa Tarime
Na Kizitto Noya
Mwananchi
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemuunga mkono Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa kwamba hakukuwa na lazima fedha nyingi kutumika katika uchaguzi mdogo jimboni Tarime na kubabinisha kwamba chenyewe kimetumia Sh60 milioni.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilibrod Slaa aliliambia gazeti hili jana kuwa haikuwa lazima sio tu kwa vyama vya siasa kutumia fedha hizo, bali pia serikali kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuwapeleka askari 4,000, magari ya kifahari na magari ya maji ya kuwasha katika uchaguzi huo.
Licha ya chadema kuweka wazi kiasi cha fedha kilichotumia, CCM kimegoma kutaja fedha kilizotumia na kueleza kuwa hoja ya Makamu Mwenyekiti huyo, itajadiliwa katika vikao vya chama.
Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kauli hiyo iliyotolewa na Msekwa siku moja baada ya kumalizika uchaguzi huo ulioupa ushindi Chadema.
Makamba, alisema suala hilo halilihusu gazeti la Mwananchi bali wana-CCM ambao watalijadili kwenye vikao vyao.
"Hii hoja inatuhusu sisi wana-CCM na tutaijadili kwenye vikao vyetu, hivyo sina cha kueleza leo," alisema Makamba na kukata simu.
Hata hivyo, jana Msekwa aliendelea kusisitiza hoja yake ya kushangazwa na matumizi makubwa ya fedha yaliyojumuisha gharama za helikopta, magari ya kifahari na fedha yaliyofanywa na vyama vya siasa wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani wilayani Tarime.
Alisema anaamini matumizi ya kiasi hicho cha fedha ni makubwa kuliko ilivyostahili na kwamba kitendo hicho hakikujali thamani ya matumizi ya fedha.
"Kama mwanasayansi ya siasa kwa kusomea ninaona kuwa kwanza chaguzi ndogo ni gharama kubwa. Hivi tunatambua kweli thamani ya kutumia fedha nyingi kiasi hiki ili kupata jimbo lililoachwa wazi, wakati Bunge lina zaidi ya wabunge 320 ikizingatiwa chama kinachoshinda hakibadilishi uwiano wowote katika uimara wa chama," alisema.
CCM ilitumia helikopta mbili zilizokodishwa kutoka nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya kujiimarisha kwenye kampeni zake, baada ya Chadema kuendelza mtindo wake wa kutumia helikopta iliyouanza mwaka 2005 wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Mbali na matumizi ya helikopta vyama vya Chadema na CCM, vilitumia magari ya kifahari na kupeleka ujumbe mzito wa viongozi wa juu na wakereketwa huku CCM ikidaiwa kutumia magari ya kifahari zaidi ya 40.