Magabe Kibiti
JF-Expert Member
- Jan 20, 2008
- 292
- 2
*Familia: Wangwe alichomwa singe kisogoni (Gazeti la Majira)
*Yadai pia alivunjwa taya, mbavu tatu
Na George John,Tarime
WAKATI uchunguzi wa kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime marehemu Chacha Wangwe ukiendelea, familia ya mwanasiasa huyo imeibuka na kutamka hadharani kuwa ndugu yao aliuawa kwa kuvunjwa mbavu tatu, taya, kunyongwa na kuchomwa singe kisogoni.
Kaka wa marehemu Wangwe, Bw. Keba Wangwe, alitangaza hayo jana katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye kinyang'anyiro cha Ubunge Jimbo la Tarime, zilizohudhuriwa pia na ndugu mwingine wa familia hiyo, Profesa Samwel Wangwe.
Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Itiryo, Kata ya Nyanungu ambayo ni ngome kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na nyumbani kwa mgombea ubunge wa chama hicho,Bw. Charles Mwera
Bw. Keba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime kwa miaka 10 na kitaaluma ni mwanasheria, alisema familia baada ya kusita kukubali uchaguzi uliofanywa huko Dodoma, yeye na Prof. Wangwe walilazimika kufungua jeneza lililokuwa na mwili wa marehemu na kubaini mauji hayo ya kinyama.
Alidai kuwa familia hiyo itazidi kuilaumu CHADEMA kuwa huenda ilihusika na mauji hayo ya ndugu yao kutokana na kushindwa kufika kumzika na hata kutoa mkono wa pole kwa mbunge huyo ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho.
"CHADEMA wametufanya familia kuota upara, hadi sasa hawajaja hata kutoa mkono wa pole kwa familia pamoja na kwamba walichangisha rambirambi kutoka kwa watu mbalimbali hazijafika, leo tena wanatuomba kura?Si wakati wake,"alisema Bw. Keba huku akichanganya lugha na kuufanya umati huo kuinamisha vichwa.
Katika hatua nyingine, Makamu Mweyekiti wa CCM, Tanzania Bara Bw. Pius Msekwa alisema kuchotwa kwa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni wizi kama ulivyo wizi wa ng'ombe na watuhumiwa wote watashughulikiwa bila kukurupuka.
Alisema baada ya kubainika kuwepo wizi huo, serikali imechukua hatua za kuhakikisha fedha za EPA zinarejeshwa mara moja kabla ya kuwafikisha mahakamani wahusika hao bila kukurupuka.
"Suala la EPA ni wizi kama ulivyo wizi wa ng'ombe, Serikali ya CCM inapambana kwa vitendo kwa kurejesha kwanza fedha na baadaye hatua nyingine za kisheria zitafuta si kama wapinzani wanavyotaka tukamate watu kisha hela zetu zipotee,"alisema Bw. Msekwa.
Hata hivyo Bw. Msekwa, alikiri kuwa kushindwa kwa CCM katika chaguzi mbalimbali za ubunge na udiwani kunatokana na makosa yanayosabishwa na chama kuteua wagombea wasiokubalika kwa wapiga kura.
Alisema kutokana na CCM kugundua makosa hayo, imekuwa makini kuteua wagombea kwa kufuata maoni ya wananchi na ndivyo ilivyofanya kwa mgombea wao jimboni humo, Bw. Christopher Kangoye.
Aliishutumu CHADEMA na kudai kwamba ni chama cha kikabila kisicho na sera za kuongoza Watanzania na kimejaa ufisadi ambao unawanufaisha viongozi wa juu huku wanachama wake wakitumiwa kama daraja.
"Sisi tunapambana na ufisadi kwa dhati lakini wenzetu wanasema bila vitendo, ndani ya CHADEMA kuna ufisadi ambao hauelezeki ...tumewapa wilaya miaka miwili, wamefanya nini? Wamekula hela zote za miradi ya maendeleo tena mkiwapa hii iliyobaki, hamtapata kitu chagueni chama chenye sera nzuri,"alikipigia debe chama chake.
Alisema tangu mfumo wa vyama vingi ukubaliwe nchini CCM,imezidi kukubalika kwa wananchi kutokana na sifa, sera na umakini wake kushughulikia hoja na matatizo ya wananchi ukilinganisha na wapinzani ambao sasa wanakubalika kwa asilimia 12 tu nchi nzima.
Kwa upande wake akizungumza kabla ya kumkaribisha Bw. Msekwa, Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Yusuf Makamba alitamba kushinda kwa kura nyingi katika uchaguzi huo mdogo kwa madai kuwa CCM ndiyo yenye serikali inayoweza kushughulikia matatizo ya wananchi wa Tarime na si wapinzani.
"Msinilinganishe mimi na Slaa (Dkt. Wilbrod -Katibu Mkuu wa CHADEMA) kufanya hivyo ni sawa na kulinganisha kichuguu na Mlima Kilimanjaro. Eti kuna watu wanamfananisha Rais Jakaya Kikwete na Mbowe ( Freeman -Mwenyekiti wa CHADEMA), hapana ! Kufanya hivyo mnakosema, Kikwete ni Rais wa nchi Mbowe ni mtu wa kutangatanga hata hana Ikulu kama sisi,"alitamba Bw. Makamba.
Aliwataka wananchi hao kumchagua, Bw. Kangoye kwani ni mtu makini mwwenye upeo anayeweza kutatua shida zao kwa haraka tofauti na wapinzani na kwamba ameoa mke mzuri mwenye mvuto wa kuwa mke wa mbunge.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Bw. Stephen Wasira aliibeza CHADEMA kuwa ni chama cha kikabila na kinaendeshwa kama kampuni ya watu wachache.
Alisema uchaguzi wa Oktoba 12 ndicho kipimo cha watu wa Tarime kupata maendeleo na kuonya kuwawakishindwa kutumia nafasi hiyo, wataijutia kwa muda mrefu.
Naye Bw. Kangoye alisema mipango ya maendeleo katika jimbo hilo aliianza mapema kwa kununua vifaa vya hospitali vyenye thamani ya sh. mil. 600 kabla ya kufikiri kugombea ubunge na endapo wananchi watamchagua, watashirikiana vyema kufanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo jimboni humo.
"Nilianza zamani kuchukizwa na umasikini wa wananchi wa Tarime na kuleta miradi hapa, mimi siombi kuchaguliwa ili niwaletee maendeleo bali kazi hii nilishaianza mapema mniwezeshe tu niendeleze hayo yote ili Tarime ya neema iwezekane,"alisema Bw. Kangoye
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho na kupambwa na kundi la sanaa la TOT.
Wanaccm, chonde chonde chonde... msituletee mambo ya ukabila Tarime. Elezeni sera zenu na sio mambo ya kikabila, na ya kifo cha Wangwe ambayo mlikataa kuunda tume huru kuyachunguza.
Tanzania hii sijui tunaelekea wapi, yaani kama Msekwa, Makamba na Wassira wote wanaleta pumba hivi kwenye mkutano wa siasa, je nini kitegemewe toka kwa mgombea mwenyewe?
Ushauri kidogo tu kwenu wanaccm, watu tusio na vyama Tarime tunahitaji mtu ambaye atasimamia maslahi ya Tarime lakini wakati huo huo akiunganisha Tarime na makabila mengine Tanzania. Mnakoelekea huku sio kuzuri.
Chonde chonde Makamba... muogope MUNGU