Date::9/23/2008
Makamu mwenyekiti CCM aomba nguvu ya dola kudhibiti upinzani
Frederick Katulanda, Tarime
Mwananchi
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pius Mskekwa, amesema atawasiliana na Rais Jakaya Kikwete ili amwagize Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mstaafu Isaac Machibya, aruhusu nguvu zaidi ya dola itumike kuwadhibiti wanachama wa Chama cha Demokrasia (Chadema), aliyodai kuwa wanafanya fujo.
Akizungumza jana wakati wa kumnadi mgombe udiwani wa CCM Tarime mjini, Peter Zacharia, Msekwa, alisema atamweleza Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM amwamuru Kanali Machibya awaamuru polisi kutumia nguvu ya ziada katika kubilina na hali hiyo wakati huu wa kampeni za kuwania kiti cha ubunge wa Tarime.
"Wanatufanyia fujo, jana mfuasi wetu, Rubeni Marwa, alijeruhiwa kwa mawe na amekatika kidole na mwingine, Omari Nzungu, leo hii amemwagiwa pilipili machoni. Sasa hizi ni vurugu hatuwezi kuendela kuvumilia, nitamwambia Rais leo hii, hivyo yatakayo tokea shauri yenu," alisema Msekwa wakati akihutubia mkutano huo wa kampeni.
Hata hivyo wachunguzi wa masuala ya siasa ambao wamezungumza na gazeti hili baada ya kauli hiyo ya Msekwa, walionya kuwa kama Rais atapokea taarifa hiyo na kuamuru Jeshi la Polisi kutumia nguvu, hali ya usalama Tarime inaweza kuchafuka zaidi.
Walisema eneo hilo linaweza kugeuka uwanja wa vita kutokana na msimamo wa wananchi wa wilaya Tarime ambao wamekuwa wakiishi kwa mapigano ya koo kwa kwa muda mrefu.
Dalili za kuwapo kwa vurugu, zilianza kuonekana tangu kuanza kwa kampeni hizo na hasa baada ya kuwasili kwa viongozi wa ngazi za juu wa CCM ambao walipkewa kwa kuzomewa wakati wanaingia mjini Tarime.
Hata hivyo vurugu ziliibuka zaidi mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya wafuasi wa Chadema kukerwa na vitendo vya viongozi wa CCM kuwakikejeli chma chao kwa kukiita kuwa ni cha watu wawili.
Hata hivyo, juzi jioni wakati wa mkutano wa kampeni wa CCM ambapo kada mmoja wa chama hicho, alimwagiwa pilipili na kijana ambaye anayedaiwa kuwa mfuasi wa chadema, kulisababishwa na viongozi wa CCM kuanza kuishambulia chadema kwa maneno hivyo kuamsha hasira za wananchi hao ambao walianza kuzomea.
Vurugu zilizuka baada ya askari polisi kumshika kijana huyo na kutak kumpeleka kituoni ndipo wafuasi Chadema waliwasonga wakiwataka wamwachie mwenzo huku wakirusha mawe mpaka alipoachiwa.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Luteni Yusuph Makamba, aliwataka wananchi hao kutomchagua mgombea wa Chadema, kwa madai kuwa chama hicho hakina bajeti ya kuendeshea nchi, hivyo hawatapata maendeleo haraka.
Tangu kuanza kwa kampeni huizo kumekuwapo msuguano mkali kati ya wafuasi wa CCM na Chadema.