[Source Tanzania Daima]
Vijana 30 wa CHADEMA waswekwa ndani
na Mwandishi Wetu, Tarime
ZAIDI ya vijana 30 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wamekamatwa na polisi wilayani Tarime kwa kile kilichodaiwa kuwa ni operesheni kamata wazembe na wazururaji.
Operesheni hiyo ilianza jana asubuhi ambapo askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walimwagwa katika mitaa yote ya mji mdogo wa Tarime, hususan katika vijiwe maarufu vya wafuasi wa CHADEMA.
Vijana hao ambao hadi sasa bado wapo ndani, walifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Tarime ambapo Mkuu wa Kituo hicho (OCD), aliwataka viongozi wa chama hicho waliokuwa wakiwafutilia vijana hao, kuacha kumwingilia katika kazi zake.
Akizungumza katika mikutano mitatu ya kampeni katika vijiji vya Mrito, Karende na Kewanja, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema kitendo cha Serikali kumwaga polisi wengi katika jimbo hilo, kinawatisha wananchi.
Dk. Slaa ambaye alikuwa akimnadi mgombea wa CHADEMA, Charles Nyanguru, alilalamikia kauli za Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa na Katibu Mkuu, Yusuph Makamba, kwamba wametumwa na Rais Kikwete, kuangalia hali ya vurugu ili wamjulishe rais.
Kauli hiyo ni ya vitisho na kamwe hapaswi kutolewa na viongozi hao. Tunasema serikali ndiyo inayojenga mazingira ya hofu katika uchaguzi huu, wakati wananchi hawana mpango wa kuanzisha vurugu, alisema.
Dk. Slaa alisema katika mkutano huo kuwa ana ushahidi wa kikao cha Makamba cha Septemba 19 kwamba Jimbo la Tarime liwe mikononi mwa CCM kwani wana pesa na polisi, hivyo hawana sababu ya kushindwa.
Alisema kutokana na hali hiyo, ndiyo maana polisi mjini hapo, wamekuwa wakitekeleza maagizo ya CCM ya kuwakamata vijana wanaoonyesha alama ya vidole viwili, inayotumiwa na CHADEMA.
Dk. Slaa alisema serikali inataka kulifanya Jimbo la Tarime kama visiwa vya Zanzibar katika uchaguzi kwani matokeo wanayoyafanya, yanaonyesha ni jinsi gani wanataka kuleta vurugu.
Katika mkutano huo, Dk. Slaa, alimlaumu Rais Kikwete kuwa amekuwa bingwa wa kusuluhisha matatizo ya nchi jirani kama vile Kenya na Zimbabwe wakati Zanzibar ikibaki katika uhasama na sasa hali hiyo inataka kupandikizwa Tarime.
Aliwataka wananchi hao kuacha kumpigia kura mgombea wa CCM kwani hataweza kuwaletea maendeleo na badala yake wamchague mgombea wa CHADEMA ili kumalizia kazi iliyoachwa na marehemu Chacha Wangwe.
Naye mgombea CHADEMA, Nyanguru, aliwaahidi kuwatetea vijana, hasa katika operesheni za aina hiyo ambazo alisema ni za kinyanyasaji.
Uchaguzi katika jimbo hilo utafanyika Oktoba 12.