HALI imezidi kuwa mbaya kwenye kampeni za uchaguzi wa mbunge na diwani wilayani Tarime, baada ya Mwenyekiti wa chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila kupigwa mawe na kujeruhiwa baada ya kudai kwenye mkutano wa hadhara kuwa Chadema ilimuua mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Chacha Wangwe.
Mashambulizi hayo yamekuja siku moja baada ya Kamanda wa Operesheni ya Jeshi la Polisi, Venance Tossi, kutangaza kuwa atatumia nguvu kudhibiti wafuasi wa vyama vya upinzani -Chadema na CUF- kwa madai kuwa wana vurugu, na pia ikiwa ni siku moja baada ya kiongozi wa Chadema kuuawa kwa risasi katika mapigao yanayodaiwa kuwa ya ukoo.
Mtikila, ambaye ni maarufu kwa kutoa tuhuma kali bila ya woga, aliwahi kutoa tuhuma hizo kwa Chadema mapema mwezi huu, akihusisha kifo cha mbunge wa jimbo la Tarime na mgongano wa kikabila ndani ya chama hicho na kumuhusisha mfanyabiashara mmoja maarufu.
Lakini jana, hakupewa nafasi ya kuendelea na tuhuma hizo kwa Chadema na badala yake wale waliokuwa akiwahutubia waliamua kumshambulia kwa mawe na kumjeruhi kiasi cha kushonwa nyuzi saba.
Mchungaji huyo wa makanisa ya ufufuo alikuwa ameanza kueleza kifo cha Wangwe ambaye alifariki kwenye ajali ya gari ndogo wakati akisafiri kutoka Dodoma kuelekea Dar es salaam kuhudhuria mazishi ya mfanyabiashara Bhoke Munamka.
Wakati akiendela kuwahutubia wananchi na kuituhumu Chadema kuwa ndio iliyomuua mbunge huyo wa zamani wa jimbo hilo, ghafla alipondwa na jiwe baada ya kuwa amegeukia upande wa kulia na hivyo kujeruhiwa kichwani.
Shambulizi hilo lilisababisha mkutano huo wa hadhara kukatishwa wakati wasaidizi wake walipoanza harakati za kutafuta usafiri wa kumkimbizia hospitali ambako alitibiwa na kushonwa nyuzi saba.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11:00 jioni katika Uwanja wa Shule ya Msingi Sabasaba mjini Tarime.
Kifo cha Wangwe kilizua utata mkubwa kutokana na uhusiano wa muda mfupi baina yake na kijana anayedaiwa kuwa alikuwa akiendesha gari hilo, Deus Mallya, ambaye kwa sasa amefunguliwa mashtaka ya makosa yanayohusiana na usalama barabarani, mazingira ya ajali hiyo na mtu hasa aliyekuwa akiendesha gari hilo.
Awali ilisemekana kuwa Wangwe, ambaye alikuwa akijulikana pia kwa kuzua hoja tata bungeni, aliuawa kwa kupigwa risasi, lakini baada ya uchunguzi ilibainika kuwa kifo chake hakikutokana na kushambuliwa kwa risasi.
Lakini Mtikila amekuwa akishikia bango kifo hicho na wiki chache zilizopita aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwarushia shutuma viongozi wa Chadema na mfanyabiashara mmoja kuwa ndio waliosuka njama za kumuua Wangwe, ambaye alikuwa akiripotiwa kuwa na mgogoro na viongozi wenzake wa chama hicho kiasi cha kusimamishwa wadhifa wake wa makamu mwenyekiti.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutibiwa,Mtikila alisema analitupia lawama Jeshi la Polisi kutokana na shambulio hilo la mawe ambalo anadai kuwa alishataarifu mapema kuwa kulikuwa na njama ambazo alidai zilipangwa na Chadema.
Mchungaji huyo matata alisema mara baada ya kufika mjini Tarime alipata taarifa za kufanyika kwa mkutano wa kiongozi mmoja wa Chadema na kwamba katika mkutano huo, kiongozi huyo aliwaagiza wafuasi wake kuhakikisha wanamshambulia kwa mawe ili kumdhibiti yeye asisambaratishe chama hicho.
Nilitoa Taarifa mapema kwa msimamizi wa Uchaguzi na OCD, niliwaeleza juu ya agizo la mimi kupigwa mawe, lakini nashangaa polisi hawakuweza kuleta ulinzi mkali kwangu licha ya kutoa taarifa hiyo, alieleza mchungaji huyo.
Alisema kitendo cha kupigwa mawe si cha kiungwana na kwamba kimemsikitisha kwa kuwa anaamini kuwa siasa ni majibizano na hoja na wala si vurugu.
Hata hivyo, mchungaji mtikila alisema kuwa hatasitisha kampeni zake na kwamba leo ataendelea na kampeni za chama chake kumnadi mgombea wake mchungaji, Denison John Manyika.
Kabla ya mkutano huo, Mtikila alifanya mkutano katika kijiji cha Nyamwaga na Sirari ambako alikuwa akisisitiza na kueleza kuwa marehemu Wangwe ameuawa.