SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Democratic(DP) Mch. Christopher Mtikila kushambuliwa kwa mawe mkutanoni Tarime, ameibuka na kusema leo atalipiza kisasi kwa unyama waliomfanyia wabaya wake.
"Nitalipiza kisasi na ninajua watashindwa. Siwezi kuchukua mawe na kujeruhi watu lakini kisasi changu ni kuzidi kufunua mipango mingine ya siri ya mauaji ya wapigaji wazalendo wa nchi hii," amesema.
Ameapa kwamba pamoja na kujeruhiwa, leo ataendelea na mkutano wake na hata kama Polisi isipompa ulinzi wananchi tayari wanaomuunga mkono wamejitolea kumlinda vya kutosha.
Akizungumza na Dar Leo kwa njia ya simu kutoka Tarime leo asubuhi, Mtikila amesema tukio la kupigwa kwake ni la kupangwa siku nyingi na alishajua hilo litatokea kwa kuwa alikwishapewa taarifa na wananchi wema.
"Watu waliosuka mpango wa mimi nishambuliwe katika mkutano nawafahamu na tayari nimeshatoa taarifa Polisi na nimezungumza na Mkuregenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) na mchana huu wapinzani wote tutakutana naye kujadili hali ya kampeni inavyokwenda,"anasema Mtikila.
Alisema kushambuliwa kwake haina maana yale aliyokuwa amekusudia kuwaambia wananchi wa Tarime katika mikutano yake ya hadhara itakuwa mwisho bali sasa anajipanga zaidi ili aweze kuwafikia wananchi wote kuwaeleza mwenendo mzima wa mambo ya siasa yanayofanywa na vyama vingine vya siasa.
"Kwa bahati mbaya Polisi wa Tarime hawataki kunipa ulinzi lakini nitaendelea kufanya kazi yangu kama kawaida, wananchi wamejitolea kunipa ulinzi na wengine wamejitolea kunipa Landcruiser ili niwafikie wananchi wengi zaidi kueleza yale ninayofahamu mchungaji wao,"amesema Mtikila.
Amesema kushambuliwa kwake kumetokea baada ya kuzungumzia ukweli anaoufahamu kuhusu kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime marehemu Chacha Wangwe (CHADEMA)
"Wasijidangenye kwamba wamenifunga mdomo nitakachofanya sasa ni kuchapisha nakala nyingi zaidi zinazozungumzia kifo hicho na kuzisambaza kwa wananchi wengi zaidi," amesema na kusisitiza:
"Nimekuja kuwaeleza wananchi maovu yanayofanywa na wanasiasa kwa wananchi wa Tarime na nitalipa kisasi cha kushambuliwa kwangu kwa hoja kwa kueleza wananchi ukweli."
Alipoulizwa kama wakati anashambuliwa Polisi walikuwepo eneo la tukio, Mtkila amesema kwa bahati mbaya amekuwa hapewi ushirikiano na polisi katika suala la kumpatia ulinzi lakini pamoja na hali hiyo wananchi wameamua kumlinda ili aweze kufanya mikutano yake vizuri.
Anaongeza kuwa anashindwa kuelewa kitu gani ambacho wapinzani wenzake wanataka kutoka kwake kwani kila chama kinafanya kampeni zake bila kupangiwa na chama kingine ndio maana wapo wanazungumzia ufisadi na yeye ameamua kuzungumzia yale anayoyajua yeye.
Mwandishi Wetu kutoka Tarime anaripoti kuwa Mkuu wa Kitengo cha Operesheni Maalum Venance Tossi ameagiza kufikishwa mahakamani watu wanne wanaodaiwa jana kumpiga mawe Mtikila.
Amesema leo asubuhi kuwa tataribu zilikuwa zikifanywa maafisa wa polisi kuwafikisha mahakamani watu hao ambo ni Mussa Peter, Mwita Chacha, Hafidh Stanslaus na Mwita Kiongo wakazi wa Tarime mjini.
Kwa mujibu wa Tossi, watu hao ambao ni wafuasi wa vyama vya upinzani walikula njama na kumpiga jiwe Mtikila wakati akihutubia mkutano wa Kampeni katika Viwanja vya Sabasaba mjini Tarime.
Mtikila alipigwa jiwe kisogoni kutokana na kauli yake kwamba Rais Jakaya Kikwete alimkumbatia mmuaji Ditopile na kwamba ana ushahidi kwamba Chacha Wangwe aliuawa kutokana na mpango uliosukwa na Chadema.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa jana jioni walimtaka Mtikila kuondoka mara moja kabla hajadhurika kwani kutumia kifo cha Wangwe kunaweza kugharimu maisha yake.
Hata hivyo ilidaiwa na baadhi ya viongozi wa vyama upinzani kwamba anatumiwa na Chama Cha Mapinduzi CCM na kwamba siasa hizo zitaifanya Tarime iwe kama Kenya na ishindwe kukalika, endapo vyama vitatumia kifo cha Wangwe badala ya kutumia sera.
Source;Dar leo.