Helikopta ya Mbowe yabomoa CCM Tarime
2008-10-09 12:31:04
Na Mashaka Mgeta, Tarime
Joto la kampeni za kusaka kiti cha ubunge jimbo la Tarime likiwa limepanda kuelekea upigaji kura Jumapili ijayo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepata pigo baada ya kada wake, Mwita Mwikwabe Waitara, kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Waitara ambaye alikuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Tanga, kisha akajitosa kwenye kinyang\'anyiro cha uchaguzi huo mdogo akitafuta tikiti ya CCM kuteuliwa kuwa mgombea na kuambulia nafasi ya tatu, alianza kampeni dhidi ya CCM jana na kuonya kwamba chama hicho kinakaribia mwisho kwa kuwa kinakimbiwa na vijana.
Kada huyo aliyegoma uhamisho wa kwenda kuwa Katibu Muyeka wa Mwenyekiti wa UVCCM, alianza kuonyesha dalili za kuichoka CCM wiki iliyopita alipofanya mkutano na waandishi wa habari na kudai kwamba kampeni za chama hicho Tarime zilikuwa zimekosa mwelekeo, na kuwataka wanachi kumchagua mbunge yeyote hata kama ni wa Chadema.
Waitara awali alikuwa akimdadi mgombea wa CCM Tarime, Christopher Kangoye, lakini alilalalamika kuenguliwa rasmi na nafasi yake kuchukuliwa na watu aliosema wametoka makao makuu Dar es Salaam, lakini wasiojua siasa za Tarime.
Waliotoka makao makuu ni pamoja na Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Propaganda, Tambwe Hiza.
Waitara jana alisema amefikia hatua ya kujiengua CCM kwenye mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea ubunge wa Chadema katika Jimbo la Tarime, Charles Mwera, uliofanyika mjini Sirari, wilayani hapa.
Katika mkutano huo, Waitara alikabidhi kadi yake ya UVCCM namba 572182 na kadi ya CCM namba AL 1216241 kwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe.
Akitangaza uamuzi wake huo, Waitara alisema amejiondoa CCM kutokana na kushindwa kuvumilia vitendo vya dhuluma na unyanyasaji wanavyofanyiwa wakazi wa Tarime anakotoka yeye.
``Wananchi Tarime wanapigwa sana na polisi, wananyanyaswa kutokana na shinikizo la CCM. Nimeshindwa kuvumilia kuwa ndani ya chama kinachonyanyasa baba zangu, mama zangu, dada zangu na kaka zangu, hivyo, nimeamua kutoka,`` alisema Waitara.
Aliongeza kuwa kujiondoa kwake CCM ni sehemu ya falsafa ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyewahi kusema kwamba: ``CCM si baba yangu wala mama yangu.``
Hata hivyo, Waitara aliionya CCM kuhusu kuchukia harakati za vijana wanaotaka kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho, akisema kwamba hali hiyo inasababisha vijana wengi wakichukie chama hicho.
``Ukiona chama kinachochukia vijana kinawapenda na kuwakumbatia wazee peke yao, chama hicho kinaenda kufa. Hivyo, CCM nayo inakwenda kufa,`` alisema Waitara.
Alisema yeye ni miongoni mwa watu walionufaika na fedha zilizotolewa na CCM katika kampeni zinazoendelea Tarime, lakini yuko tayari kufa kuwatetea wananchi maskini walio wengi jimboni humo.
``Sisi watu wa Tarime ni wanaharakati, hatuogopi kutetea haki zetu, nipo tayari kufia Tarime nikimnadi mgombea wa Chadema, Charles Mwera,`` alisema Waitara.
Kampeni za jana za Chadema, zilifanywa na helikopta yenye namba 5Y-HSN iliyowasili mchana na kutua kwenye Uwanja wa Sabasaba, mjini Tarime.
Wakati helikopta hiyo ikitua, watu waliokuwa wakisikiliza mkutano wa kampeni za mgombea udiwani katika Kata ya Tarime Mjini kwa tiketi ya CCM, Peter Zakaria, kwenye uwanja wa Menonite, waliondoka katika mkutano huo na kuikimbilia helikopta hiyo.
Helkopta hiyo ilikuwa imewachukua Mbowe, Mwera, Waitara na Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, ambao walifanya mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Mogabiri, kabla ya kufanya mkutano mjini Sirari, mpakani na Kenya.
Akihutubia mkutano huo, Mbowe aliwataka wananchi wa Tarime wasimame imara kutetea haki yao kwenye uchaguzi kwani kazi ya kuondoa watu kwenye utawala ni ya hatari kwa wanaharakati wanaoshiriki.
NEC yaonya polisi wasio na namba Tarime
Nayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeonya kuhusu kuwepo askari polisi wanaoshiriki kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime, bila kuwa na namba za jeshi hilo kwenye sare zao.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lewis Makame, alisema hayo jana, wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari mjini hapa.
Jaji Makame, Mkurugenzi wa NEC, Rajab Kiravu, na maofisa wengine wa Tume hiyo, waliwasili jana mjini hapa, kushuhudia mwenendo wa kampeni na uchaguzi wa udiwani na ubunge jimboni humo.
Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko kutoka vyama vya upinzani, hususan Chadema, wakilalamikia kuwepo askari polisi wasiokuwa na namba kwenye sare zao.
Jaji Makame alisema kwa mujibu wa sheria zilizopo, askari polisi hapaswi kutekeleza majukumu yake, bila kuwa na namba za kijeshi.
``Nitashangaa sana kama kuna askari mwajiriwa wa polisi aliyevaa sare hana namba,`` alisema na kumwagiza Msimamizi wa uchaguzi huo, Trasias Kagenzi, kufuatilia na kupata ufumbuzi wa kadhia hiyo.
Kwa mujibu wa sheria namba 1 ya mwaka 1985, polisi ni miongoni mwa wadau wanaosimamia uchaguzi nchini.
Jaji Makame alisema askari polisi anapaswa kuwa nje ya chumba cha kupigia kura kwa ajili ya ulinzi na kusimama nyuma ya mtu wa mwisho baada ya muda wa kupiga kura kufikia ukomo.
Mtikila amvulia kofia Mbowe Naye Mwenyekiti wa DP, Christopher Mtikila, amesema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anaheshimika kama `Mungu-mtu` kwa wakazi wa wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Mtikila alisema hayo jana alipokuwa akizungumzia mapokezi makubwa aliyoyapa Mbowe, alipowasili mjini hapa kushiriki kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani, utakaofanyika Oktoba 12, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mtikila alisema inashangaza kuona, licha ya wakazi wa Tarime wakiwemo wafuasi wa Chadema kupigwa na vyombo vya dola, walipokuwa katika harakati za kumpokea Mbowe, bado walijitokeza kwa wingi kumlaki mwanasiasa huyo.
Mtikila amekuwa akimtuhumu Mbowe na watu wengine, kuwa walihusika katika mipango ya kumuua aliyekuwa Mbunge wa Tarime (Chadema), marehemu Chacha Zakayo Wangwe.
Kauli hiyo, ilisababisha hasira kwa wakazi wa Tarime baada ya Mtikila kurejea hoja hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Starehe hivi karibuni, na hivyo kusababisha kupigwa mawe na kujeruhiwa kichwani.
Licha ya Mtikila viongozi na makada wa vyama vya CCM na NCCR-Mageuzi, wamekuwa wakiitumia hoja hiyo katika mikutano ya kampeni za uchaguzi huo, na kujikuta wakinusurika kupigwa ama kuzomewa.
``Ninawashangaa hawa watu Tarime, sijui wamelishwa nini na Mbowe, walipigwa, lakini bado wanaenda kumpokea Mbowe,?wanamfanya Mbowe kama Mungu-mtu,`` alisema.
Hata hivyo, Mtikila aliukejeli umati wa watu waliomlaki Mbowe, na kusema uliwahusisha wahuni wanaovuta bangi na kunywa pombe haramu ya gongo.
Kwa upande mwingine, Mtikila alidai kuwa DP, NCCR-Mageuzi na CCM, vinatekeleza mpango wa kuhakikisha Chadema inashindwa katika uchaguzi huo.
Alidai kuwa wameamua kuwa na mpango huo kwa sababu matumizi ya fedha za umma zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo wilayani Tarime, zinafujwa na uongozi wa halmashauri hiyo inayoongozwa na Charles Mwera, ambaye pia ni mgombea ubunge kupitia Chadema.
Alisema nakala ya matumizi ya fedha hizo, iliwasilishwa kwake na NCCR-Mageuzi kupitia kwa maofisa wa serikali ya CCM ambao hata hivyo hakuwataja.
``CCM na NCCR-Mageuzi wanazungumza kuhusu ukweli huu? wenzetu NCCR walishaanza, tunachotaka ni kuwatendea haki wananchi wa Tarime,`` alidai.
Waziri adai polisi wako ngangari Tarime
Naye Simon Mhina anaripoti kuwa serikali imesema Jeshi la Polisi limejizatiti vilivyo kuhakikisha uchaguzi mdogo wa Tarime unafanyika kwa amani na kusisitiza kwamba halitasita kutumia nguvu iwapo wanasiasa watachochea fujo kwa kisingizio cha demokrasia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki, alisema suala la kampeni za uchaguzi huo pamoja na upigaji kura kukamilika kwa amani, bila mabomu limo mikononi mwa wanasiasa.
Hatuwezi kuachia vurugu yo yote, hatuwezi kukubali kuona watu waovu wanafurukuta, tunataka uchaguzi ufanyike kwa amani, alisema.
SOURCE: Nipashe