Date::10/11/2008
Waziri Chilligati atimuliwa hospitali Tarime
*Majeruhi aliyekwenda kumuona ahamishiwa Bugando
Mpoki Bukuku na Mussa Juma, Tarime
Mwananchi
KATIBU mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Chiligati na Mbunge wa Musoma, Vedasto Matayo jana walitimuliwa hospitali wakati walipokwenda kuwajulia hali vijana waliojeruhiwa kwa mapanga katika vurugu zilizotokea juzi wilayani Tarime.
Tukio hilo lilitokea jana asubuhi wakati Chiligati, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, alipowasili kwenye zahanati ya Tarime kuwatembelea vijana hao waliokatwa mapanga wakati kulipotokea mapambano baina ya wafuasi wanaoaminika kuwa wa CCM na Chadema, lakini akapokelewa na vijana waliomzuia kuingia hospitalini.
Toka hapa hakuna mtu mwenye shida na nyie... mimi nitamuuguza mdogo wangu sihitaji msaada wenu, alisikika mmoja wa jamaa waliokuwa sehemu ya mapokezi ya hospitali hiyo, wakionekana dhahiri kuwa walipania kutoruhusu viongozi na wafuasi wa CCM kuona majeruhi hao.
Hilo lilitokea baada ya Chiligati kuongea na waandishi wa habari jana kuhusu tukio hilo lililotokea kwenye Uwanja wa Sabasaba wakati vijana wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chadema walipokuwa wakiandaa eneo ambalo ndege ya kukodi wanayoitumia kwa kampeni ingetua na kuzuiwa na vijana wanaoaminika kuwa wafuasi wa CCM.
Jana asubuhi, Chiligati alikwenda kwanza Hospitali ya Wilaya ya Tarime, lakini akaambiwa kuwa vijana hao walikuwa hawajafikishwa hospitalini hapo na hivyo kuambiwa ajaribu kwenda zahanati hiyo ya binafsi.
Baada ya kutoka hapo alielekea moja kwa moja katika zahanati hiyo iliyo katikati ya mji, akiwa ameongozana na Mathayo, ambaye pia ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM.
Walipoingia mapokezi wakiwa wamevalia sare za CCM, kundi la watu lilitoka ndani ya hospitali hiyo na kuanza kupiga kelele kupinga kitendo chao cha kwenda hospitali hipo.
Hali ilianza kuwa mbaya baada ya vijana zaidi waliokuwa nje kuanza kujazana na wengine wakitishia kuwapiga iwapo wasingeondoka mara moja katika eneo hilo.
Hata kama umekuja na gari la milioni 400, ni lako na wenzako sisihatuhitaji msaada... toka kabla hatujakuchenjia, alisema mmoja wao. Pamoja na jitihada za Chiligati kuwasihi kuwa walikuja mahali hapo kwa nia njema ya kutaka kuwajulia hali vijana hao, hakuna aliyewaelewa na kuzidisha amri ya kuwataka watoke nje na kuondoka.
Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, Chiligati alitoka nje ambako, pia alizongwa na kurushiwa maneno ya kashfa yeye na chama chake, kabla ya kuingia garini na kuondoka.
Baada ya kutoka eneo hilo, Chiligati alionyesha wazi kukerwa na kitendo
hicho na kusema kuwa kitendo hicho hakikuwa cha kistaarabu na kwamba watu wenye akili timamu wasingeweza kufanya hivyo.
Suala la kumjulia hali mgonjwa halina itikadi. Tumekuja kwa nia njema, lakini naona hawa jamaa wanashindwa kuelewa, alisema baadaye kabla ya kwenda mjini Sirari ambako alishiriki kumnadi mgombea wa ubunge kwa tiketi ya CCM, Christopher Kangoye.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema jana, Chiligati alieleza kusikitishwa na mapambano yaliyohusisha mapanga, akisema hata chama chake, CCM hakikufurahishwa na vurugu hiyo.
Lakini akageukia vyombo vya habari na kusema: "Watu waliojeruhiwa ni watatu tu, lakini magazeti yameandika kana kwamba Tarime nzima wamekatwa mapanga."
Wakati huohuo, majeruhi Genya Sabai alitarajiwa kuhamishiwa hospitali ya rufani ya Bugando baada ya hali yake kuwa mbaya.
Sabai ambaye alikuwa amekatwa panga la shavu la kushoto, jana alianza kuvuja damu kutokea masikioni licha ya kushonwa katika jeraha lake.
Daktari mfawidhi wa zahanati ya Tarime, ambako majeruhi huyo amelazwa, Dk Philemon Hungiro alisema hali yake sio nzuri na hivyo anapaswa kuhamishiwa hospitali ya rufani ya Bugando.
Jana tulimshona nyuzi za ndani sita na nje nyuzi 19, lakini leo damu zinatoka hivyo tunashauri apelekwe Hospitali ya Rufani ya Bugando, alisema Dk Hungiro.
Alisema hali za majeruhi wengine Masham Edward(23) mkazi wa Rebu, Athuman Selemani (22) mkazi wa Ronsoti na Joseph Daniel(25) Songambele zinaendelea vizuri na wameruhusiwa kutoka hospitali.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana, ndugu wa Sabai, Paulo Agostine na dada wa Modesta Mwita, walisema walilazimika kumkatalia Waziri Chilligati kuonana na ndugu yao kutokana na kuamini kuwa CCM ndio waliomshambulia.
Amekuja hapa Chiligati akiongozana na Mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Matayo, lakini tumewafukuza na tumewaambia kwanza wawakamate watuhumiwa, alisema Mwita.
Alisema anawajua kwa majina vijana ambao walimshambulia Sabai na wenzake.
Leo asubuhi mimi nimewakuta hawa watuhumiwa wakiwa ofisi za CCM na wanalindwa na viongozi, sasa tunashangaa iweje huyu Chiligati aje kumuona mgonjwa, alisema Mwita.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Leberatus Barlow alisema juzi kuwa bado wanawasaka watuhumiwa hao, ili kujibu shitaka linalowakabili na tayari gari lililotumika linashikiliwa.
Wakati huohuo, kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime, zinahitimishwa leo katika mikutano itakayofanyika mjini Tarime na eneo la Nyamongo ambapo kuna migodi ya machimbo ya dhahabu.
Kuhitimishwa kwa kampeni hizo kunatazamiwa kuwa kwa aina yake baada ya CCM kushusha helikopta ya pili kupambana na helikopta moja ya Chadema.
Jana Chadema walikuwa wakiendelea kutumia helikopta yao moja ikiwa imembeba mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, mgombea wa ubunge, Charles Mwera, kada aliyehamia Chadema toka CCM, Mwita Mwikwabe Waitara na Tundu Lissu.
Wakati CCM inatarajia leo kuhitimisha kampeni katika uwanja wa michezo Sabasaba, Chadema leo watakuwa na mikutano mitatu tofauti ambayo itamalizikia katika machimbo ya Nyamongo na mjini Tarime.
Naye Festo Polea anaripoti toka Dar es Salaam kuwa, baadhi ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoa wa Dar es Salaam, wameshinikiza mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe kujiuzulu mara moja.
Wanachama hao jana walifanya maandamano ya amani kwa lengo la kushinikiza mwenyekiti huyo kujiuzulu na kusema endapo mwenyekiti huyo atashindwa kufanya hivyo wataitisha mkutano mkubwa ili kumshinikiza.
Wanachama hao pia walitaka chama hicho kiitishe kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Chadema chenye lengo la kujadili mustakabali wa chama kwa madai kuwa, kwa sasa chama hicho kimekuwa kikiyumba kutokana na ukabila unaoonyeshwa.