Waziri Ngeleja awekwa 'kiti moto' Busanda
Na Frederick Katulanda, Busanda
Mwananchi
Mgombea Ubunge wa Chadema Finias Magesa akijinadi kwa wapiga kura katika mkutano wa chama chake uliofanyika Katoro jana na kuhudhuriwa na Zitto Kabwe.
WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja jana alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuzongwa na kundi la wananchi waliomuhoji juu ya ahadi zake za umeme alipowasili katika mji wa Katoro wilayani Geita.
Tukio hilo mithili ya mdahalo lilitokea kati ya majira ya ya saa 9:30 hadi saa 10:15 muda mfupi tu baada ya Ngeleja kuwasili Busanda akitokea Mwanza.
Maswali yalianza baada ya Waziri Ngeleja kusalimiana na wananchi hao na akajibiwa kwa kuonyeshwa alama za vidole viwili.
Hali hiyo ilimfanya waziri huyo kuwauliza wananchi hao sababu za kuichukia CCM wakati imekuwa ikijitahidi kuwaletea maendeleo na ndipo walipoanza kumuuliza maswali huku akiyajibu wakati fulani kugeuka mabishano.
"Hatuwezi kuwashangilia nyinyi... mmetuahidi umeme siku nyingi na hatuuoni, leo mnakuja kutuambia nini. Alikuja hapa sijui (Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam) Malima akasema umeme utakuja, lakini wapi hatujaona lolote mpaka leo," alisema mwananchi mmoja.
Ngeleja alipotaka kujibu, mwananchi mwingine alidakia kusema: "Hata kwenye machimbo mmekuwa mkitunyang'anya maeneo yetu na kuwapa wawekezaji. Sisi mnatuona hatufai kama vile ni wakimbizi ndani ya nchi yetu."
Ngeleja alilazimika kuwatuliza na kuwaomba wapunguze maswali ili ajibu swali moja baada ya jingine, lakini kila mtu akataka kumuuliza swali na kukawa na msuguano kati yake na wananchi.
Alianza kujibu kwa kusema kuwa serikali ipo mbioni na kwamba kinachofanyika sasa ni kufuata taratibu kwa sababu mchakato wa suala hilo hauwezi kumalizika siku moja, hivyo akawaomba wawe watulivu wakati mchakato ukiendelea.
Ngeleja alidai kuwa suala lao kuhusu umeme liko katika hatua ya kuridhisha na kwamba wanapaswa kutambua utaratibu wa kushughulikia miradi ya serikali umekuwa ukifanyika kwa hatua.
Majibu hayo yalipingwa na wananchi ambao walimwambia wamekuwa wakidanganywa kama watoto kwa sababu ya kutaka kura na wakishapata, hutoweka.
"Sikiliza basi nikujibu, wewe naona umetanguliza ushabiki tuu. Naomba unisikilize. Ni kweli tulipowaahidi umeme tulidhani mchakato ungekamilika mapema, lakini kuna mambo yametukwamisha, tunaomba mtuvumulie," alisema huku wananchi hao wakiendeleza maswali.
Wakati wakiendelea na mjadala huo, lilipita gari la mgombea CCM wa kiti cha
ubunge cha Busanda, Lolensia Bukwimba na mara moja wananchi hao wakageuka na kuanza kuzomea msafara.
Wakati wakiendelea kuzomea ndipo Ngeleja alipopata mwanya na dereva wake akawasha gari na kuondoka.
Waziri Ngeleja alitaja mlolongo wa maeneo ambayo alisema mengi yatapata umeme kabla ya kumalizika kwa mwaka huu, lakini mkakati wao wa umeme ulitibuliwa baada ya Bunge kukataa kuinunua mitambo ya umeme wa dharura ya Dowans Tanzania Limited.
CCM imekuwa na wakati mgumu tangu kuanza kwa kampeni za ubunge wa jimbo hilo lililoachwa wazi na Faustin Kabuzi Rwilomba ambaye alifariki akiwa nchini India alikoenda kutibiwa.