Zitto aitikisa Busanda
na Edward Kinabo, Geita
[ Source: Tanzania Daima ]
NAIBU Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, jana alitikisa mji wa Katoro wilayani Geita, baada ya kupokewa kwa maandamano makubwa alipoingia jimboni hapa kuendesha kampeni za kumnadi mgombea wa ubunge wa chama hicho, Finias Magessa.
Zitto aliyeingia Busanda akitokea Geita alipokewa kwa maandamano kuanzia kwenye kizuizi cha kuingilia mjini Katoro, na kutembea kwa miguu, hadi kwenye viwanja vya stendi ya Katoro.
Magessa, Zitto wa Busanda, CCM tunaizika, ndizo zilizokuwa kauli na nyimbo zilizokuwa zikitoka vinywani mwa vijana waliokuwa wakiyaongoza maandamano hayo kuelekea kwenye uwanja wa mikutano.
Baadhi ya vijana waliokuwa katika maandamano hayo walikuwa wamebeba jeneza lililovikwa kitambaa cha rangi ya kijani, wakiashiria kukizika Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kutumia jeneza hilo, lakini walipofika kwenye uwanja wa mikutano walilichoma moto jeneza hilo.
CCM haina dini, tunaizika kipagani, kwa kuchoma moto, tunaichoma, ndivyo walivyokuwa wakisema vijana hao huku wakishangilia.
Akihutubia umati mkubwa wa watu, uliohudhuria mkutano huo, Zitto alisema kutokuwepo kwa umeme katika jimbo hilo kunafanya gharama za bidhaa kuwa kubwa kuliko maeneo mengine nchini.
Mkipigia kura CCM maana yake mnakubali matatizo ya umeme, mmepata bahati ya kuondokana na matatizo, hii ni bahati pia ya kuikataa CCM, kwa kumchagua Magessa, alisema Zitto.
Aliongeza kuwa katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Kikwete, idadi ya maskini nchini imeongezeka kutoka watu milioni 11, mwaka 2005 hadi kufikia milioni 12.7 mwaka 2008.
Aliomba wakazi hao kumchagua Magessa ili awaongezee nguvu kuendeleza vita ya ufisadi inayoongozwa na wabunge 11 wa CHADEMA.
Aliongeza kuwa CCM ni chama cha mafisadi na hakuna mbuge wala mtu yeyote atakayeweza kupambana na ufisadi akiwa ndani ya CCM.
Aidha, alisema CCM imejiandaa kuwaleta wabunge wake wanaojidai kupinga ufisadi ili kuja kuwarubuni wakazi wa Busanda, kwamba chama hicho kinapambana na ufisadi.
Watakuja, kina Dk. Mwakyembe kuwaambia wao wanapambana na mafisadi, lakini hao ni wanafiki, na wao ni mafisadi tu, kwani huwezi kusema unapambana na ufisadi halafu ukiwa ndani ya CCM, alisema Zitto.
Alifafanua kuwa Magessa ni kijana msomi na CHADEMA imempima na kuridhika kuwa ana utashi na dhamira ya dhati ya kuwapigania wananchi wa Busanda.
Aliwataka wakazi wa Katoro kumchagua Magessa ili awe mtetezi wa kweli kwao kama wananchi wa Kigoma Kaskazini wanayotetewa naye.
Aiwahimiza kutunza vitambulisho vyao vya kupigia kura ili wavitumie kumhagu Magessa.
Aliongeza kuwa ni sheria kwa vijana wote wa Busanda kutengeneza manati na kutumia mawe kuwapiga mabalozi wote wa CCM watakaokuwa wanapita kwenye numba zao kununua vitambulisho vya kupigia kura ili waweze kukomesha ukiukwaji wa haki na sheria za nchi.
Hata hivyo, naye mgombea wa ubunge wa chama hicho, Finias Magessa, alihitimisha kwa kusema kuwa akichaguliwa atatumia asilimia 30 ya mshahara wake wa ubunge kusomesha watoto yatima waliomo ndani ya jimbo hilo na kuahidi kuwa sekondari zote za kata ndani ya jimbo hilo zinaendelezwa na kuboreshwa zaidi.