Simon Mhina
Maelfu ya wananchi wa Jimbo la Busanda, leo wanamiminika vituoni kupiga kura kumchagua atakayemrithi aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Kabuzi Rwilomba huku wagombea na viongozi wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo wakitambiana kwa kila mmoja kuibuka mshindi.
Vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali, ni pamoja na Chadema, ambayo imemsimamisha Finias Magessa na CCM, iliyomsimamisha Lolesia Bukwimba kuwania kiti hicho.
Vyama vingine, ni CUF kilichomsimamisha Oscar Ndalahwa na UDP, ambacho kimemsimamisha Beatrice Lubambe.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya vyama hivyo kufanya kampeni kwa kipindi cha zaidi ya wiki tatu, kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu, kuwanadi wagombea wao.
Kampeni hizo zilihitimishwa jana kwa Chadema kufanya mkutano wake wa hadhara katika viwanja vya Mnadani vilivyoko katika mji mdogo wa Katoro, ambako ni makao makuu ya jimbo.
UDP ilifunga kampeni za mgombea wake katika viwanja vya kituo cha mabasi, wakati CCM ilihitimisha katika viwanja vya CCM vilivyoko mjini humo na CUF kwenye viwanja vilivyoko katika Kata ya Nyarugusu, wilayani Geita.
Matukio, kauli na vitendo vingi, vimekuwa vikiripotiwa na vyombo vya habari kutokea tangu kuanza kwa kampeni hizo, vinavyolenga kuzua vurugu na kuhatarisha amani katika kuelekea uchaguzi huo.
Miongoni mwa matukio hayo, ni pamoja na kukamatwa kwa watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa baadhi ya vyama wakinunua shahada za kupiga kura kwa wapigakura.
Mengine, yalihusu wafuasi wa chama kimoja kuwashambulia kwa kuwapiga na kuwajeruhi wafuasi wa chama kingine.
Hata hivyo, hali chafu ya hewa kufikia jana, ilifanikiwa kudhibitiwa na Jeshi la Polisi, ambalo kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wake Mkoa wa Mwanza, Elias Kalinga limeongeza askari kutoka 113 hadi 183 kwa ajili ya kuimarisha ulinzi katika uchaguzi huo.
Askari hao, wakiwamo askari kanzu na wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliokuwa wamejiandaa na zana za kivita, yakiwa na magari ya kurusha maji yanayowasha mwilini, walifanya doria katika mji mdogo wa Wilaya ya Geita wa Katoro na vitongoji vyake kuanzia jana asubuhi na hali kuwa shwari.
Doria hiyo walikuwa wakiifanya kwa kutumia magari maalum ya polisi wakati huo wafuasi wa vyama vya Chadema na CCM wakiwa kwenye pikipiki, baiskeli na wengine kutembea kwa miguu wakizunguka maeneo mbalimbali ya mjini Katoro kuhamasishana kuhusiana na uchaguzi huo.
Katika hatua isiyo ya kawaida, polisi wote wamevua namba zao, ambazo huwa zinabandikwa kifuani ili waweze kutambulika kirahisi. Mmoja wa Polisi aliyeulizwa, alisema kwa kawaida wakiwa kwenye oparesheni kama hizo huwa wanaamriwa kuvua namba zao.
Ukiachilia mbali hayo, mchuano mkali katika uchaguzi huo umetabiriwa kuwa kati ya vyama vya Chadema na CCM, ambavyo vimeonyesha mbwembwe kubwa katika kampeni zao.
Mbwembwe hizo, ni pamoja na matumizi ya helikopta yaliyofanywa na Chadema na pia vikundi mbalimbali vya burudani na hamasa, kikiwamo kile cha Tanzania One Theatre (TOT) kwa CCM, ikiwa ni sehemu ya mikakati yao ya kutia chachu na hamasa kampeni za wagombea wao.
Katika kampeni zake, CCM ilikuwa na timu tano za kampeni zilizojichimbia katika Kata zote 13 za jimbo hilo kumnadi mgombea wake kwa siri na dhahiri. Timu hizo zilikuwa na watu wazito wa chama na serikali.
Hata hivyo, kulingana na tathmini ya hali ya siasa jimboni hapa na hali halisi ya CUF, lolote linaloweza kutokea kwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Pia, ule muujiza wa Yesu Kristo wa kubariki mkate mmoja kuwa mingi ukitarajiwa kutokea kwa chama cha UDP, ambacho matumaini ya kushinda uchaguzi huo ni finyu sana.
Licha ya kampeni za kumnadi mgombea wake kutokuwa na mbwembwe, CUF inaweza kubadili hali ya mambo kwa kuibuka mshindi na kuwashangaza wengi kutokana na faida iliyonayo ya kujijengea mtandao wa chama kwa muda mrefu katika wilaya Geita.
Akizungumza na Nipashe mjini Geita, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema wana matumaini makubwa ya kushinda uchaguzi huo ingawa alisema hawezi kutaja asilimia za ushindi huo kwa vile huenda watu waliojiandikisha wasiweze wote kujitokeza kupiga kura.
Katibu Mkuu wa UDP, John Nkolo alisema wana matumaini ya kushinda katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, naye aliungana na Profesa Lipumba kwa kusema kwamba, hawezi kutaja watashinda kwa asilimia ngapi kwa vile vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo ni vinne.
Mratibu wa Kampeni za CCM, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, George Mkuchika alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, mgombea wao, Rwilomba alishinda kwa asilimia 79, hivyo katika uchaguzi wa leo wana mategemeo ya kufanya vizuri zaidi katika uchaguzi wa leo.
Naye mgombea wa Chadema, Magessa alipoulizwa na Nipashe aliwataka wananchi kusubiri matokeo akisema kwamba, kwa sasa bado wangali kwenye mapambano.
Awali, Afisa Habari wa Chama hicho, David Kafulila alisema kulingana na utafiti walioufanya wana matumaini makubwa ya kushinda uchaguzi huo kwa zaidi ya asilimia 78.
Katika kile kinachoonekana kama jumuiya ya kimataifa imeamua kufuatilia kwa karibu uchaguzi huo uliovuta hisia za watu wengi ndani na nje ya nchi, imetuma waangalizi wake jimboni hapa kuangalia hali ya mambo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geita jana, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Lewes Makame, alitaja nchi zilizotuma waangalizi wao katika uchaguzi huo, kuwa ni Uholanzi, Marekani, Uingereza na umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
Katika kuhakikisha kuwa kila kitu kinaenda sawa, wajumbe wote wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa wamehamia Busanda, kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa ufanisi, uhuru na amani.
Tambo na vijembe vilivyokuwa vimetawala kwa kila chama jimboni Busanda jana jioni vilifikia tamati. Hata hivyo, tofauti na ilivyodhaniwa kila chama kilihitimisha mikutano yake kwa amani.
Wakati viongozi wa vyama vya upinzani bado wapo mijini Busanda, wale wa CCM waliondoka kuelekea mjini Geita kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam.
Viongozi hao wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Bara, George Mkuchika, wako mjini Geita wakijipumzisha katika hoteli ya Tulo kujiandaa na safari kesho.
Habari zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni zinasema kuwa matokeo ya awali yanaonyesha kuwa CCM wanaongoza katika uchaguzi mdogo wa Magogoni baada ya kupata kura 2910 na CUF 1972, wakifuatiwa na chama cha SAU ambacho kimepata kura chache katika uchaguzi kati ya wapiga kura 5493, Mwinyi Sadallah anaripoti.
Kwa matokeo hayo, ni dhahiri kuwa CCM kimeshashinda katika uchaguzi huo na matokeo kamili yalitarajiwa kutangazwa saa tatu usiku jana.
NIPASHE JUMAPILI