Boniface Meena na Geofrey Nyang'oro, Igunga
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimewawekea pingamizi wagombea ubunge kupitia vyama vya Chadema na CCM kwa madai kuwa hawakurudisha fomu kwa kufuata kanuni na sheria za uchaguzi. Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Msimamizi wa Uchaguzi, Magayane Protas alisema ametupilia mbali pingamizi hilo."Mgombea wa CUF, Ndugu Mahona amewasilisha pingamizi dhidi ya wagombea wa Chadema na CCM akidai kuwa walirudisha fomu kinyume cha sheria. Lakini nimeangalia sheria inavyoeleza na kuona hawakufanya kosa lolote wakati wakirudisha fomu hivyo, nimelitupilia mbali pingamizi hilo."
CHADEMA Kuzindua Kampeni Igunga Leo
Chadema kinatarajia kuzindua kampeni zake rasmi leo. Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa chama hicho, Waitara Mwita alisema kuwa watawapokea viongozi wa kitaifa kwa maandamano kuanzia saa 6:00 mchana ili kuelekea kwenye eneo la mkutano katika Uwanja wa Sokoine.
"Tutaanza maandamano yatakayoongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa na wajumbe wa kamati kuu pamoja na wabunge na mkutano utaanza saa 8:00 mchana na kumalizika saa 12:00 jioni," alisema
Chanzo:
CUF yakwama kuvizuia CCM, Chadema Igunga