[TABLE="class: contentpaneopen"]
[TR]
[TD="class: createdate"]Friday, 09 September 2011 21:57
[/TD]
[/TR]
[TR]
[TD]NI KWA AJILI YA KUSHIRIKI MKUTANO WA UZINDUZI LEO, ROSTAM HAKIJAELEWEKA
Mwandishi Wetu, Igunga
JIMBO la Igunga jana lilikumbwa na kitimtim cha maandamano ya wanachama na wapenzi wa CCM waliokuwa wakipita katika mitaa mbalimbali kuhamasisha wakazi wa hapa kujitokeza kwa wingi leo kwenye ufunguzi wa kampeni za chama hicho zitakazozinduliwa na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.Kadhalika, mji huo ambao umeingia kwenye pilikapilika za uchaguzi mdogo wa ubunge, umeshuhudia vigogo wa CCM wakiongozwa na Mkapa wakihamia kwa muda mjini humo, kuhudhuria uzinduzi wa kampeni za chama hicho ambao unafanyika baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wake, Rostam Aziz (CCM).
Rostam licha ya kuachia nafasi hiyo huku akiwashutumu baadhi ya vigogo kuhusika na kile alichokiita siasa chafu, ametajwa kuwa miongoni mwa watakaoshiriki katika uzinduzi wa kampeni hizo. Hata hivyo, hadi jana jioni kada huyo wa CCM hakuwa ameonekana mjini humo hivyo kuzua wasiwasi kuhusu ushiriki wake.
Vigogo wa CCM waliowasili hapa ni Makamu Mwenyekiti (Tanzania Bara), Pius Msekwa, Katibu Mkuu, Willson Mukama. Mwingine ni Mtunza Hazina, Mwigulu Nchemba ambaye pia ndiye Mratibu wa Kampeni za chama hicho katika uchaguzi huo na viongozi wengine wa wilaya zote za Mkoa wa Tabora.
Awali, kulikuwa na taarifa kwamba Mukama na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye wasingekwenda Igunga kwa kile kilichodaiwa kwamba walikuwa hawatakiwi kutokana na kusimamia kidete suala la kujivua gamba ambalo lilimngoa Rostam.
Jana, makada wa CCM walizua kitimtim ambacho kilianzia kwenye ofisi za chama hicho za wilaya na baadaye kuzunguka mitaa mbalimbali na kadri muda ulivyokuwa unasonga, idadi yao iliongezeka na kuwa shamrashamra za aina yake.
Maandamano hayo yaliandamana na nyimbo za kukisifu chama hicho tawala, viongozi wake pamoja na mgombea wa chama hicho jimboni humo, Dk Dalaly Peter Kafumu.
Kinamama na vijana hawakusita kuonyesha hisia zao pale waliposerebuka mitaani kucheza nyimbo za kukisifu chama hicho ambazo ziliandamana na majigambo ya ushindi kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 2, mwaka huu.
Chadema juzi kilizindua kampeni zake na leo ni zamu ya CCM. Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, Mkapa, atakuwa mgeni rasmi kwenye shamrashamra hizo za kupuliza kipenga cha kuanza kumnadi Dk Kafumu.
Mkapa aliwasili hapa juzi na kulakiwa na wanachama wa CCM waliofurika kwa wingi kumlaki. Ilibidi asimamishe gari lake na kuupungua mkono umati wa watu uliofika kumlaki huku akitabasamu na baadhi ya wafuasi wa chama hicho kumsabahi kwa salamu aliyokuwa akiitumia mara kwa mara alipokuwa rais ya "mambo!"
CCM itazindua kampeni hizo katika Viwanja vya Sokoine, mjini hapa na tayari kuna kila dalili za kampeni hizo kuvunja rekodi kutokana na maandalizi yaliyofanyika jana.
Waswahili husema, "Nyota njema huonekana asubuhi" na ndivyo CCM kilivyofanya jana kwa kutikisa jimbo hili kwa maandamano yaliyovuta umati mkubwa wa watu.
Hali hiyo ni tofauti na wakati mgombea wa CCM aliporejesha fomu kimyakimya kutokana na kuwa katika maombolezo ya kifo cha mtoto aliyegongwa na gari na kufariki dunia alipokuwa katika eneo ambalo wanaCCM walikuwa wamekusanyika kumsindikiza Dk Kafumu kwenda kuchukua fomu.
Maandamano ya CCM jana yalikuwa na vimbwanga kadhaa, miongoni vikiwa ni wafuasi hao walioonyesha kuwa na shauku kubwa ya kukipigia debe chama hicho kuingia kwenye tafrani ya kugombea bendera.
Tukio hilo lilitokea kwenye Ofisi ya CCM Wilaya ya Igunga, pamoja na wingi wa bendera ndogondogo za chama hicho zilizomwagwa mbele ya ofisi hiyo, baadhi walikosa.
Baadhi ya wafuasi wa CCM ambao wanakaa maeneo ya mbali na eneo la uzinduzi walianza kufika kwa wingi hapa jana tayari kwa uzinduzi huo.
Kutokana na jimbo hili kutokuwa na magari ya kutosha ambayo ni rasmi kwa abiria, wengi wa wapenzi wa CCM walioingia hapa, walitumia gari aina ya Land Rover ambayo huweza kupita hata kwenye barabara korofi.
Nape aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba kampeni hizo zinaratibiwa na CCM Wilaya ya Igunga na kwamba viongozi wowote wa kitaifa watakaopata fursa ya kwenda, watakuwa wamefanya hivyo kwa mapenzi yao na siyo kuagizwa kwenda kufanya kampeni.
Kuna tetesi pia kuwa Rostam atakuwa miongoni mwa wanachama wa CCM watakaompigia debe Dk Kafumu ambaye anapambana na Joseph Kashindye wa Chadema, John Maguma wa SAU na Leonard Mahona wa CUF.
Nape akitangaza uteuzi wa Dk Kafumua alisema katika kufanikisha kampeni za CCM, wanachama waliowania kuteuliwa katika nafasi hiyo na kushindwa wameahidi kuwa watashiriki kikamilifu katika kampeni hizo ili kumnadi mgombea huyo wa chama hicho.
Dk Slaa amfuata Dk Kafumu alikozaliwa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa jana alitinga kijiji anachotokea Dk Kafumu na kuwaeleza wananchi wa eneo hilo kuwa mgombea huyo hawezi kuwaletea maendeleo kwa kuwa amekuwa ni tatizo ndani ya Serikali.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni za mgombea wa Chadema, uliofanyika katika Uwanja wa Mnadani katika Kijiji cha Lugubu, Dk Slaa alisema hivi sasa Watanzania wanahitaji ukombozi kwa kuwa hali zao ni mbaya.
Nawaambieni Kafumu amekuja kujenga nyumba hapa kwa sababu za uchaguzi tu na wala halali hapa, nawaombeni mumchague Kashindye ambaye mmekuwa naye kwa muda mrefu ili awasaidie kuondokana na umasikini huu uliokithiri, alisema Dk Slaa.
Alisema kuwa wananchi wa Igunga wamekuwa na mbunge wa CCM aliyeachia ngazi kwa miaka zaidi ya miaka 15 lakini hajawasaidia kitu zaidi ya kuwadanganya kila wakati wa uchaguzi ili aweze kutimiza matakwa yake.
Wananchi mmeliwa sana na CCM sijui kama mnajua maana ya mbunge, Rostam amekuwa hapa kwa zaidi ya miaka 15 je, amekuja kuwaona baada ya kumchagua? Wakati wa kudanganywa umekwisha na msikubali Serikali ya CCM ambayo inawagawia kanga za uongo na baadaye kuwatelekeza, alisema.
Mbunge wa Meatu (Chadema), Sylivester Kasulumbai alisema kuna tatizo kubwa ambalo limeletwa na CCM ambalo ni ufisadi huku akikifananisha chama hicho na fisi ambaye akiwekwa buchani haachi hata kipande cha mfupa.
Matatizo yapo lakini hayakuletwa na Mungu ni kutokana na kumweka fisi kwenye bucha ambaye haachi hata mfupa, nawaombeni CCM isiwafanye tena hivyo na wala isiwageuze wananchi kama kuku wa kienyeji, alisema Kasulumbai.
Kwa upande wake, Kashindye aliwaomba wananchi wa eneo hilo kumchagua ili waweze kuleta maendeleo kwa pamoja: Nawaombeni mnichague tuachane na unyonyaji kwani bila CCM maendeleo yanawezekana.[/TD]
[/TR]
[/TABLE]