Mamia ya wagombea wa vyama vya upinzani katika uchaguzi wa serikali za mitaa ujao wameenguliwa kushiriki uchaguzi huo.
View attachment 3148852
Chama cha ACT Wazalendo kimeripoti takribani asilimia 60 ya wagombea wake wameenguliwa kushiriki uchaguzi kwa sababu walizozitaja kukosa msingi wa kisheria na kanuni.
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi, tarehe 8 Novemba ilikuwa ni siku ya uteuzi wa wagombea waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Hata hivyo wagombea wa vyama vya upinzani pekee ndio wameripotiwa kuenguliwa kwasababu ya kukiuka utaratibu au kukosa vigezo mbalimbali.
Soma, Pia;
•
CHADEMA wanatoa Tamko kuhusu hali ya Kisiasa inayoendelea nchini kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Wakati Chadema ikiendelea kupata orodha kamili ya wagombea wao wote walioenguliwa nchi nzima, jana tawi la chama wilayani Kilosa liliwasilisha barua yenye uthibitisho wa wagombea 242 walioenguliwa katika wilaya ya Kilosa pekee.
Chadema inasema wapo wagombea wengine kutoka jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma ambao si tu wameenguliwa kushiriki uchaguzi bali pia wameshutumiwa kutokuwa raia.
Chama cha ACT Wazalendo kimesema katika jimbo la Tunduru Kaskazini, wagombea wao 69 wameenguliwa, waliopitishwa ni 23 tu.
Jimbo la Kigoma mjini wagombea wao 63 wameenguliwa na kubakizwa wagombea watano pekee.
Jimbo la Tunduru Kusini, ambalo ACT Wazalendo wanadai kuwa ni moja ya ngome yao kubwa, ni wagombea 13 tu ndio walioteuliwa huku wagombea 34 wakiwa wameenguliwa.
“Maeneo mengi ambayo wameengua wagombea wetu ni maeneo ambayo tulikuwa tunatarajia kushinda.
Wamefanya ‘mapping’ ya kuangalia huyu ana uwezo, ndio wanamuengua.
Kwenye ngome zetu hasa ndio tumeathirika pakubwa kuliko sehemu zingine” amesema Esther Thomas, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Tanzania Bara. Baadhi ya wagombea wa ACT Wazalendo wameambiwa sababu ya kuenguliwa ni kutokuwepo kwa nafasi walizoomba na kujaza fomu vibaya. Chadema wamesema kuna wagombea wao ambao wameenguliwa nje ya muda wa kisheria na pasipo kuwekewa mapingamizi halali.
“Hali ni mbaya sana maana wagombea wetu wameenguliwa hadi usiku, ambapo ni nje ya muda. Watu tu wanaitwa wanapewa barua, wanaambiwa wameenguliwa” amesema Jon Mrema, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema.
Mrema anasema baadhi ya wagombea wameambiwa wameenguliwa kwasababu chama chao cha Chadema hakijasajiliwa. Wagombea wengine kutoka Dar es Salaam wameenguliwa baada ya kujaza katika fomu zao kwamba kazi inayowapatia kipato ni ujasilia mali. “Wasimamizi wanawaengua wanasema ujasiliamali sio kazi. Sasa sisi tunajiuliza, kama ujasiliamali sio kazi halali ilikuwaje serikali ikawapa hadi vitambulisho?” amehoji Mrema.
Vyama vyote vimewasilisha mapingamizi kutaka wagombea wao warudishwe, na wanatarajia kupata majibu kufikia mwisho wa siku leo. Vyama pia vina siku tatu za kukata rufaa ambapo maamuzi ya rufaa zote yatatoka tarehe 13 Novemba. Siku mbili zilizopita, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa alivikumbusha vyama vya siasa , wagombea na wadau wengine wa uchaguzi kwamba muhisika yeyote asiyeridhika na taratibu za uchaguzi ana haki ya kukata rufaa.
“Mtu yeyote mwenye malalamiko ni vyema akajikita katika kufata sheria, kufuata kanuni, kwani kanuni na sheria zetu hazijaacha ombwe kutokana na jambo lolote linaloweza kuibuka kutokana na uchaguzi huu” amesema Mchengerwa.
View attachment 3148853
Siku ya Ijumaa Katibu Mwenezi wa chama tawala Chama Cha Mapinduzi Amos Makalla alitoa wito kwa Wizara ya Tamisemi inayosimamia uchaguzi kuhakikisha inatenda haki kwa vyama vyote huku akisisitiza kwamba CCM haihitaji kubebwa. “CCM hatuhitaji upendeleo wowote, CCM hatuhitaji kubebwa, kwahiyo tuko tayari, tulishajipanga, hatuhitaji mbeleko” alisema Makalla.
Chadema wamefananisha kile kinachoendelea sasa na yale yaliyotokea mwaka 2019 ambapo wagombea wa vyama vya upinzani karibu kote nchi walienguliwa kushiriki katika uchaguzi.
“Awali tulidhani kwamba baada ya serikali na Rais Samia Suluhu Hassan kusema uchaguzi utakuwa uhuru na wa haki, tukadhani yale yam waka 2019 hatutarudi kule. Lakini ghafla tunaona tunarejeshwa mwaka 2019, na imekuwa ghafla mno. Na tulianza kuona dalili hizi pale wakati wa zoezi la uandikishwaji ambapo hadi Watoto ambao hawajafikisha miaka18 waliandikishwa” amesema Mrema.
Hata hivyo vyama vyote viwili Chadema na ACT Wazalendo vimesisitiza kwamba havitajitoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na malalamiko ya dhulma wanazotendewa wagombea wao.
“Wanachokitafuta ni kutuchokoza, kutupa sababu tuseme kwamba tunasusa.
Tumeshasema hatutasusa hata tukibaki na Kijiji kimoja, tutaendelea kushiriki kwasababu kushinda mtaa mmoja ni ushindi wa maana kwasababu sasa hatuna mtaa hata mmoja nchi hii tunaouongoza kati ya mitaa takribani elfu 5 iliyopo. Kati ya vitongoji elfu 64 vilivyopo katika nchi hii hatuongozi kitongoji hata kimoja. Kwahivyo hata tukibaki na kitongoji kimoja na tukashinda, maana yake ni kwamba tuna ushindi wa asilimia 100,” amesema Mrema.
“Siku zote sisi hatususii shamba. Maana ukisusia shamba, litaliwa lote litaisha. Kwahiyo tunapambana huku tukishiriki, na tunashiriki huku tukipambana” amesema Thomas.
Credit: BBC Swahili
Soma:
•
ACT wazalendo: Wagombea wetu Kigogo, Dar es salaam hawajateuliwa
•
John Mrema aanika madudu ya TAMISEMI, waongeza sifuri na herufi kuwakosesha sifa Wagombea