Na: Kitila Mkumbo
KUNA imani kwamba Watanzania ni wepesi wa kusahau mambo makubwa ya kitaifa. Kuna imani pia kwamba Watanzania ni wepesi wa kukubali yaishe pale wanapoona jambo fulani walilokuwa wanalidai limekataliwa na serikali, hata kama wanajua kuwa msimamo wa serikali si sahihi.
Hata hivyo, inaonekana tumeanza kubadilika, tena kwa kasi ambayo hata watawala itabidi waanze kujiuliza kunani.
Dalili za Watanzania kubadilika zinaonyeshwa na jinsi ambavyo tumeweza kulibebea bango tatizo la ubadhirifu katika Benki Kuu. Ubadhirifu wa kutisha katika Benki Kuu umeendelea na inaonekana utaendelea kubaki katika akili na midomo ya Watanzania kwa muda mrefu ujao.
Tutakumbuka kwamba sakata la ubadhirifu liliwekwa hadharani na wabunge wa upinzani kwa mara ya kwanza katika bunge la bajeti la mwaka jana. Kwa hiyo, ni takribani zaidi ya nusu mwaka sasa bado tunaendelea kulijadili.
Hii ni tofauti na matukio mengine mengi ya kitaifa yaliyowahi kutokea, yakiwemo yale ya mikataba ya aibu inayohusu kampuni za kusambaza umeme za IPTL na Richmond pamoja na ile ya madini. Vilevile sakata la Benki Kuu limeweka historia mpya katika nchi yetu kwani ni kwa mara ya kwanza wananchi waliweza kukubaliana na maelezo ya upinzani na kukataa yale yaliyotolewa na Serikali ya CCM ya kujaribu kuukana au kuutetea ubadharifu huo.
Pamoja na hatua nzuri ya kutokusahau mapema mambo mazito ya kitaifa inayoanza kujitokeza miongoni mwa Watanzania, inaonekana bado tuna tatizo la kutambua chanzo halisi cha matatizo ya ubadhirifu katika nchi yetu. Inaonekana wengi wetu tunaendelea kuamini kwamba matatizo ya ubadhirifu katika serikali yetu yanasababishwa na watu wachache waliopo katika mamlaka na hayatokani na mfumo. Kwa hiyo inaonekana tunaelekea kuamini kwamba tunaweza kumaliza tatizo la ubadhirifu kwa kuwatoa katika serikali wabadhirifu ambao pengine ni wachache tu.
Mimi siamini kwamba tatizo la ubadhirifu katika nchi yetu ni la watu wachache wanaotumia madaraka yao vibaya. Ninaamini kabisa kwamba hili ni tatizo la kimfumo ambalo halikutokea kwa bahati mbaya bali limetengenezwa mahsusi kama njia ya kulinda huo mfumo uendelee kubaki hapo ulipo.
Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba, tatizo la samaki wenye sumu kwenye bwawa haliwezi kwisha kwa kumtoa samaki mmoja mmoja. Samaki hawawezi kuwemo kwenye bwawa pasipo kuwemo maji. Kwa hiyo sasa dawa ya kuwatoa samaki wenye sumu kwenye bwawa si kuwavizia samaki wanaojitokeza nje na kuwaua bali ni kukausha maji yote kwenye bwawa na kuanza upya. Maji yakishakauka bwawani samaki wote watakufa na hivyo utapata nafasi ya kuweka maji mengine na kupandikiza samaki wapya.
Kosa ambalo tunaelekea kulifanya katika mapambano ya ufisadi ni kuwavizia mawakala wa ufisadi na kujaribu kuwatoa hawa tukifikiri huko ndiko kupambana na ufisadi. Kwa hiyo kuna watu wanaamini kwamba kama Dk. Daudi Ballali akifikishwa mahakamani, basi tutapata jibu la wale waliotuibia pesa pale Benki Kuu.
Kuna watu wengine wameenda mbali hata kutaka Dk. Ballali apewe kinga ili awataje wenzake walioshiriki katika kutafuna hayo mapesa. Na kuna wengine wanasema kuwa Dk. Ballali alitumiwa tu na anajiandaa kuwaanika walaji hasa wa yale mapesa. Bila shaka ni kweli kabisa kwamba hata kama kweli Dk. Ballali alishiriki katika ubadhirifu wa mabilioni ya shilingi pale Benki Kuu isingewezekana akawa ameiba pesa zote zile peke yake.
Inabidi tujikumbushe pia hapa kwamba Dk. Ballali hakutoroka nchini. aliondoka kihalali, tena kwa kuaga. Kitu ambacho hatuna uhakika nacho ni sababu zilizomuondosha nchini, hasa baada ya ugonjwa na mahala anapotibiwa kufichwa na watawala kwa sababu wanazozijua wao.
Kwa hakika kuna kila sababu ya kuamini kwamba serikali imemficha Dk. Ballali, na kwa kumficha huko kuna makubwa zaidi wanayoyaficha. Bahati mbaya waliyo nayo wenzetu serikalini ni kwamba hawana uwezo wa kuficha ukweli kwa muda wote katika ulimwengu wa leo. Wakati utafika ukweli wote utakuwa wazi na itabidi wabuni uongo mwingine.
Kwa hiyo, ninachokataa mimi ni hii imani inayoanza kujengeka kwamba kuwajua walioshirikiana na Dk. Ballali katika wizi huu kutasaidia kutatua tatizo la ubadhirifu katika nchi yetu. Nakataa hili kwa sababu mbili. Ya kwanza ambayo nimeshaileza ni hiyo kwamba tatizo la ubadhirifu katika nchi yetu halisababishwi na watu wabaya au wabadhirifu katika serikali, bali mfumo wa ubadhirifu ambao ni sehemu muhimu ya utawala katika Serikali ya CCM.
Sababu ya pili ni ukweli kwamba hakuna jina hata moja atakalolitaja Dk. Ballali ambalo hatujalisikia mpaka sasa. Majina ya watu wote walioshiriki katika ubadhirifu wa Benki Kuu tayari yanajulikana sana kote nchini, mijini na vijijini na hata nje ya nchi. Kwa hiyo kama tungekuwa na mfumo ambao si wa kibadhirifu, tayari ungeshawachukulia hatua watuhumiwa wa ubadhirifu huo.
Kwa hiyo, utaona kwamba tunachotaka kukifanya hapa ni kujaribu kuwavizia samaki wenye sumu wanaojitokeza ili tuwatoe katika maji badala ya kutoa maji yenyewe. Mtazamo wangu hapa ni kwamba, bwawa letu (Tanzania) tumeliwekea maji (CCM) yenye sumu ambayo yanasababisha samaki wote (viongozi wa serikali) waliomo humo wapate sumu. Kwa hiyo dawa yake hapa ni kuyatoa haya maji (CCM) katika bwawa letu na kuweka maji mengine (chama kingine) ili tutakapopandikiza samaki wengine wasipate hiyo sumu.
Kimsingi Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kikitumia ubadhirifu kama mradi wa kutengeneza fedha za kukiwezesha kubaki madarakani. Tutakumbuka, kwa mfano, baada kuchaguliwa kwa kipindi cha pili serikali ya Rais Mkapa ilibuni mradi wa kununua ndege ya rais kwa bei kubwa huku baadhi ya wananchi wakikabiliwa na njaa. Tukalalamika sana, lakini tukakemewe na serikali ya Mkapa kupitia kwa Waziri Mramba kwa sentensi moja rahisi, lakini iliyojaa kiburi na dharau; kwamba ndege ya rais lazima inunuliwe hata kama hao wenye njaa itabidi wale nyasi.
Tukumbuke kwamba Rais Mkapa alikuwa ananunua ndege hii karibu kabisa na mwisho wa utawala wake. Kwa hiyo kama ingekuwa ni shida ya ndege kweli angekuwa hana ulazima wa kuharakisha na kuhakikisha kwamba inanunuliwa katika kipindi cha urais wake angeweza kuanzisha mchakato tu ambao rais anayemfuata angeweza kuukamilisha.
Kwa hiyo si vigumu kutambua kwamba huu ulikuwa ni mradi wa kujitengenezea hela kwa kisingizio cha kununua ndege ya rais. Hili lilikuja kuthibitishwa na wauzaji wenyewe kupitia Bunge la Uingereza kwamba bei tuliyonunulia ile ndege ilikuwa si halali bali tulijibambikizia. Sasa kama kweli mfumo wetu wa utawala si sehemu ya ubadhirifu huu iweje hadi leo hata baada ya kujua ukweli wote huu umeshindwa kuwachukulia hatua wale walioshiriki kuibambikia nchi yetu bei ya juu hiyo ndege ya rais?
Kuna watu pia wanaotaka tuamini kwamba Rais Kikwete na serikali yake wapo tofauti na hao waliopita. Mimi nitaendelea kuwauliza swali, kama kweli Rais Kikwete yupo tofauti, ilikuwaje amuweke katika baraza lake la mawaziri mtu ambaye aliwatukana Watanzania wenye njaa kwa kiwango cha kuwaambia wale nyasi, na ambaye alishiriki katika kutubambikia bei ya juu ya hiyo inayoitwa ndege ya rais?
Katika ulimwengu wa leo, ni Tanzania pekee ambako waziri wa serikali ya wananchi anaweza akadiriki kuwakejeli na kuwadharau wananchi waliomchagua kwa kiwango hiki na akaendelea kubaki madarakani. Kwingineko duniani kejeli kama hizi zilisikika mara ya mwisho kutoka kwa miongoni mwa mawaziri wa aliyekuwa Rais wa Zaire, Mobutu Sese Seko. Hata hivyo pamoja na udikteta na ujeuri wake, naye ilifika mahala akawafukuza mawaziri wa namna hii!
Kuna jambo lingine linalothibitisha kwamba ubadhirifu ni sehemu muhimu ya utawala wa CCM, na kwamba viongozi wetu wanatumia matatizo yanayoikabili nchi kubuni miradi ya kuchota pesa za walipa kodi kwa matumizi haramu. Hili ni pamoja na kutumia matatizo ya umeme katika kujitengenezea miradi ya kuchota fedha kutoka hazina kwa matumizi haramu. Sote tunakumbuka jinsi ambavyo serikali ya Rais Mkapa ilibuni miradi haramu ya IPTL na Net Group Solution.
Rais Mkapa akipingana na upembuzi wote wa kitaalamu, alizitetea kampuni hizi za kitapeli hadi akahakikisha zinapata nafasi katika kuiendesha TANESCO. Lakini sote tunajua jinsi ambavyo mashirika haya yalivyotumika kufyonza hazina yetu na watumiaji wa umeme kwa ujumla.
Kama vile ya IPTL na Netgroup hayakutosha, naye Rais Kikwete alipochaguliwa tu aliibuka na mradi mpya wa Richmond kama njia ya kutatua matatizo ya umeme yaliyokuwa yanaikabili nchi mwanzoni mwa utawala wake. Richmond wakalipwa mamilioni ya shilingi, lakini tukaendelea kukaa kwenye giza hadi pale mwenyezi Mungu alipotupatia mvua ya kuzalisha umeme. Richmond walilipwa na umeme hawakuleta! Sasa ni wapi kwingineko hapa duniani umewahi kusikia haya yakitendeka zaidi ya Tanzania?
Mlolongo wa matukio yote haya ya kibadhirifu ni uthibitisho kwamba huu ufisadi unaoendelea si wa bahati mbaya au kwamba unafanywa na watu wachache tu, bali ni mfumo na mtandao uliojengwa na kujijenga kwa makusudi na malengo maalumu. Narudia tena kwamba tatizo la ubadhirifu katika nchi yetu limetengenezwa na mfumo wa utawala uliopo kama njia ya kuiwezesha CCM kukabiliana na siasa za ushindani katika mfumo wa vyama vingi kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, kukineemesha kikundi cha watu wachache ndani ya utawala wa serikali ya CCM.
Hakuna shaka yeyote kwamba Watanzania tumeonyesha kukerwa na ubadhirifu unaoendelea katika serikali ya CCM. Lakini wasiwasi wangu ni kwamba tunayaelekeza mashambulizi yetu kusiko. Tunapoitaka serikali ya CCM iwachukulie hatua akina Dk. Ballali ni sawa na kumwambia mwizi ajikamate mwenyewe jambo ambalo haliwezekani. Ndiyo kusema madamu serikali ya CCM inaendelea kubaki madarakani, ufisadi hauwezi kwisha bali utashamiri kwa kubadili maumbo: IPTL, Richmond, Benki Kuu, na kadhalika.
Kuna haja basi ya kubadili mbinu za mapambano yetu dhidi ya ufisadi kwa kuelekeza mashambulizi dhidi ya mfumo unaozalisha mafisadi badala ya kulenga fisadi mmoja mmoja. Katika mapambano haya inabidi tujue kwa dhati kabisa mambo matatu. Mosi, lazima tumjue adui yetu, pili, tujue silaha yetu, na tatu, tujue fursa za kumshinda huyu adui.
Ni wazi kabisa sasa kuwa adui yetu hapa ni mfumo unaolea ufisadi, ambao umejengwa na CCM. Silaha tuliyonayo katika mapambano haya ni kura zetu, na fursa pekee tuliyonayo ni chaguzi zinazojitokeza sasa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Tuzitumie chaguzi zinazojitokeza sasa kama fursa ya kuimarisha mapambano yetu dhidi ya ufisadi wakati tukijiandaa kufanya mabadiliko makubwa ya kisiasa ifikapo uchaguzi wa mwaka 2010.
Tuna bahati mbili kubwa ambazo Mungu ametupa katika vita yetu dhidi ya ufisadi na uporaji wa rasilimali za nchi yetu. Kwanza, tunao majemedari ambao Mungu amewapa ujasiri wa ajabu wa kusimama kidete dhidi ya nguvu kubwa za ufisadi. Hawa ni wabunge wa upinzani. Pamoja na uchache wao, wametuonyesha kwamba majimbo yao ni wananchi na nchi wakati wenzao wa CCM, kwa matendo yao bungeni ya kutetea na kuhalalisha ufisadi, wamejionyesha wazi kabisa kuwa majimbo yao ni chama chao.
Bahati ya pili ambayo pia Mungu ametupa ni ukweli kwamba, katika wiki chache zijazo kutafanyika uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kiteto. Hii ni fursa muhimu waliyoipata wenzetu wa Kiteto ya kutuanzishia safari yetu ya mabadiliko katika uongozi wa kisiasa ambayo, kama tulivyokwishaona hapa, ndio njia ya uhakika na endelevu ya kuvunja nguvu za mtandao wa ufisadi nchini.
Kwa hiyo, nitumie fursa hii niwaombe wana-Kiteto watuanzishie safari yetu ya mabadiliko kwa kutuchagulia mbunge kutoka kambi ya upinzani katika jimbo hili. Kusema kweli wana-Kiteto wana hiari ya kuchagua kati ya kuimarisha mapambano dhidi ya ufisadi kwa kumchagua mbunge wa upinzani au kudhoofisha nguvu ya upinzani bungeni na hivyo kufifisha mapambano dhidi ya ufisadi kwa kumchagua tena mbunge wa CCM. Ni matumaini yangu kuwa wana-Kiteto hawatawaangusha Watanzania wenzao kwa kuhakikisha kuwa wanamchagua mbunge wa upinzani ili kuimarisha jeshi la kupambana na ufisadi katika Bunge letu la Jamhuri ya Muungano. Sote tunawaombea Mungu awape ujasiri na hekima ili siku ya uchaguzi watuongezee askari katika jeshi la kupambana na ufisadi kupitia bunge letu.
Kwa maoni na mchango niandikie:
kitilam@yahoo.com
au nitumie ujumbe: +44 7904 237 414.
http://www.freemedia.co.tz/daima/2008/1/30/makala1.php