Alichokifanya Nyerere baada ya uhuru Kilichofuata baada ya kupatikana uhuru ilikuwa ni kukamatwa, kuwekwa kizuizini na kuhamishwa kwa masheikh na Waislamu wengine waliodhaniwa kuwa wanapinga utawala wa Nyerere.
Mashuhuri miongoni mwao walikuwa: Abdillah Schneider Plantan, Sheikh Abdulkarim Abdulwahid, Maalim Popo Saleh, Suleiman Masudi Mnonji, Ali Migeyo, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Sharff Hussein Badawiy, Shariff Mwinyibaba na Shariff Adnan
Wengine ni Bilali Rehani Waikela, Sheikh Jumanne Bias, Maalim Matar, Abdalah Mwamba, Sheikh Hashim Haji Abdallah, Sheikh Nurdin Hussein, Salum Abdallah Popo, Sheikh Mzee Ali Comoriam, Sheikh Al Amin Maftah, Rajab Kiguu cha Mbuzi na wengine wengi.
Lakini ukweli ulikuwa kwamba si wote katika wale waliokamatwa na kuwekwa kizuizini walijihusisha na siasa. Baadhi yao walikamatwa kwa sababu tu walikuwa wakishirikiana na wale waliodhaniwa ni wapinzani wa Nyerere.
Maalim Matar na Shariff Adnan walifungwa jela kwa sababu tu walihusika na msikiti wa Badawiy mjini Dar es Salaam ambako Sheikh Hassan bin Amir, wakati huo akichukuliwa kuwa ndiyo roho ya waumini wa Tanganyika, alikuwa ikiendesha madrasa yake kila magharibi pale msikitini.
Shariff Hussein na nduguye Mwinyibaba walihamishiwa Kenya, walikotoka si kwa sababu walikuwa wamejishughulisha katika harakati za kuipinga serikali, ila lakini kwa sababu walikuwa waangalizi wa msikiti wa Badawiy.
Sheikh Mzee Ali Comorian alitiwa kizuizini kwa sababu kila mara alikuwa akifuatana na Sheikh Hassan bin Amir kama vile alikuwa kivuli cha sheikh. Huenda kile kilichomfanya Nyerere kuwatia kizuizini masheikh na wengine kuhamishwa ni kufuata ule msemo wa Biblia usemao, 'yule ambae hayuko nasi basi ni dhidi yetu'.
Jinsi siasa na za Tanzania zilivyobadilika na jinsi Nyerere alivyoanza kuonesha uadui dhidi ya Waislamu kulimsikitisha sana Abdulwahid. Alishindwa kuelewa uhasama huu ulikuwa unatoka wapi. Alihisi kuwa anahusika na yale yaliyokuwa yanawapata Waislamu. Mawazo haya yalimzonga kama jinamizi. Kwa ufahamu wake alikuwa akidhani matatizo yote ya udini walikuwa wameyashinda toka miaka ya 1950. Mwaka 1953 Abdulwahid akiwa Muislamu na akiungwa mkono na Al Jamiatul Islamiyya aligombea kiti cha urais wa TAA na Nyerere, Mkatoliki.
Abdulwahid alishindwa uchaguzi ule. Waislamu hawakuuchukulia uchaguzi ule kama uchaguzi kati ya Muislamu na Mkristo. Kilichotazamwa ni uwezo wa wagombea.
Nyerere alikuwa amemzidi Abdulwahid na kwa ajili hii alichaguliwa kuiongoza TAA. Abdulwahid alikumbuka ugomvi wa Sheikh Suleiman Takadir wakati ule Mwenyekiti wa Baraza La Wazee wa TANU. Sheikh Takadir aliwaonya Waislamu wachukue tahadhari kwani Nyerere atakuja kuwapendelea Wakristo wenzake pale atakaposhika madaraka. Kama walivyofanya Waislamu wengi, Abdulwahid alimuunga mkono Nyerere na kumpinga Sheikh Takadir.
Wakati ule Abdulwahid aliamini kama Waislamu wengi walivyoamini kuwa Sheikh Takadir alikuwa anataka kuleta siasa za kibaguzi ambazo alikuwa anaziegemeza katika dini. Abdulwahid aliona udini aliokuwa anataka kuuleta Sheikh Takadir lilikuwa jambo ambalo lingeiletea hatari Tanganyika.
Abdulwahid alikufa mwaka 1968 wakati nchi ikiwa imegubikwa na hasama za chinichini kati ya Waislam dhidi ya serikali ya Nyerere ambae sasa alikuwa amehodhi madaraka yote katika serikali.
Umoja wa kitaifa, moja ya maadili ambayo yeye(Abdulwahid ) aliyapigania katika maisha yake yote katika siasa ulikuwa unahatarishwa. Halikadhalika umoja wa Waislamu ulikuwa unaelekea kuvunjika. Kulikuwepo na kuwekwa kizuizini kwa masheikh chini ya Preventive Dentation Act of 1962.
Baadhi ya masheikh waliotiwa gerezani walikuwa watu waliomuunga yeye mwenyewe mkono wakati anaunda TANU. Baadhi yao aliwashawishi kumuunga mkono Nyerere na TANU katika kile kipindi kigumu cha harakati za kudai uhuru. Mwanakamati wa Kamati Ndogo ya Siasa ya TAA, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, kiongozi wa ngazi ya juu kabisa kwa Waislamu alikuwa amekamatwa na kuondolewa nchini na kurudishwa kwao Zanzibar kwa amri ya Nyerere. Sababu iliyotolewa ya kukamatwa kwa Sheikh Hassan bin Amir ilikuwa alikuwa ati 'akipanga njama ya kupindua serikali'.
Sheikh Hassan bin Amir alikuwa kati ya Waislamu wachache ambao walithubutu kusimama kidete dhidi ya serikali na kutoa mawazo yake kuhusu jinsi serikali ilivyokuwa ikiwakandamiza Waislam. Kabla hajafa Abdulwahid alikuwa akifikiwa na habari kuwa Nyerere alikuwa alikuwa akiendesha kampeni makini sana ndani ya chama kuwafuta Waislamu ndani ya TANU.
Abdulwahid alikuwa anafahamu matokeo ya kuvunjika kwa umoja wa Waislam. Yeye alikuwa anajua vyema nguvu ya umoja wa Waislamu wakati walipokuwa wanapigania uhuru wa Tanganyika.
Abdulwahid halikadhalika alikuwa anafahamu nguvu ya wale waliokuwa nyuma na njama zile za kuwagawa Waislamu katika makundi hasimu. Vilevile alikuwa anatambua hofu na watu wote waliokuwa nyuma ya njama zile.
Alifahamu kuwa wale aliowapokea na kuwatia katika harakati za kudai uhuru sasa walikua na hofu na Uislam. Kama Uislamu ulitumika kuwaondoa wakoloni Uislam hautashindwa kuwatoa wao madarakani. Uislam ikiwa itkadi ya kupinga ukoloni sasa ilikuwa ni tishio kwa Ukristo katika Tanzania huru.
Kabla hajafariki dunia Abdulwahid alifanya mazungumzo na Nyerere. Mazungumzo haya baina ya Abdulwahid na Nyerere yalifanyika katika miezi ya mwisho ya mwaka 1968 wakati mashekhe na Waislamu mashuhuri wanasombwa na kutupwa gerezani. Abdulwahid na Nyerere walikuwa wametoka mbali. Watu hawa walikuwa marafiki wa zamani. Huenda kama isingelikuwa kwa msaada wa Abdulwahid historia ya TANU na ya Nyerere mwenyewe zingechukua mkondo tofauti.
Mazungumzo haya yalikuwa muhimu kwa Abdulwahid kwa sababu kwa kiasi fulani alihisi anahusika na yale yaliyokuwa yakiwasibu Waislamu, wale kutoka Dar es Salaam. Taarifa za Waislamu kukamatwa usiku na kuwekwa kizuizini zilikuwa zikimfikia karibu kila siku. Abdulwahid hakuweza kujifanya kuwa haathiriki na matokeo yale. Baadhi ya watu ambao Nyerere alikuwa anawatupa gerezani walikuwa watu ambao yeye Abdulwahid binafsi walimuunga mkono wakati anaanza siasa na watu ambao aliwashawishi wamkubali Nyerere wakati wa kuundwa TANU.
Abdulwahid alimwambia Nyerere huenda yeye akawa hana hisia wala uhusiano wowote na watu ambao yeye anatia sahihi wakamatwe na kutupwa gerezani. Lakini kwake yeye hao ni jamaa zake anaokutananao ama msikitini au mitaani. Yeye kama mtu anayeishi miongoni mwa Waislamu na zile familia zao alikuwa anaelewa majonzi yao.
Abdulwahid alimwambia Nyerere kwamba watu wale wanajua kuwa yeye, Abdulwahid ndiye aliyesamsaidia Nyerere wakati akiwa mgeni mjini Dar es Salaam, watu wakamjua na kumkubali na hivyo kuja kuweza kufika hapo alipofika.
Abdulwahid alimwambia Nyerere kuwa ndugu na jamaa za wafungwa wale wanamjia wakimbembeleza amsihi Nyerere awatoe ndugu zao jela. Abdulwahid alimwambia Nyerere kwamba kule kuwatia watu kizuizini ni uonevu kwa sababu wale watu hawana uwezo wa kupindua serikali yake.
Kwa sauti ya masikitiko Abdulwahid alimaliza maelezo yake kwa kumwambia Nyerere 'Naondoka hapa nikiwa nataka kuamini kuwa wewe Julius Nyerere, leo hujatugeuka.' Kwa maneno hayo Abdulwahid aliaga na kuondoka.
Alichosikia Nyerere kuhusu Abdulwahid baada ya maneno yale ilikuwa taarifa ya kifo chake jioni moja Jumamosi tarehe 12 Oktoba, 1968. Mkewe Mama Maria Nyerere, alizirai aliposikia habari zile za msiba. Alikuwa Abdulwahid ndiye aliyewapokea yeye na mume wake mara ya kwanza walipokuja Dar es Salaam.
ITAENDELEA....