Mohamed Said, hivi kweli mtu utakuwa sawa kichwani kama unaandika hivi...
Angalau leo umefunguka...
Bwana Sweke hiki kisa cha Sheikh Suleiman Takadir na Julius Nyerere hata TANU wakikiogopa
kukikhadithia.
Nakiweka hapa kwa faida ya wanaukumbi ili wajue tulikotoka:
''Baada ya kurejea kutoka Tabora, Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi Mohamed, Elias Kassenge na Bhoke Munanka walifuatana na Nyerere kwenye ziara ya Jimbo la Mashariki kuwaeleza watu umuhimu na maana halisi ya uchaguzi uliokuwa mbele yao.
Nyerere aliwafafanulia watu kile ambacho Waafrika wangepoteza endapo TANU ingesusia uchaguzi.
Lakini Sheikh Takadir alikuwa akishiriki katika mikutano ile kimwili tu; moyo na fikra zake havikuwa pale. Alikuwa na wasiwasi jinsi matukio yalivyokuwa yakitokea katika TANU na namna siasa ilivyokuwa ikichukua mwelekeo mpya.
Sheikh Takadir alikuwa anautazama kwa hofu uongozi wa Wakristo katika TANU ambao ulikuwa ukielekea kuchukua uongozi baada kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria.
Kwa sababu ya yale masharti magumu ya uchaguzi, TANU ilibidi itazame nje ya uongozi wake ili kupata wagombea uchaguzi wenye sifa zilizohitajika kugombea uchaguzi dhidi ya UTP.
TANU iliwachagua Julius Nyerere, Chief Abdallah Said Fundikira, John Ketto, Nesmo Eliufoo, John Mwakangale, Lawi Sijaona, Paul Bomani na George Kahama kusimama kama wagombea wa TANU. [1]
Baadhi ya hawa walikuwa watu ambao hawakuinukia katika TANU au harakati za siasa. Sheikh Takadir alihofu kuwa hawa Wakristo walioelimishwa na wamisionari na ukuzingatia kuwa walikuwa watu wapya katika harakati, mara watakaposhika madaraka watafanya juhudi kudumisha hali ile ile ya ukoloni, wakiwa hawana dhima ya kuongoza harakati kufikia lengo lake lake lililokusudiwa.
Sheikh Takadir alikuwa kiongozi wa kwanza katika TANU kuwatanabaisha Waislam kuhusu hatari hii mpya iliyokuwa ikiwabili.
Sheikh Haidar Mwinyimvua, mjumbe wa Baraza la Wazee wa TANU na mjumbe wa Kamati Kuu ya TANU katika mwaka 1958 na aliyekuwa rafiki mkubwa wa Sheikh Suleiman Takadir, anakumbuka jinsi Sheikh Takadir ghafla alipotoa dukuduku lake kwa Nyerere, dukuduku ambalo lilionekana lilikuwa halina sababu:
''Ilikuwa katika ofisi ya zamani ya TANU tukisubiri kufanya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa.
Ghafla tu Sheikh Takadir alisimama wima akishikilia fimbo yake ya kutembea akimuelekezea Nyerere huku akisema, ''Huyu mtu katu hatakuja kutujali sisi atakuja kuwajali ndugu zake. Usipoziba ufa utajenga ukuta''
Sheikh Takadir alirudia maneno haya mara mbili. Sisi sote katika kile chumba cha mkutano tulipigwa na butwaa kutokana na maneno yale.
Nilimwona Nyerere akilia.
Nyerere alitugeukia sisi na kutuuliza, ''Je, Sheikh Suleiman amesema maneno yale kwa niaba yenu?''
Tulijibu kwa pamoja kuwa hatukuwa na habari kuhusu shauri lile; na mkutano ukavunjika hapo hapo.
Sheikh Takadir alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa kumuunga mkono Nyerere na alikuwa ameifanyia kampeni TANU kwa bidii kubwa, akihutubia mikutano jukwaa moja na Nyerere.
Halikadhalika alikuwa amesaidia kufutilia mbali Ukristo wa Nyerere kwa watu wa Dar es Salaam kiasi kwamba watu mjini Dar es Salaam hawakumnasibisha Nyerere na Kanisa Katoliki ila na TANU kama chama cha wananchi.
Wadhifa wa Sheikh Takadir mwenyewe kama mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU ulikuwa wa heshima kubwa.
Haikuwa kwamba wale wote waliokuwemo ndani ya chumba kile hawakuelewa kile alichodokeza Sheikh Takadir.
Walielewa kila neno alilotamka na maana yake halisi hasa kwa uongozi wa TANU. Kile ambacho hawakufahamu, kutambua au kusadiki kilikuwa ule ukweli kuwa Nyerere, mtoto wao mpendwa na kiongozi wao, iko siku moja atawageuka Waislam na kuwatazama kama adui zake na mahasimu kwa imani yake ya Kikristo.
Lakini kwa wakati ule hili lilikuwa wazo lililokuwa mbali sana na lisilokuwa na maana yeyote kwao.
TANU na chama kilichotangulia, African Association, hazikuundwa kwa ajili ya masilahi ya kikundi fulani pamoja na ukweli kuwa Waislam ndiyo waliounda vyama hivyo viwili na kuviongoza.
Sheikh Takadir alikuwa ametonesha jambo nyeti sana. Njia pekee ya kuzuia mgogoro huu mpya usikue ilikuwa kwa Nyerere kuthibitisha kuwa Waislam watatendewa haki baada ya uhuru kupatikana.
Kwa wakati ule, umoja wa wananachi ulikuwa muhimu kwa ajili ya harakati.
Umoja wa Watanganyika ukawa ndiyo hoja kuu ya Nyerere katika hotuba zake zote kuanzia mkasa wa Takadir utokee na alishikilia hoja ya umoja katika kila hotuba yake hadi kufikia uchaguzi wa kura tatu.
Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU iliamua kuunda kamati ya haraka haraka kwenda nyumbani kwa Sheikh Takadir Mtaa wa Msimbazi kumuuliza kwa nini alimshutumu Nyerere. Miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo walikuwa Idd Faiz, Mwenyekiti wa Halmashauri ya TANU, Idd Tulio na Jumbe Tambaza.
Sheikh Takadir aliiambia kamati hiyo kuwa Nyerere alikuwa akitumia sharti la elimu katika uchaguzi wa kura tatu ili kuwaweka Wakristo wenzake madarakani kwa hoja kwamba wanazo zile sifa zitakiwazo kushika majukumu ya serikali.
Kisha Sheikh Takadir akarudia tena maneno yale yale aliyomwelezea Nyerere, neno kwa neno, akiongeza kwamba hana majuto yoyote kwa msimamo wake huo.
Wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Idd Tulio walisimama na kuondoka kimya kimya. Matokeo yake ikawa Sheikh Takadir kufukuzwa kutoka TANU kwa kuanzisha suala la udini, ambalo lilidhaniwa lingewagawa wananchi.
Idd Tulio akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU kushika nafasi ya Sheikh Takadir.
Idd Tulio alikuwa kati ya watu waliohudhuria mkutano wa kwanza wa TANU pale Ukumbi wa Arnatouglo.
Kuingizwa kwa watu kama Eliofoo, Mwakangale, Sijaona, Bomani, Kahama na wengine katika Baraza la Kutunga Sheria ili kuwakilisha TANU kuliwatia wasiwasi idadi kubwa ya wanachama Waislam waliokuwepo makao makuu ya TANU.
Lakini kwa hakika viongozi hawa walikuwa wazalendo wakiwakilisha sehemu muhimu nchini Tanganyika ambazo kwa mfano wale kutoka vyama vya ushirika kama Bomani kutoka Jimbo la Ziwa, walijitoa mhanga sana katika harakati.
Hakuna namna ambayo Nyerere angeweza kuwakwepa kwa hofu ya kuujaza uongozi katika TANU na Baraza la Kutunga Sheria na Wakristo.
Kwa upande mwingnine halikadhalika haikufikiriwa kuwa ni lazima kuwa na uwakilishi ulio sawasawa baina ya Waislam na Wakristo katika TANU au katika Baraza la Kutunga Sheria.
Wakati ule tatizo la udini lilikuwa halijulikani kabisa.''
(Kutoka ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes...'')