Yericko,
Kuna mashujaa wengine hujapata kuwasikia.
Hebu soma hapa chini kisha tuendelee na darsa:
''Jina la huyu mzee wangu ni Mohamed Omar Mkwawa.
Ilikuwa katika barza yetu ya kawaida ya kunywa kahawa na kula pweza huku tukijadili historia ya Tanzania ambako siku moja Mzee Mkwawa alinambia, Mohamed nataka nikuambie kitu. Unajua mimi nimehusika sana katika mapinduzi ya Zanzibar?
Nilimuangalia Mzee Mkwawa kwa makini. Fikra yangu ya utafiti na uandishi ishashtuka haipo tena usingizini. Mzee Mkwawa aliendelea, Mimi ndiye niliyekuwa nikiwavusha Wamakonde kutoka Kipumbwi kwenda Zanzibar kuipigia kura ASP na wakati wa mapinduzi mie ndiye niliyewavusha Wamakonde kwenda kuipindua serikali ya Jamshid.
Sasa moyo wangu ukaanza kudunda kwa nguvu. Naisemesha nafsi yangu, Huyu mzee anajua uzito wa maneno haya? Tuishie hapa.
Kuanzia siku ile nikawa sasa namtazama Mzee Mkwawa kwa jicho jingine na heshima yangu kwake ikawa imepanda maradufu. Nilikuwa nimeshatambua kuwa Mzee Mohamed Omari Mkwawa alikuwa mmoja wa wanahistoria waliosahaulika katika historia ya Tanganyika na Zanzibar...
Yericko,
Tuendelee na darsa letu la historia ya mapinduzi ya Zanzibar na nakuomba uangalie wapi utampachika ''Field Marshal Okello'' katika nyavu hizi abaki salama bila ya kujifungafunga:
Kitu kimoja mashuhuri kwa mashujaa wa harakati za siasa katika Tanzania ni kuwa takriban wote wana hali ngumu sana za maisha. Sikujua vyema hali ya Mzee Mkwawa hadi nilipofika nyumbani kwake na Dkt Ghassany.
Utu uzima na udhaifu wa maisha ulikuwa umempiga barabara. Nilimjulisha Dkt Ghassany kwa Mzee Mkwawa na kuwaacha waendelee na maongezi yao. Niliporudi mchana kumchukua Dkt Ghassany rafiki yangu alinambia nimuache nije jioni kumfuata. Niliporudi jioni nilimkuta Dkt Ghassany amechoka na uso umesawijika.
Tukiwa ndani ya gari yangu tunaondoka nikamuuliza kulikoni. Dkt Ghassany akanambia maneno ambayo hadi leo yamebaki kichwani mwangu,Mohamed ufunguo wa kitabu changu anao Mzee Mkwakwa na kama nisingeonana nae utafiti wangu wote wa kabla ungelikuwa hauna maana yoyote.
Dkt Ghassany alikuwa amechukuliwa na Mzee Mkwawa katika safari ya zaidi ya nusu karne. Mzee Mkwawa akimshika mkono kwanza kumpeleka Pemba ambako akiwa kijana wa kiasi cha miaka 25 akifanya kazi ya uashi. Huo ndio ulikuwa wakati wa siasa za ASP na Hizbu zimepamba moto.
Mzee Mkwawa alikuwa mmoja wa wachezaji wa ngoma ile hata kama alikuwa anatoka Tanganyika. Dkt Harith akavushwa na kuletwa pwani ya Kipumbwi na Sakura ambako Mzee Mkwawa alikuwa akisimamia kambi ya mafunzo iliyokuwa msituni ya wakata mkonge wengi wao wakiwa Wamakonde, kambi ambayo ilitoa askari waliotumika kuipindua serikali ya Mohamed Shamte 12 Aprili 1964.
Dkt Ghassany hakuwa amejitayarisha kwa haya. Alishangwazwa na uwezo wa kumbukumbu wa Mzee Mkwawa, akitaja majina na mahali na akirudia mazungumzo neno kwa neno kati yake na maofisa wa serikali ya Tanganyika kutoka vyombo vya usalama waliomtia katika operesheni maalum ya kuipindua Zanzibar kutoka Tanganyika.
Majina ya Abdulla Kassim Hanga, Jumanne Abdallah, Ali Mwinyi Tambwe, Victor Mkello, Oscar Kambona na wengine yakawa yanadondoka moja baada ya lingine. Taarifa hizi ndizo zilizommaliza Dkt Ghassany na kumsawajisha uso.
Mimi binafsi nilipigwa na butwaa. Nilibaini kama alivyobaini Dkt Ghassany kuwa Mzee Mkwawa alikuwa hazina na tulikuwa tumevumbua mgodi wa dhahabu. Kazi yetu sasa ilikuwa kuchimba tu. Kumekuwa na uvumi kwa miaka mingi katika duru za wanasiasa wapya na wa zamani na katika wanafunzi wa historia ya Tanzania na Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Ali Mwinyi Tambwe alihusika sana katika kupinduliwa kwa serikali ya Zanzibar lakini hakuna aliyejuwa ni kwa kiwango gani na alihusika vipi.
Lakini zito ni kuwa yeye mwenyewe akiudhika sana mtu akimuuliza habari zile. Kwa nini ilikuwa hivyo? Kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru cha Dkt Ghassany kilikuja kutoa majibu. Hakuna binadamu apendae historia yake ihusishwe na mauaji na dhulma na kufutwa kwa nchi yake.
Kwa kipindi cha takriban miaka saba Dkt Ghassany alikuwa akija Tanga kwa mahojiano na Mzee Mkwawa na katika kipindi hicho Mzee Mkwawa alitupeleka Kipumbwi na Sakura na kutuonyesha sehemu zile ambazo walikuwa na kambi na wakifanya mazoezi ya kivita na matumizi ya silaha.
Mkahawa ambao wale wakata mkonge walikuwa wakila chakula cha usiku kabla ya kuvushwa kwa vyombo vya bahari kwenda Unguja bado upo hadi leo ingawa kwa sasa kijumba kile hakitumiki tena kama mkawaha. Endapo itakuja siku serikali ya Zanzibar itataka kuhifadhi historia ya Mapinduzi ya Zanzibar bila shaka moja ya vitu vitakavyokuwa katika makumbusho ni picha ya hicho kibanda.''