Kila binadamu ana historia yake.mHistoria hiyo yaweza kuwa mbaya au nzuri. Hata hivyo jambo moja ni kweli juu ya historia, kuwa historia imepita na hatuwezi kubadilisha kilichohistoria. Jambo la kweli ni kwamba tunaweza leo tukasimamia katika ukweli ili tuwe na historia nzuri miaka 50 au 100 ijayo. Nimshukuru
Mohamed Said kwa maelekezo ya kitabu. Nitakisoma.
Pamoja na hayo, nina mambo machache ninayotaka kusema hapa.
1. Ukiangalia kwa kina mtiririko wa mada hapa, utagundua kuwa haswa haswa ni kati ya Uislamu na Ukristo. Kwamba Nyerere alifanya jitahada za makusudi, si tuu kutowatambua wiaslamu waliopigania uhuru, bali pia kuwakandamiza waislamu katika maendeleo. Wapo ambao hawataki kutamka kuwa Nyerere ni baba wa Taifa na wengine wanamtamka kwa kejeli. Vyovyote vile iwavyo, hili halimwongezei wala kumpunguzia kitu Nyerere na ukweli unabaki kuwa amekuwa raisi wa kwanza wa Tanzania, na dunia imemtambua kuwa alikuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru wetu.
2.Kuhusu malalamiko ya waislamu wa muda mrefu sidhani kwamba Nyerere anapaswa kubeba mzigo huo pekee. Pia hawezi kukwepa kabisa maana amekuwa raisi wa kwanza kwa miaka zaidi ya 20. Sababu za kwanini waislamu wanaona wapo nyuma ni nyingi na nyingine zimechangiwa na waislamu wenyewe.
Hebu tazama waislamu wa Moshi/Arusha na wale wa mkoa wa Lindi! Kwanini maendeleo yao ni tofauti ingawa wote ni waislamu? Kwanini fursa zao kuendelea ni kubwa kwa baadhi ya maeneo na maeneo mengine ni ndogo?
3.Matatizo ya waislamu hayatatatuliwa kwa waislamu kusema 'ni wakati wetu sasa'. Kwamba 'wametukandamiza' vya kutosha. Hayawezi pia kutatuliwa kwa vikao vya wakristo na waislamu. Wala serikali haiwezi kutatua matatizo ya waislamu. Nionavyo mimi, suluhu ipo kwa waislamu wenyewe. Kwanza katika umoja wao watambue nini vipaumbele vyao. Waanze kuvitekeleza halafu tuone serikali gani itawazuia na kwasababu gani. Lawama hizi hazitawapelekea popote. Mimi nimetembea Kigoma, Tabora, Morogoro, Pwani, Lindi, Kilimanjaro nk. Nimeona misikiti mikubwa sana katika vijiji ambavyo maisha ya watu wake ni duni. Sasa nikajiuliza, kama upo uwezo wa kujenga haya, kwanini wasiende hatua moja zaidi kuhusu shule, zahanati, vyuo nk nk? Jukumu la serikali libakie kuwa ni kutoa fursa sawa, yaani ardhi, ruzuku, rasilimali watu nk nk
4. Upo mkakati wa kusema sasa raisi awe Mwisalmu. Kama kweli tunataka maendeleo lazima tuwaze zaidi ya hapa. Tumekuwa na maraisi wawili waislamu. Na tumeona Kikwete aliwekwa kimkakati (Hata Lipumba amekiri hilo). Na kwakweli amefanya mengi katika hayo. Bado sisi tumekuwa wakwanza kulalamikia mfumo Kristo! Kumbe kuwa na raisi mwislamu na mawaziri wote, na hata wakuu wa mikoa bado inaweza isisitatue matatizo yetu. Zipo nchi zinazoongozwa na dola ya kiislamu lakini bado malalamiko yapo kila kukicha.Tunahitaji kama taifa kuwaza beyond our religions.
5.Nimeangalia mafundisho ya baadhi ya mashekhe na hata baadhi ya michango ya watu hapa, utaona chuki ya wazi dhidi ya watu wa dini mbili hizi. Sioni kama chuki itatusaidia. Wapo ambao wamehoji kwanini baadhi ya waislamu walishirikiana na makafiri! Kwa chuki hizi,matatizo yetu hayaishi. Wengi hapa ni wasomi. Hivi kweli ukinichukia mimi kama Mkristo ndio unapataje maendeleo?
Ndio maana nasema maendeleo ya waislamu yatapatikana kama waislamu wenyewe watakaa, wakaainisha vipaumbele vyao na wakaanza kuvifanyia kazi. Serikali ifanye kazi ya promoter! Na maendeleo ya waislamu na wakristo yataonekana wazi kama Tanzania kwa ujumla wake itaendelea. Tukijiangalia kwa jicho la Uislamu na Ukristo, mwaka 2061 na hata 3011 tutakuwa bado tunazungumzia jambo hili, na pengine katika hali mbaya zaidi.
Inawezekana nimetoka nje ya mada, lakini nadhani ni vyema tushauri pia nini kifanyike ili baadae tuwe na historia sahihi ya nchi yetu. Mahali nimekosea naomba nisahihishwe, maana mimi ni kijana bado na pengine nimetawaliwa na hoja mufilisi!