A
Anonymous
Guest
Tunashukuru uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kufika katika Kituo cha Afya Fumagila wiki iliyopita na kutoa maagizo kuhusu changamoto zilizokuwa zikilalamikiwa, hususan suala la utoaji na upokeaji wa fedha kwa wagonjwa.
Hata hivyo, baada ya viongozi hao kuondoka, hali inaonekana kurejea katika utaratibu uliokuwa ukilalamikiwa.
Pia soma ~ Kituo cha Afya Fumagila - Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wajawazito wanalipishwa, hawalipi kwa Control Number
Kwa mujibu wa malalamiko haya, katibu wa kituo anaendelea kupokea baadhi ya fedha mkononi badala ya wagonjwa wote kufuata utaratibu rasmi wa malipo. Baadhi ya wagonjwa wanapewa control number, huku wengine wakitozwa fedha taslimu na kisha kupewa muhuri unaosomeka “PAID” kama uthibitisho wa malipo.
Kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba, baadhi ya wanaolipishwa ni wajawazito, ambao wanadai wanapaswa kupata huduma zinazohusiana na uzazi bila kutozwa fedha. Hali hii inazua maswali kuhusu utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na uongozi wa Halmashauri pamoja na utaratibu unaotumika katika kupokea na kurekodi fedha zinazolipwa na wagonjwa.
Tunaomba uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza na mamlaka husika wafuatilie suala hili kwa karibu, ikiwa ni pamoja na kuchunguza madai ya malipo ya fedha taslimu, matumizi ya muhuri wa “PAID” na malipo yanayodaiwa kufanywa na wajawazito. Wananchi tunahitaji huduma za afya zinazofuata taratibu rasmi na uwazi katika kila malipo yanayofanyika kituoni.