Pinda aagiza waliohujumu UDA wachunguzwe
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewaagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa kina wa madai ya wizi katika Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA). Katika agizo hilo, Pinda amesema, baada ya uchunguzi huo, watakaobainika kulihujumu shirika hilo wawajibishwe mara moja.
Akitoa ufafanuzi bungeni jana, Pinda alisema kanuni ya 38(4) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, inaruhusu kutolewa kwa ufafanuzi kwa jambo linalojadiliwa bungeni lenye umuhimu na maslahi makubwa kwa umma. "Serikali imesikia kilio cha wabunge, kwa sasa tumeviagiza vyombo hivyo kufanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha taarifa serikalini mapema iwezekanavyo, alisema Pinda na kuongeza: "Baada ya uchunguzi huo, tutachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu kwa watakaobainika kulihujumu shirika hili," alisema Pinda.
UDA inasemekana kuuzwa isivyo halali na watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, akiwamo Meya wa Jiji hilo, Didas Masaburi, Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, Idd Simba. Wengine wanaohusishwa na kashfa hiyo ni Mkurugenzi wa Jiji, Bakari Kingobi, Meneja Mkuu wa UDA, Victor Milanzi na viongozi wengine akiwamo Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya, ambaye ilielezwa ana hisa 10,000 kwenye kampuni ya Simon Group inayodaiwa kununua UDA isivyo halali.
Katika hatua nyingine, wabunge wa mkoa wa Dar es Salaam na wadau wa mkoa huo, walitoa tamko la kusikitishwa na tuhuma za ufisadi na ukiukwaji wa taratibu kwenye shirika hilo na kusema wako tayari kutoa ushahidi kwa vyombo vilivyopewa kazi ya kuchunguza kadhia hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini hapa, Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa huo, Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu (CCM), alisema pamoja na Serikali kuagiza uchunguzi wa suala hilo, wabunge hao wanaomba pia isitishe mara moja mkataba batili wa ununuzi wa UDA. "Tumekubaliana sisi wabunge wote wa Dar es Salaam, tuko tayari kutoa ushahidi kwenye vyombo hivyo, pamoja na kushirikiana na Serikali kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa, ili kulinda mali za umma," alisema Mtemvu.
Alisema uamuzi wote uliofanywa na Meya Masaburi ambao unataja kuridhiwa na vikao vya Jiji ni batili kwa kuwa ulifikiwa na vikao visivyo halali. Aliongeza kwamba uamuzi huo pia ulifanywa bila kuheshimu maelekezo ya barua ya ofisi ya Waziri Mkuu ya Februari 28 mwaka jana, ikiagiza kusitishwa mara moja kwa mchakato wa kuuza hisa ambazo hazijagawiwa. Aliongeza kuwa vikao hivyo vya kamati ya uongozi na Baraza la Madiwani viliitishwa kinyemela wakati wabunge wakihudhuria mkutano wa Bunge la Bajeti mjini hapa, hivyo wabunge wa mkoa huo kutoshirikishwa.
Alisema mikutano maalumu ambayo ni batili, iliitishwa kuhalalisha uamuzi haramu wa Masaburi kwa kikao cha Kamati ya Fedha na uongozi cha Juni 29 na cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji Julai 20. Mtemvu alitoa mwito kwa wakazi wa Jiji hilo kuwaunga mkono wabunge hao ili kuhakikisha mali za umma zinasimamiwa kikamilifu na watakaobainika wamehujumu UDA, wachukuliwe hatua za kisheria.
HabariLeo | Pinda aagiza waliohujumu UDA wachunguzwe