KERO UDART mnawaza nini? Abiria tunateseka na kuingia hasara kwa kusubiria Mwendokasi muda mrefu

KERO UDART mnawaza nini? Abiria tunateseka na kuingia hasara kwa kusubiria Mwendokasi muda mrefu

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) inayotoa huduma za usafiri wa umma kupitia barabara ya Morogoro Road, kuanzia Mbezi Luis na kituo kikuu cha Kimara kuelekea maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, ikiwemo Kariakoo (Gerezani) na Kivukoni, imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kuchelewa kwa mabasi, hali inayowalazimu abiria kukaa vituoni kwa muda mrefu.

Licha ya taarifa zilizotolewa kuwa UDART iliongeza mabasi mapya 49 mnamo Januari 2026 kwa lengo la kupunguza adha ya usafiri katika njia ya Kimara, hali ya usafiri bado ni tete, hususan nyakati za asubuhi na jioni.

Kwa mfano, katika eneo la Kimara, huduma ya usafiri imekuwa changamoto kubwa. Abiria tunajazana vituoni na kusubiri kwa zaidi ya saa moja bila basi kufika kwa ajili ya kutupakia. Hali hii inasababisha usumbufu mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa muda mwingi tunaoutumia vituoni tunakuwa tumesimama tukisubiri usafiri.

Changamoto hiyo inajitokeza pia katika vituo vya Mbezi Luis na Magufuli Bus Terminal. Abiria hukata tiketi, lakini mabasi huchelewa kufika vituoni. Matokeo yake, baadhi ya abiria hulazimika kuacha kutumia huduma hiyo na kupata hasara ya fedha walizolipia tiketi, huku wakilazimika kutafuta usafiri mwingine ili kuwahi kazini.

Katika njia hizi, idadi ya abiria inaendelea kuongezeka, huku mahitaji ya usafiri kuelekea katikati ya jiji na kutoka nje ya jiji yakiwa makubwa. Katika mazingira kama haya, ilitarajiwa kuwa huduma ya mabasi yaendayo haraka ingekuwa suluhisho muhimu katika kurahisisha usafiri kwa wananchi. Hata hivyo, kwa sasa, huduma hiyo imekuwa kero na chanzo cha sintofahamu kwa abiria.

Tuliahidiwa kuwa mabasi yangeongezwa zaidi ili kurahisisha usafiri, lakini ahadi hiyo inaonekana kutotekelezwa ipasavyo. DART imekabidhiwa jukumu la kusimamia eneo kubwa la utoaji huduma, lakini kwa hali inavyoonekana, UDART imeshindwa kumudu mahitaji ya usafiri katika maeneo inayohudumia. Wakati wananchi tukiendelea kuwa na matumaini ya kupata huduma bora, hali inazidi kuwa mbaya na malalamiko yanaongezeka.

Wito wangu kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na mamlaka nyingine zinazohusika kufuatilia changamoto hii na kufanya tathmini ya haraka kuhusu ufanisi wa huduma zinazotolewa na UDART. Tathmini hiyo itasaidia kubaini uhitaji halisi wa kuongeza mabasi pamoja na kuboresha ufanisi wa huduma nyingine zinazohusiana na usafiri huo.

Iwapo itabainika kuwa UDART haina uwezo wa kukidhi mahitaji ya usafiri katika maeneo inayohudumia kwa sasa, basi utaratibu ufanyike wa kuruhusu wawekezaji wengine kuingia katika sekta hiyo ili kuongeza uwezo wa utoaji huduma na ushindani. Hatua hiyo inaweza kusaidia kurahisisha usafiri kwa wananchi, kuboresha huduma na kupunguza kero zinazowakabili abiria, hususan kusubiri mabasi kwa muda mrefu vituoni.
 
Zile za mbagala ziko vizuri sanaaa MOFAT hana utani
 
Back
Top Bottom