Kuua, kuhamasisha watu kuuawa, kutishia kuua au kushiriki kwa namna yoyote ile katika mauaji ni makosa ya jinai. Polisi hawastahili kusubiri kuambiwa wamkamate na kumfikisha mahakamani mtu anayefanya makosa haya.
Kwa uwazi kabisa, Musiba, tena kwenye TV na kwa kupitia magazeti yake alisikika wazi akihamasisha baadhi ya watu kama Tundu Lisu kuuawa, alisikika wazi akiwatukana watu kama Zito kuwa walikuwa wanagombania shoga. Kauli hizo zilisikika wazi kabisa, na kwa uhakika hakuna kiongozi wa Polisi ambaye hakumsikia.
Lakini kati ya aliowataja, mtu kama Lisu aliishia kupigwa risasi. Lakini wapo ambao mpaka leo wamepotezwa au kuuawa. Tuna uhakika gani kuwa hao walioshambuliwa kwa lengo la kuwaua, au waliopotezwa au waliouawa, hawakuafanyiwa hayo yote kwa kuhamasishwa na kauli za watu waovu kama Musiba? Au pengine hata Musiba mwenyewe kushiriki?
Kazi ya polisi ni pamoja na kuchunguza matukio yote yenye viashiaria vya uhalifu, na kisha kama kuna uhalifu uliothibitika, ni mhusika kufikishwa mahakamani. Kwa nini hilo halikufanyika dhidi ya Musiba? Au jeshi la Polisi ili kufanya kazi ni lazima liamriwe na viongozi wa kisiasa ambao siyo Polisi, ndiyo lifanye kazi? Huu ni udhaifu mkubwa sana kwa Jeshi la Polisi.
Shukrani nyingi sana kwa Mh. Membe kwa kuchukua hatua dhidi ya muovu huyu (mahakama imethibitisha). Nadhani Membe aliamua kuchukua hatua ya kumshtaki Musiba baada ya kuona Jeshi la Polisi limeshindwa kufanya kazi yake.
Na kwa vile mtu binafsi hawezi kumfungulia mhalifu wa makosa ya jinai kwa shtaka la jinai, aliamua kufungua kesi ya kuvunjiwa heshima. Na mahakama ikatoa hukumu. Hukumu hii japo siyo ya kumpeleka mhalifu Musiba gerezani, lakini angalao inamfanya Musiba alipie uhalifu wake.
Mhalifu anapoadhibiwa, inapeleka ujumbe mpana kwa wahalifu wengine au wanaotegemea kuwa wahalifu. Hatutaki Musiba wengine, hivyo ni vema ujumbe huu uwafikie Musiba wengine kwa ukamilifu. Mhalifu mmoja anapoadhibiwa sawasawa, unawalinda Watanzania mamilioni walio wema.
Jambo la kusikitisha ni taarifa kuwa eti kuna viongozi wa dini wamekuwa wakitumwa na Musiba kwenda kwa Membe kutaka Musiba asiadhibiwe. Hilo linasikitisha sana. Na tungependa kuuliza, hawa viongozi wa dini wakati Musiba anahamasisha watu wengine wauawe, walikuwa wapi? Walitoa kauli gani?
Je, wamechunguza kauli hizo za Musiba zilisababisha watu wangapi wauawe, kutekwa au kupotezwa? Wanaupata wapi ujasiri wa kusimama na muovu mmoja dhidi ya familia, marafiki na ndugu wa wale ambao jamaa zao au waliuawa, walishambukiwa au kupotezwa?
Tunamshukuru sana Mh. Membe kwa kulisimamia hili. Manufaa ya hili ni mapana sana, hasa kwa vizazi vya sasa na vya mbeleni. Na utekelezaji wa hukumu hii uwekwe wazi sana, utangazwe ili watu wajue kuwa uovu huwa hausimami milele. Watu wajivunie wema na siyo uovu unaoweza kukupa mafanikio na umaarufu wa muda mfupi.