University of Dodoma (UDOM)
Public Institution
- Feb 24, 2024
- 50
- 55
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), leo Mei 25, 2026, kimetoa mafunzo ya ukusanyaji wa taarifa za msingi kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa SAFARI, unaotumia teknolojia ya Akili Unde (AI) kuboresha huduma za ultrasound kwa akina mama wajawazito.
Mradi huo unatekelezwa na UDOM kwa kushirikiana na Liverpool School of Tropical Medicine (LSTM), chini ya ufadhili wa Gates Foundation.
Mafunzo hayo yamewahusisha watoa huduma za afya kutoka vitengo vya afya ya mama na mtoto katika vituo 32 vya kutolea huduma za afya kutoka halmashauri zote 8 za Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo, Msaidizi Mkuu wa Mradi huo, Dkt. Maria Rweyemamu, amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watoa huduma za afya katika ukusanyaji wa taarifa sahihi na za ziada ili kubaini hali halisi ya upatikanaji wa huduma za ultrasound kwa wajawazito wakati wa kliniki.
Amesema taarifa hizo mara nyingi hazipatikani kwenye vitabu vya kawaida vya mahudhurio ya kila siku.
“Kwa mfano, tunataka kufahamu mama aliagizwa kufanya ultrasound lini, alienda lini kufanya kipimo hicho, majibu yalikuwa yapi, na kama hakufanya kipimo, sababu zilikuwa zipi,” aliongeza Dkt. Rweyemamu.
Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuupokea mradi huo kwa matumaini makubwa, wakisema kuwa mafunzo hayo yamewaongezea uelewa na kuwajengea uwezo wa ukusanyaji sahihi wa taarifa katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Aidha, hatua hiyo imeelezwa kuwa muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wenye mafanikio wa mradi huo, huku matumizi ya teknolojia ya Akili Unde (AI) katika huduma za ultrasound yakitarajiwa kuboresha kwa kiwango kikubwa huduma za afya ya mama na mtoto katika Mkoa wa Dodoma.