The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika moja ya ziara zake kurekodi The Royal Tour, 2021
Tumesikia na kuona Rais Samia akiwa katika kile kilichojulikana kama The Royal Tour, lakini huenda kuna baadhi yetu hatujaelewa ni kitu gani hiki.
Wapo wanaodhani Rais kajitungia jina na kutafuta wapiga picha kadhaa anaoambatana nao. La hasha!
Wapo waliopendekeza kwamba Rais angetumia watu wenye ushawishi nchini kufanya kazi hiyo - lakini je, inafaa kuwa hivyo? Hapana.
Wapo pia tuliodhani Royal Tour ni ile picha moja iliyobadilishiwa background mara nyingi na kusambazwa mtandaoni.
Royal Tour ni mfululizo wa vipindi vya televisheni vinavyorushwa na chaneli ya PBS (Public Broadcasting Service) huko nchini Marekani.
Mtayarishaji wa The Royal Tour ni nani?
The Royal Tour inazalishwa/tayarishwa na Peter Greenberg ambaye -- kwa mujibu wa vyanzo kadhaa -- ni mmoja wa waandishi wa habari wa musuala ya utalii wanaojulikana na kuheshimiwa zaidi nchini Marekani. Anajulikana katika tasnia ya utalii kama “The Travel Detective”.
Bw. Greenberg pia ni Mhariri wa Masuala ya Utalii wa kituo cha CBS News kwa sasa.
Maandiko yake yamechapishwa na Forbes.com, CBS.com, Oprah.com n.k. Pia amewahi kushirikishwa kama mgeni na vyombo vya habari na vipindi vikubwa kama vile CNN, The Oprah Winfrey Show, Late Night with Conan O'Brien, Larry King Live n.k
Peter Greenberg
The Royal Tour inafanyikaje?
Kipindi kinalenga kumhusisha mkuu wa nchi husika ambaye ndiye anakuwa mwenyeji au “tour guide” akionesha maeneo mbalimbali ya kuvutia kwa mgeni wake Peter Greenberg. The Royal Tour inatoa fursa ya kuonesha nchi na watu wake na kutoa uelewa bora - na wa kuaminika - juu ya utamaduni wake na watu kupitia uzoefu wa kiongozi wake. Well, ndiyo maana nikasema Rais hawezi kuwakilishwa na mtu maarufu ama kiongozi mwingine katika hili. Lengo kuu hapa ni Kiongozi Mkuu wa Taifa kushiriki na kumtembeza Bw. Greenberg maeneo ambayo ni muhimu na yenye kuvutia watalii pamoja na kujibu maswali anuai kuhusu nchi anayoiongoza. Je, Rais anajua zaidi ya kila mwananchi? Huenda hapana, lakini kwakuwa kipindi kinamlenga yeye, basi hana budi kushiriki katika nafasi hiyo.
Je, Rais Samia ni wa kwanza kushiriki The Royal Tour?
Hapana. The Royal Tour tayari imewashirikisha viongozi kadhaa duniani ikiwa ni pamoja na wafuatao:
- Helen Clark, aliyekuwa Waziri Mkuu wa New Zealand (1999 - 2008)
- Benjamin Netanyahu, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israeli (1996 – 1999/ 2009 – 2021)
- Mfalme Abdullah II wa Jordan (tangu 1999)
- Alejandro Toledo, aliyekuwa Rais wa Peru (2001 - 2006)
- Felipe Calderón, aliyekuwa Rais wa Mexico (2006 – 2012)
- Rais Paul Kagame wa Rwanda
- Mateusz Morawiecki, Waziri Mkuu wa sasa wa Poland (tangu 2017)
Peter Greenberg akiwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wakati wa kurekodi The Royal Tour, Jerusalem, 2014
Mafanikio yake kuwavutia watalii yapoje?
Kwa uchache tu ni kwamba, ingawa The Royal Tour imechukuliwa na baadhi ya watu kama jukwaa la PR Stunts za wakuu wanchi, lakini pia kumekuwapo “ripoti” za mafanikio, tofauti na zile zinazoonekana kulenga kubadili narrative kuhusu viongozi wa nchi na tawala zao.
Baada ya The Royal Tour iliyomshirikisha Mfalme Abdullah II kurushwa, “iliripotiwa” kuwa utalii ulipanda karibu asilimia 20 nchini Jordan, huku Mexico, Peru na Jamaica zikishuhudia ongezeko la 10%
Wizara ya Utalii ya Israeli pia ilisema kuwa baada ya filamu hiyo kuoneshwa, nchi hiyo ingepata ongezeko la watalii 200,000 zaidi. Hata hivyo, si kila mmoja alipendezwa na filamu hiyo nchini Israel. Lakini Greenberg alisisitiza kwamba filamu hiyo si PR kwa Israeli, na kwamba wafanyakazi wa Waziri Mkuu hawakuruhusiwa kukagua baada ya production kukamilika.
Kwa upande wa Rwanda, pamoja na kutembelea vivutio mbalimbali, pia Rais Kagame alipata fursa ya kueleza kuhusu mambo mbalimbali likiwemo la tuhuma za kung’ang’ania madarakani. Siku kadhaa baada ya kuzinduliwa, ilioneshwa katika eneo la umma huko Rwanda.
Hii ni trailer ya The Royal Tour iliyomshirikisha Rais wa Rwanda, Paul Kagame mwaka 2018
Hii ni trailer ya The Royal Tour iliyomshirikisha Waziri Mkuu wa Poland, Mateusz Morawiecki mwaka 2019
Hii ni trailer ya The Royal Tour iliyomshirikisha Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu mwaka 2014