SoC03 Ufanisi na uthabiti katika mambo madogo (msingi/awali)

SoC03 Ufanisi na uthabiti katika mambo madogo (msingi/awali)

Stories of Change - 2023 Competition

Vincent Nestory

New Member
Joined
Jun 9, 2023
Posts
2
Reaction score
1
Utangulizi
Neno “Utawala Bora na Uwajibikaji” huonekana kulenga shabaha yake katika utendaji wa uongozi na mamlaka za “juu” katika Taifa, Bara na Dunia kwa ujumla; na mtazamo huu ndio kikwazo kikubwa zaidi cha kufikia utawala wenye sifa ya kuitwa “bora” na uwajibikaji wenye maendeleo chanya. Hii inachangiwa na dhana iliyo ndani ya wanadamu wengi kuona mafanikio ni mambo yenye sifa na picha kubwa tu, huku wakisahau kuwa “kila jambo lililofanikiwa ni mkusanyiko wa mafanikio mengi madogomadogo”.

Fikiri kuhusu chakula kitamu ulichowahi kula hotelini, nyumbani ama kwa mama lishe.
Tazama watu wafuatao;
1. Mkulima mwenye ustadi, mbegu bora, mazao mazuri.
2. Mtunzaji wa mazao mwenye weredi.
3. Opareta mwenye ujuzi wa mashine bora za kuchakata zao ghafi kuwa zao lifaalo kutumika.
4. Msafirishaji wa mazao ghafi na mazao kamilifu.
5. Mpishi mwenye uzoefu.
6. Msimamizi wa vyanzo bora vya nishati,mazingira safi na afya ya mlaji.

Hawa wote ndiyo huamua chakula kiwe vile ulivyokiona.

Uzembe mdogo tu katika utunzaji ama usafiri ungefanya chakula kiwe na michanga au punje hatarishi nyinginezo ambazo kwa hakika zingeondoa ubora wa chakula hicho.

Kila mtajwa hapo juu hufanya kwa UFANISI na UTHABITI kazi aliyonayo bila kuwaza mtendaji mwingine atafanya badala yake, yaani mtunza mazao hasemi “acha niyaweke kwenye mazingira machafu kwa sababu mpishi ataosha kwanza kabla ya kupika” HAPANA, yeye hupambana kwa hali zote ili yawe bora ingawa hajui mlaji ni nani, ni kana kwamba anasema “acha niwe mshumaa uwakao, nitie nuru katika eneo hili bila kujali anayefaidika ni nani.” Na hivyo ndivyo utawala bora na uwajibikaji hupaswa kutazamwa.

Kila mwanajamii anapaswa kuwajibika na kutenda kila jambo kwa UFANISI na UTHABITI haijalishi ni dogo kiasi gani na nani anaona huku akijua ya kuwa yeye mwenyewe ni kiongozi wa maisha yake na ya jamii inayomzunguka.

Vyeo na Madaraka ni kama “Jua” na haifai kutegemewa kipekee kama vyanzo vya “nuru” kila sehemu na kila wakati, kuna sehemu zenye uvuli, Nyakati za giza kadhalika usiku pia katika maisha ya jamii na taifa kwa ujumla.

Hivyo basi, Watanzania, Waafrika na Taifa lolote linalowaza kuinua Utawala Bora na Uwajibikaji ni lazima tugeuze mtazamo wetu kutoka kwenye “Kuwa Jua” hadi “Kuwa mshumaa uwakao. Kwanini?

Hoja namba 1;
Jua ni chanzo cha mwanga cha asili na utendaji wake hauathiriwi na mabadiliko ya maisha ya viumbe vitumiavyo nishati yake.

Mtazamo sahihi:
Kiongozi bora sio lazima azaliwe na karama ya uongozi ndani yake bali anaweza kujifunza uongozi huku akisukumwa na uzalendo wa kweli nafsini mwake na hatimaye kupambana na changamoto za jamii yake zinazobadilika kila siku.

Hoja namba 2;
Jua halina mbadala na nishati yake haiwezi kutumika kuunda jua lingine.

Mtazamo sahihi:
Viongozi bora na wawajibikaji wanapaswa kuwa mfano na waandaaji wa viongozi bora chipukizi na haifai kusemwa “hakuna kama yule” au “hatotokea mfano wa kiongozi kama Mwl.J.K Nyerere na Mh.J.P Magufuli”.

Hoja namba 3;
Jua linapatikana mchana hivyo usiku sio wakati sahihi kufanya yale tuyafanyayo mchana

Mtazamo sahihi:
Viongozi bora hawapaswi kudhaniwa kuwa ni kitu cha msimu na nchi haitakiwi kusubiri miujiza ya kutokea kiongozi mwingine mwenye chachu ya maendeleo kama yule aliyepita. “Taifa hupiga hatua kila siku, aidha mbele au nyuma kulingana na aina ya utawala ulioshika hatamu zake.”

Hoja namba 4;
Jua liko mbali sana na viumbe hai na ni ngumu ama haiwezekani kulifikia.

Mtazamo sahihi:
Utawala bora na unaowajibika haupaswi kuwa mbali na wananchi wake na usiofikika kimawazo na mashauri ili kuboresha utendaji wake.

Hoja namba 5;
Utendaji kazi wa Jua haueleweki kibinadamu, dhana za kitaaluma pekee hujaribu kuelezea jambo hilo

Mtazamo sahihi:
Utendaji kazi wa viongozi wenye utawala bora na uwajibikaji haupaswi kuwa wa kufikirika ama usioeleweka kwa wananchi wake; mapendekezo na makubaliano yanapaswa kujadiliwa kwa uwazi, ukweli na unyoofu.
“Haifai kumtazama kiongozi kama mwana-mazingaombwe, mtu mwenye kubahatisha ama kutenda bila mipango thabiti ya utekelezaji". Nini kitatokea endapo kila mmoja wetu atakuwa na mtazamo wa mshumaa uwakao? Giza litaondolewa.

Hapa nitaongelea giza 3 mioyoni mwa watu katika safari ya utawala bora na uwajibikaji.

1. ”Hakuna siasa safi, kila kiongozi lazima ajali maslahi yake binafsi kisha aangalie yale ya wanachi
Viongozi wengi wamehusishwa na “Rushwa, Ufisadi, Mikataba isiyo na tija kwa wananchi” baadhi yao kwa kulaghaiwa na ulimbukeni lakini wengi ni mtazamo wa “jua” wakihisi watatawala milele na kufaidika daima.
Hii itaondoka endapo kila mmoja wetu atajua “yeye ni nuru ya Dunia kwa kitambo tu” kama mshumaa uwakao na “fedha na mali matokeo ya uwajibikaji wa mtu ipasavyo.”

2. ”Sio kila elimu ni ufunguo wa maisha hususani elimu ya darasani”
Waliosoma hawajaajiriwa, walioajiriwa hawajasoma
, je tukate tamaa kuhusu elimu kama njia kufikia utawala bora na uwajibikaji? HAPANA. Nini kifanyike?

i. Ni lazima wanafunzi tukubali kusoma kwa malengo ya kuelewa kwa undani na kutumia tunachokielewa kama nuru ya jamii, kinyume na hapo hata mitaala mipya haitatusaidia kutatua changamoto zetu. Tuna MAKISATU na COSTECH kama vichocheo, tuvitumie ipasavyo.

ii. Walimu na wanafunzi sote tuwe na uzalendo huku tukijua taifa la sasa na la kesho linategemea maarifa yetu kusonga mbele. Inatupasa kuitazama mifumo bora iliyopo kama CBET ili kutia chachu hapa.

3. ”Kila kitu hutokea chenyewe katika mpangilio fulani,mwanadamu hawezi kubadili wala kuingilia utendaji wa mfumo huo”
Kuamini kuna mtu au miujiza itafanya majukumu yako ni njia nzuri ya kudidimiza utawala bora na uwajibikaji.

Jua {Madaraka/Vyeo} limetuaminisha ukianika nguo itakauka hata kama umelala, mwenye busara hatolala maana anajua mabadiliko ya hali ya hewa hutokea muda wowote. Amka Mtanzania, Mwafrika mwenzangu
Utayari
• Ubunifu na
• Uchapakazi

vitumike katika kila jambo, wewe na mimi tufanye kazi kama mishumaa iwakayo tukijua mafanikio yetu ni mnyororo wa utendaji kuanzia chini kabisa kwa raia katika mambo madogomadogo hadi juu kabisa kwa kiongozi wa jamii na nchi kwa ujumla.

Hitimisho
Andiko hili sio maneno ya hamasa wala onesho la ubunifu, bali ni wito kwa kila asomaye kutambua nafasi yake na mchango wake katika maendeleo ya pamoja huku akiwa tayari kufanya kwa UFANISI na UTHABITI mambo yote yanayomzunguka akijitazama kama kiongozi wa maisha yake binafsi na wa jamii yake. Mama Theresa {1910-1997} aliwahi kusema “vitu vidogo vitabaki kuwa vidogo, lakini kuwa mwaminifu katika vitu vidogo ni kitu kikubwa.”

Marejeo;
Chanzo: Tovuti ya www.google.com
 
Upvote 1
Back
Top Bottom