Ukataji Wa Midomo
Ukataji wa kuku midomo ni hatua muhimu sana ambayo mfugaji lazima aipitie.Kazi ya ukataji wa midomo inapendekezwa ifanyike kabla kuku hawajaanza kutaga.
Kwa kawaida kuku huanza kutaga wanapofikia umri kati ya wiki 19 na 20 toka kuzaliwa. Kuku watatakiwa wakatwe midomo watakapokuwa na umri wa wiki 15. Kama wataanza kudonoana mapema zaidi kabla ya umri huo kufika, basi wakatwe midomo yao mapema zaidi kadri iwezekanavyo.
Sababu zinazochangia kuku kudonoana ni pamoja na mlundikano mkubwa wa kuku kwenye chumba kimoja, upungufu wa madini na vitamini kwenye chakula, vyombo vya chakula na maji kuwa vichache, mwanga mkali kupita kiasi kwenye mabanda ya kuku na wadudu mfano, utitiri, chawa na viroboto. Tatizo hili pia linachochewa na unyonyokaji wa manyoya (moulting) unaoambatana na utokaji damu ambayo huwavutia kuku na hivyo kuwafanya waanze kudonoana wao kwa wao.
Ili kudhibiti tatizo hili kutokea, mfugaji anashauriwa kuku wake, wakati wa mchana, waning'iniziwe majani au mboga kama vile chainizi, wapewe pia dawa zenye vitamini kwa wingi mfano, Egymycine, multivitamin, amin'total na vitalyte. Pia wawekewe bembea ambayo kuku watatumia kuchezea. Hiyo yote ni kuwafanya kuku wawe bize na hivyo kuwasahaulisha na kudonoana wao kwa wao.
Tatizo la kuku kudonoana iwapo mfugaji hatowahi kulidhibiti mapema atasababisha kuku wengi wafe na kuwafanya pia kuku wanaotaga washindwe kutaga kutokana na mshituko wa vidonda vya kudonolewa.
Ukizingatia kwa umakini yote yaliyoelezwa, hutapata shida kwenye ufugaji, kuku wako watakuwa wazuri na wachangamfu pia vifo havitakuwepo na hivyo utaweza kunufaika na kazi ya ufugaji.