Kwa mujibu wa Mhadhiri Mwandamizi kutoka Idara ya Sayansi ya Wanyama ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUAambaye pia ni mtaalamu wa lishe ya samaki na uzalishaji Dr. Berno Mnembuka, ili kujua aina za vyakula vya samaki ni lazima mfugaji ajue tabia za ulaji wa samaki, tabia hizo zipo katika makundi 3.
Kundi la kwanza ni samaki wanaokula nyama, hili ni kundi linalonufaika na vyakula vilivyo na asili ya nyama, mfano wa samaki waliopo kwenye kundi hili ni pamoja na sangara na kambale.
Kundi la pili ni samaki wanaokula mimea vipando kwa mfano samaki aina ya ‘carps’. Kundi hili la samaki ustawi wake hutegemea vyakula vilivyo na asili ya mimea vipando kwa maana ya masalia ya mabaki ya mazao ya mashambani na mazao ya bustani.
Kundi la tatu ni samaki wanaokula vyakula mchanganyiko kama perege, sato na mwatiko (samaki wa maji chumvi). Kundi hili la samaki hutegemea zaidi upatikanaji wa vyakula vyenye asili ya nyama na mimea.
Baada ya kuyaangalia makundi hayo matatu ya tabia za ulaji wa samaki, sasa tuangalie aina za vyakula vya samaki. Kuna aina mbalimbali za vyakula vya samaki kama anavyotueleza mtaalamu wa lishe ya samaki na uzalishaji Dr. Mnembuka.
Aina ya kwanza ya chakula cha samaki ni mabaki ya nafaka ambayo yanahusisha pumba za mahindi, ngano na mpunga. Hapa mtaalamu huyu anawataka wafugaji kuchukua tahadhari pindi wanapotumia pumba za kununua kwa sababu wakati mwingine pumba zinazotokana na nafaka hizo huwa na dawa(sumu ya kuulia wadudu) ambayo iliwekwa wakati nafaka hizo zinahifadhiwa, dawa hizo zinaweza kuleta madhara kwa samaki hivyo cha msingi ni mfugaji kuwa na chanzo cha uhakika cha kupata pumba hizo.
Aina nyingine za vyakula vya samaki ni pamoja na dagaa, damu iliyokaushwa, unga wa mifupa, machicha ya pombe, mboga mboga (kama vile tembele, mchicha na kabichi), matunda (kama maembe na ndizi zilizoiva sana), chumvi na chokaa.
Ili mfugaji aweze kujua namna ya kuchanganya vyakula hivyo hana budi kuwasiliana na wataalamu kwa kuwa mchanganyiko wa vyakula hivyo unategemea aina ya samaki, umri wake na hali yake kwa mfano samaki mzazi mahitaji yake ni tofauti na samaki wengine.
Muongozo wa mahitaji ya viinilishe vya samaki
Kwa ujumla samaki huhitaji viini lishe vile vile ambavyo wanahitaji wanyama wengine, viini lishe hivyo ni protini, wanga, mafuta, madini na vitamini. Mpaka sasa kuna aina 210 za samaki wafugwao ambapo kwa mujibu wa Dr. Berno Mnembuka,Mhadhiri Mwandamizi kutoka Idara ya Sayansi ya Wanyama SUA, muongozo wa kutayarisha vyakula vya samaki hao ni lazima uzingatie viwango vifuatavyo;
(i) Vyakula vyenye asili ya wanga viwe kati ya wastani wa asilimia 20 hadi asilimia 25
(ii) Vyakula vyenye mafuta viwe kati ya wastani wa asilimia 10 hadi asilimia 15
(iii) Vyakula vyenye vitamin viwe kati ya wastani wa asilimia 1 hadi asilimia 2
(iv) Vyakula vyenye madini viwe kati ya wastani wa asilimia 1 hadi asilimia 2
(v) Maji – hapa ifahamike kuwa wakati tunazunguzia viwango vya maji vinavyohitajika kwa wanyama wengine wafugwao, hitaji la maji kwa samaki ni ubora wa maji anayofugiwa na sio wingi wake.