Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
- Thread starter
- #41
LEO tutazungumzia ugonjwa wa kisonono ambao umekuwa kama umesahaulika katika jamii ila ni kwamba upo na uambukizo upo kwa kiasi kikubwa sana na wenye hatari kubwa ya kuambukizwa ni wanawake.
Wanawake wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuambukizwa ugonjwa wa kisonono kwa asilimia 80, huku wanaume wakiwa katika hatari ya kupata ugonjwa huo kwa asilimia 20 tu.
Dalili
Dalili za ugonjwa huo huwa hazijitokezi kwa uwazi kwa wanawake ikilinganishwa na wanaume na pia ugonjwa huu una madhara zaidi kwa wanawake kwani huweza kuwaathiri watoto walio tumboni kwa wajawazito na anapojifungua. Hayo yote yanaonyesha umuhimu wa kutibiwa ugonjwa huo mapema.
Madhara
Moja ya madhara anayoweza kupata mtu kutokana na ugonjwa wa kisonono ni mwanamke kutoweza kuzaa yaani kuwa mgumba au mimba kutoweza kutunga. Inajulikana kuwa magonjwa ya zinaa ya Chlamydia na kisonono yana mchango katika
kusababisha wanawake kutozaa kwani magonjwa hayo kwa asilimia 15 huweza kusababisha uvimbe kwenye kizazi na hasa kwa kuwa wanawake wengi wenye kisonono huwa hawaonyeshi dalili.
Kwa upande wa wanaume ugonjwa wa kisonono pia huweza kuwafanya wasipate watoto kwani huwasababishia uvimbe katika sehemu ya mbele ya korodani ambako
mbegu za kiume hutengenezwa. Uvimbe huo usipotibiwa husababisha utasa.
Ugonjwa wa kisonono au gono pia huweza kuathiri moyo, ubongo, ngozi na kadhalika
kwa hivyo ni hatari kwa mtu yeyote aliyeambukizwa kutokutibiwa mapema.
Pia ugonjwa huo huleta madhara au uvimbe kwenye maungio ya viungo, ambapo vimelea vinavyosababisha kisonono huweza kusambaa kwenye damu na kuleta
maambukizo kwenye sehemu nyinginezo mwilini. Maambukizo hayo huleta homa, vipele, vidonda kwenye ngozi, maumivu ya viungo na uvimbe. ilevile wanawake ambao ni wajawazito walioambukizwa ugonjwa huu wako kwenye hatari ya mimba kutoka au kuzaa mapema kabla haijatimiza umri wake (preterm labor).
Kwa wale wanaoambukizwa kisonono kipindi cha kukaribia kujifungua, wanaweza kuwaambukiza watoto wao na hivyo watoto kupata ugonjwa wa uti wa mgongo (meningitis), kuwa vipofu, homa ya mapafu (pneumonia) na ugonjwa wa mifupa (septic arthritis).
Kinga
Unaweza kujikinga na gonjwa hili la zinaa kwa njia zifuatazo. Kwanza kabisa ni kuwa mwaminifu katika ndoa na kujiepusha na uasherati. Kuchukua tahadhari na kuzungumzia
juu ya ugonjwa huo na dalili zake ili kuweza kufahamu kuwa mshirika wako wa ngono ana ugonjwa huo au la na iwapo anao hatua inayofuata ni kutibiwa na kupata ushauri wa daktari.
Njia nyingine ya kujikinga ni kuepuka kufanya ngono na mtu aliyeambukizwa gono. Vilevile kutumia mipira (kondom) wakati wa kujamiiana na wanawake wajawazito
wanapaswa kuhakikisha kuwa wanahudhuria kliniki mapema ili waweze kuchunguzwa na kupatiwa tiba muafaka iwapo watagundulika kuwa na ugonjwa wa kisonono au ugonjwa mwingine wowote.
Wajawazito wanashauriwa kujifungua hospitalini ili kama mtoto ameathirika na kisonono apate matibabu ya haraka baada ya kuzaliwa ili kuepusha kuwa kipofu na madhara mengine.
Matibabu na ushauri
Tiba ya ugonjwa wa kisonono inahusishwa na tiba ya ugonjwa wa Chlamydia kwani mara nyingi magonjwa haya mawili ya zinaa huambatana pamoja.
Matibabu ya kisonono pia hutegemea umri wa mgonjwa. Kisonono ambacho si sugu kilicho kwenye shingo ya kizazi (cervix), urethra na puru, hutibiwa kwa dawa za
Cephalosporin, ambapo mgonjwa hupewa dozi moja ya dawa hizo pamoja na dawa aina ya Macrolide kwa mfano Azithromycin na za jamii ya Penicillin kwa mfano Doxycyclin kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa Chlamydia.
Mara nyingi kwa wagonjwa walio na umri wa chini ya miaka 18 na wajawazito, hutibiwa kwa kuchomwa sindano. Mgonjwa hutakiwa kufuata ushauri wa daktari kabla ya kutumia dawa hizo kwani nyingi huwa na madhara kwa wajawazito kwa mfano Doxycyclin.
