Kivuko cha Mv.Nyerere kilichozama huko Mwanza jana kinadaiwa kilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 100 tu lakini kilizidisha karibu mara tano ya uwezo wake. Kuna "mazwazwa" wameanza kukwepesha lawama kwa serikali na kuanza kuwabebesha mzigo wafanyakazi wa kivuko hicho eti ni kwanini waliruhusu abiria kuzidi.!
Kuna mambo matano ambayo "mazwazwa" hao wanayakwepa ama makusudi au kwa udogo wa akili zao.
#Mosi; Kama abiria walizidi, serikali haiwezi kukwepa lawama. Mamlaka za usimamizi wa safari za majini zilikua wapi? SUMATRA na watu wa bandari waliruhusuje abiria kuzidi kiwango? Na kwa hali inavyoonesha hii si mara ya kwanza kwa kivuko hiki kuzidisha abiria. It seems ni jambo la kawaida. TPA wapo, SUMATRA wapo, Polisi wapo, wote wanaangalia tu. Baada ya maafa ndipo kila mmoja anajaribu kujitoa kwenye lawama.
Kwa vyovyote serikali kupitia mamlaka zake inapaswa kuwajibika. Nilitegemea RPC Mwanza, Mkuu wa kikosi cha zimamoto na uokoaji, Mkuu wa bandari ya Ukara, Meneja wa SUMATRA Mwanza, RC Mongela, DC Ukerewe, Waziri wa uchukuzi wawe wameshajiuzulu kama sehemu ya kuonesha uwajibikaji. Lakini zimebaki porojo za kutupiana lawama tu. At the end dereva wa kivuko hicho na wafanyakazi wale wa ngazi za chini ndio watatolewa mhanga, ili kufunika kombe. What a shame?
#Pili; Pamoja na abiria kujaa lakini kivuko cha Mv.Nyerere kilikua kimeshachakaa sana. Kwa miaka mingi kimekuwa kikilalamikiwa kutokana na uchakavu wake. Na kabla hakijazama, kimewahi kusababisha dhoruba kadhaa kikiwa majini. Mwaka 2016 kilizima katikati ya ziwa na kuanza kwenda mrama (bila uelekeo). Mafundi waliokuwepo kwenye kivuko hicho wakasaidiana kufanya matengenezo kikatengemaa na safari ikaendelea. Hata hivyo hii haikua mara ya kwanza kwa kivuko hicho kuzima katikati ya maji. Imewahi kutokea mara kadhaa na kuripotiwa, lakini nani anayejali?
Mbunge wa Ukerewe Mhe.Joseph Mkundi amewahi kulalamikia mara kadhaa uchakavu wa kivuko hicho na kuomba kifanyiwe marekebisho makubwa au kinunuliwe kingine lakini serikali haikumsikiliza (labda kwa kuwa ni kutoka upinzani). Leo serikali inataka kuondolewa kwenye lawama hizi. How?
#Tatu; Huduma ya uokoaji bado ni ya kiwango cha chini sana. Kivuko kimezama just mita 100 kabla ya kutia nanga, lakini watu wameshindwa kuokolewa. Tangu maafa ya Mv.Bukoba yatokee miaka 22 iliyopita Serikali haijajifunza, wala haijajiandaa kukabiliana na majanga kama haya? Hakuna boti za uokozi, hakuna wazamiaji, hakuna teknolojia ya kisasa za uokoaji, lakini mbaya zaidi hakuna hata taa. Ni aibu na inatia kinyaa. Nchi yenye uhuru miaka karibu 60 inakosa taa za kumulika just mita 100 majini?
Jana serikali ilisimamisha zoezi la uokoaji baada ya kukosa taa. Yani ni kama vile iliruhusu manusura waliokuwa wamesalia ziwani hadi majira ya jioni wafe kwa sababu hakukua na taa za kwenda kuwafuata. Waokoaji wakaruhusiwa kwenda kulala majumbani kwao, huku manusura wakihangaika peke yao ziwani bila msaada wowote na wengine wakipoteza maisha.
Leo serikali imekuja kuokota maiti za watu walewale iliowatelekeza jana kwa kuogopa giza. Halafu kuna watu wanasema ajali ni mipango ya Mungu. Hivi hata kutelekeza manusura ziwani kwa kukosa taa ni mipango ya Mungu? Hivi kukosa hata vikosi vya uokoaji ni mipango ya Mungu? Hivi kukosa vifaa vya kisasa vya uokoaji kama boti na Helcopter ni mipango ya Mungu? Hebu kuweni serious kidogo.!
#Nne; Kwa mujibu wa taarifa ya bunge, kivuko hiki kilikua kinahudumia watu 50,000 wakazi wa Bugolora na Ukara. Uwezo wake ni kubeba tani 25 tu sawa na abiria 100 na magari 3 kwa wakati mmoja. Lakini mara zote kimekuwa kikizidisha uzito kutokana na demand kubwa ya wasafiri. Hata jana kilipozama kinadaiwa kilikua na abiria karibu 400 na magunia 100 ya mahindi, yani karibu mara 5 ya uwezo wake.
Kichekesho ni kwamba eti serikali inashangaa ilikuaje kivuko hicho kikazidisha watu kiasi hicho. Yani watu 50,000 wanahitaji huduma ya usafiri then mnawapelekea kivuko cha watu 100 halafu mnashangaa kimezidishaje abiria? Kwani hili linahitaji degree ya uchumi kujua demand ilizidi supply?
Mahitaji yanapokua makubwa kuliko huduma lazima mtoa huduma azidiwe. Hili eneo lilikua linahitaji vivuko angalau viwili vyenye uwezo wa kubeba abiria 800 kila kimoja. Lakini mmewapelekea kivuko cha kubeba watu 100 tu halafu mnashangaa kwanini kimezidisha abiria. Hivi mko serious?
#Tano; Yamekuwepo madai ya muda mrefu kuwa serikali inatumia pesa kwenye mambo yasiyo na tija na kuacha mambo ya msingi yanayogusa maisha ya wananchi. Kuna madai ya kushawishi wabunge na madiwani kuhamia CCM katika kile walichokiita "kuunga mkono juhudi" za serikali.
Taarifa ya Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC) inaeleza kuwa gharama za kurudia uchaguzi jimbo moja ni Bilioni 1, na udiwani kata moja ni Milioni 30 hadi 45. Hadi sasa kuna wabunge watano waliojiuzulu kuunga mkono juhudi (Kinondoni, Siha, Monduli, Ukonga na Liwale). Hizi ni Bilioni 5 zimepotea kurudia uchaguzi. Na kuna kata zaidi ya 100 zimerudia uchaguzi baada ya madiwani wao kuunga mkono juhudi. Hizi ni bilioni tatu na nusu.
Jumla ya pesa ambazo serikali imetumia kurudia uchaguzi kwa kigezo cha madiwani na wabunge "kuunga mkono juhudi" ni karibu bilioni 9 hadi sasa. Hizi ni zile zilizotolewa moja kwa moja na NEC kwa ajili ya kuchapisha karatasi za kura na kuwalipa wasimamizi wa uchaguzi. Bado hazijajumuishwa gharama za vyama vya Siasa kufanya kampeni.
Bilioni 9 zilizochezewa na NEC kwenye chaguzi za marudio, zingetosha kabisa kununua kivuko kikubwa na cha kisasa kama hiki cha Mv.Kazi (pichani). Hiki kina uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 200 kwa wakati mmoja. Kilinunuliwa kwa shilingi Bilioni 7.5 za kitanzania.
Yani bilioni 9 zilizochezewa kwenye uchaguzi na kuwarudishia ubunge watu walewale waliojiuzulu, zingetosha kununua kivuko kikubwa kama hiki cha Mv.Kazi kikapelekwa Ukara. Kingesaidia kubeba watu wengi zaidi na kuepusha maafa yaliyotokea. Lakini kwa kuwa kupanga ni kuchagua, tuliona watu kuunga mkono juhudi ni jambo la muhimu zaidi kuliko "kusave" maisha ya ndugu zetu wa Ukara na maeneo mengine ya nchi.
Ni kama vile maisha ya watanzania sio muhimu sana kama kuchezea pesa kwenye "zugazuga ya demokrasia" iitwayo marudio ya uchaguzi. Bado tuna safari ndefu sana.!