Basi tulipofika getini walitushusha na kutuambia mnaweza kwenda sasa.
Ilikuwa yapata saa kumi za usiku, tuliporejea kutoka chini ya ardhi. Kusema kweli nilipofika juu ya ardhi nilihisi utofauti mkubwa mno, maana nilianza kupigwa na baridi kali, hali ya hewa nzito na changamoto nyingi tu.
Basi Misoji akaniambia unaweza kwenda nyumbani sasa, usimwambie mtu jambo uliloliona kwa sasa maana wanaweza kuanza kuniita mimi mchawi. Ndio maana huwa tunakuja huku usiku watu wasiweze kutuona. Ufahamu wa watu wengi umefingwa ni vigumu sana kukuelewa. Mpaka utakapopata mafunzo kadha wa kadha ndio utaweza kufungua geti hilo hata mchana.
Kisha akaniambia unatakiwa sasa ujiandae, kwaajili ya kuanza mafunzo. Kumbuka ulichoambiwa usisahaau hata kimoja.
Tuliweza kuagana nami nikarejea nyumbani kwetu na yeye akarejea kwao.
Asubuhi tuliamka nikiwa natafakari sana, kwamba kile kilichotokea ni ndoto au ni uhalisia? Maana kwenye ule mbuyu hakuna hata dalili yoyote ya kuwa na mlango. Hali yangu ya kila siku ikaendelea kuwa vilevile. Nikawa nawaza kwanini sasa asingeniacha tu huko? Nilikuwa na mawazo mengi sana. Na mawazo hayo ilibidi nikae nayo ndani ya moyo wangu maana hakuna mtu wa kuweza kumuelezea isipokuwa huyo Misoji tu.
Yapata kama saa kumi hivi kulikuwa na mashindano ya mpira wa miguu hapa kijijini kwetu, timu ya Amaboko na timu ya Amagulu zilikuwa zinashindana. Nilijisogeza pale ili anagalau kupunga upepo na kupunguza mawazo mengi ndani ya kichwa changu.
Nilimuona Misoji kwa mbali akiwa na wasichana wenzake wakiwa na furaha, wakipiga soga za hapa na pale. Wao walikuwa wakiishangilia timu ya Amagulu wakati mimi nilikuwa ni mpenzi wa timu ya Amaboko. Timu ya Amagulu walikuwa na mshambuliaji mmoja hatari aliyejulikana kwa jina la Klementi. Huyu jamaa alikuwa na uwezo wa kupiga mpira kwa kutumia miguu yote.
Klementi alikuwa na miguu yenye matege, ni mrefu kiasi fulani na pia alikuwa na kichwa kikubwa. Watu wengi sana walikuwa wanampenda maana alikuwa anajua kupiga chenga na kufunga. Klementi akiukamata mpira ni vigumu sana kumnyang'anya. Timu ya Amagulu ilikua hatari sana kutokana na huyo jamaa. Ndio maana wanawake wengi walikuwa wakiishabikia timu hiyo.
Amaboko ni timu ya muda mrefu ilikuwa na utamaduni wa kushangili kwa kupiga ngoma kubwa kubwa. Ngoma hizo zilikuwa zikipigwa watu wa vijiji vingine waliweza kuzisikia. Vijana wa maridadi, wanaojua kucheza ngoma, walikuwa wakinengua huku midundo ya ngoma hizo zikipigwa.
Amaboko iliweza kujizolea mashabiki wengi kutokana na aina ya upekee wao wa kushangilia. Mimi mwenyewe nilijikuta ni mshabiki wa Amaboko.
Siku hiyo akili zangu hazikuwepo kabisa kwenye shindano. Hata ile hamu ya kuimba nyimbo zetu za Amaboko kwa pamoja sikuwa nayo. Lengo langu lilikuwa japo kidogo niende kuonana na Misoji tuweze kuongea mawili matatu hivi. Kichwa changu kimejaa mawazo nataka kujua hivi yale yaliyotokea ni ndoto au ni kweli? Kwanini Misoji yupo na furaha hivyo! Yeye hawazi?