Kuna asimilia fulani ya imani ya kweli katika kila dini -- hata zile ambazo zinaeneza uongo wa wazi.
Ukweli unaweza kuchanganywa na uongo ilimradi tu uvutie akilini mwa watu wanaopenda kudanganyika na kudanganywa.
Aidha, ukweli halisi wa Mungu haujifichi na wala hauna sababu ya kujificha.
Kanuni ya ukweli ni kudhihirika kama nuru ya adhuhuri, isiyohitaji wala umahiri kuing'amua.
Kanuni ya uongo ni kujificha kama giza la usiku wa manane, linalohitaji kutia maanani ili kupata utambuzi wa ziada ili kubaini kinachoendelea duniani.
Tatizo la wengi sana si kwamba hawaujui ukweli.
Shida ipo kwenye maslahi binafsi wanayohofu yatavurugika iwapo wakiufuata ukweli.
Maslahi (mali, kipato, fedha, familia, marafiki, mazingira, mfumo, mipango fulani fulani, nk)
Shida ipo kwenye utaratibu mpya wa maisha watakaolazimika kuufuata iwapo wakiukubali ukweli huo.
Shida ipo kwenye raha na starehe potofu watakazolazimika kuzivua kwa vile zinakinza ukweli mpya ambao hawana budi kuupokea.
Shida ipo akilini mwao kwamba jamii iliyowazoea wakiwa hivi itawaonaje ghafla tu wakiwa vile.
Shida ipo kwenye utashi wao ambao haujafanya maamuzi ya kina, wakidhani kwamba wana muda wa ziada kesho, ambayo kimsingi haitafika kamwe.